17 December 2010

Heineken Golf kuanza kesho

Na Elizabeth Mayemba

MASHINDANO ya Heineken Golf Challenge yanatarajiwa kuanza kuchezwa kesho katika viwanja vya Lugalo, Dar es Salaam.Akizungumza Dar es Salaam jana, nohodha wa klabu ya Golf ya Lugalo,  Samuel Hagu, alisema maandalizi ya mashindano hayo
yamekamilika kwa kusaidiana na wadhamini wakuu, bia ya Heineken.

"Mashindano haya yataanza saa mbili na nusu asubuhi,  wataanza kucheza wachezaji wa kulipwa na baada ya hapo, watafuatia wachezaji wa ridhaa ambao wapo 100," alisema Hagu.

Alisema mchezo huo utakuwa wa siku mbili, Jumamosi na Jumapili, ambapo kutakuwa na makundi manne, watoto, vijana, wazee na akina mama na wachezaji wa kulipwa.

Hagu alisema kila kundi litatoa washindi wawili na washindi hao, kila mmoja atapata kombe na zawadi ambazo zitatolewa na wadhamini.

Alisema jumla ya viwanja 18 vitatumika katika mashindano hayo.Akizungumzia mashindano hayo,  mwakilishi wa bia ya Heineken,  Jerome Lugemalila, alisema wameamua kudhamini mchezo huo ili kuutangaza kama michezo mingine.

"Gofu ni kama mchezo wa soka, mpira wa kikapu, netiboli na michezo mingine inayojulikana sana, tunataka na mchezo huu nao ujulikane," alisema.
Katika mashindano hayo, bendi ya K-Mond Sound itatoa burudani siku zote za mashindano.

No comments:

Post a Comment