29 December 2010

Fukuto la Katiba mpya

CUF waandamana Dar
*Polisi wawatawanya kwa mabomu
*wenyewe wawapiga chenga ya mwili
*Wawasilisha rasimu yao wizarani


Rabia Bakari na Athumani Mpochi
MABOMU risasi na ving'ora vilitawala baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam jana polisi walipojaribu kuzima
maandamano ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), walioandamana kupeleka rasimu ya mabadiliko ya katiba mpya, Wizara ya Katiba na Sheria.

Kuanzia saa moja asubuhi magari ya polisi namba T 337 AKV na PT 0890 likiwemo gari la upupu yalianza kuvinjari maeneo ya TAZARA na Buruguni kudhibiti mikusanyiko ya wafuasi wa CUF waliopania kuandamana.

Maandamano hayo yalipangwa kuanza saa mbili asubuhi, Buguruni Shell, ambapo hadi kufika saa tatu, kulikuwa hakuna dalili za watu kukusanyika lakini ilipofika saa nne asubuhi magari kutoka makao makuu ya CUF yalipita mitaani kuhamasisha maandamano na kueleza kuwa yataanza saa 4.30 

Akizungumza na gazeti hili, Naibu Katibu Mkuu Bara, Bw. Julius Mtatiro alisema awali waandamanaji waliogopa kujitokeza kwa kuhofia vitisho vya polisi.Matangazo hayo yaliibua morari kwa wafuasi wa chama hicho, na kadri muda ulivyozidi kuyoyoma, idadi yao ilizidi kuongeza ofisi za makao makuu chama hicho maeneo  ya Buguruni.

Wanachama hao walijikusanya makundi huku wakiimba hawaogopi polisi wanataka katiba mpya. Ilipotimu saa 4.45, walianza kuingia barabara ya Uhuru kwa ajili ya kuanza maandamano hayo huku polisi wakitoa matangazo ya kuwasihi kuacha kuandamana, kwani wanaweza kusababisha vurugu.

Licha ya matangazo ya polisi, lakini wafuasi hao wa CUF hawakutii amri hiyo na kuzidi kuingia barabarani wakiwa na mabango huku moja  likisomeka 'Kikwete muige Karume, katiba mpya ni lazima.' Waandamanaji walitumia barabara ya Uhuru na njia za mitaani ili kutimiza azma yao ya kufika  Wizara ya Sheria na Katiba.

Polisi walilazimika kupiga risasi juu kuwatawanya huku wakifukuzana nao katika mitaa mbalimbali ya maeneo ya Ilala na kufanikiwa kuwakamata watu wanne ambao walidaiwa kuwa ni miongoni mwa waandamaji.

Kutokana na kuzidiwa na idadi ya waandamanaji, polisi ilibidi waongeze magari na askari waliozunguka maeneo yote ambayo walihisi wafuasi wa CUF wangepita.

Majira lilishuhudia polisi wakiwatia mbaroni baadhi ya waandamanaji, akiwemo mwanamke mmoja na mzee aliyekadiriwa kuwa  na umri wa miaka kati ya 70-75 na vijana wawili, na kuwabeba katika  gari la polisi lenye namba PT 1858 na kuwafikisha katika kituo kidogo cha Karume.

Pamoja na heka heka hizo viongozi wa CUF, walifanikiwa kufikisha rasimu ya hiyo wizarani ambapo ilipokelewa na Katibu Mkuu, Bw. Andrew Mhaiki, huku  magari takribani sita ya polisi yakitanda nje ya wizara hiyo , huku mengine yakizunguka mitaa ya Kivukoni.
Bw. Mtatiro alizungumza na waandishi wa habari na kuwafahamisha kuwa utaratibu waliokuwa wamepanga umeshakamilika, licha ya kusikitishwa na vitendo vya jeshi la polisi, vinavyokiuka haki na misingi ya haki za binadamu.

"Nchi hii inaendeshwa kiimla, kulikuwa hakuna sababu kuzuia maandamano ya amani, ambayo msingi wake ni kusimamia demokrasia. Sisi tumeshatimiza wajibu wetu kikatiba, tunashukuru na tutaendelea kupambana kudai demokrasia bila kuogopa polisi kwa sababu polisi nao ni watu kama sisi, ni wenzetu,"alisema.

Aliongeza kuwa rasimu hiyo ya katiba ina kurasa 88, ambapo iliandikwa kutokana na mchango wa mawazo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wadau wa masuala ya siasa na wananchi wengine. Alisema rasimu hiyo itakuwa wazi kwa wadau wote hivi karibuni na mapambano kudai katiba mpya yataendelea.

8 comments:

  1. SASA KUPELEKA KATIBA WIZARANI NDIO POLOSI HAWATAKI? POLISI WANACHEZA! MNAWANDALIA CCM KABURI. ACHENI WATU WAANDAMANE. NDANI YA MIAKA MITANO HII, TUTASHUHUDIA MAJENGO YA SERIKALI YAKICHOMWA MOTO, NGOJA TUONE. ACHENI WATU WAANDAMANE WAKIHOKA SI WATALALA? MMEWACHOKOZA WAJINGA WATANZANIA WALIOWACHAGUA, MTALIPIA.

    ReplyDelete
  2. utawala usio bora lazima ndivyo uwe mpaka mabomu na risai. wewe polisi unalipwa kidogo eti unatoka na mabomu kumuua ndugu yako. unaacha vigogo wanakula

    ReplyDelete
  3. mimim ninaona cuf suala la katiba wanakurupuka halikuwapo katika ajenda zao na sasa baada ya kuona CHADEMA wanaungwa mkono wanadandia vitu ambavyo, hawakaa chini kutafakari kwa kina, tuswe vichaa katika hili inabidi tathmini ya kina ifanyike.
    KATIBA inagusa uhai wa taifa mbona wanakuwa na mihemko bila fikara tunduizi katika hilo , nasema nanyi mtakuwa mashahidi hawatafika mbali anayebisha asubiri sitaki nimlazimishe kwa hili,unapoona mwenzako anainuka usiwe na kisirani bali kaa chini na kufikiri kabla ya kutenda,kwa hilo CUF wamechemko hawakuona wenzao wa CHADEMA kupitia MNYIKA walivyojenga hoja?
    acheni ukurupukaji umaarufu haulazimishwi,C UF msitake ndoa yenu ya mkeka na CCM muilete huku upinzani ili kuua uzalendo wa wanafikara mahiri.
    ACHENI KUWA KAMA VICHAA KATIKA KATIBA MNASEMA MNASAMBAZA RASIMU SIFURI KWA WATANZANIA NANI KAWATUMA? HARAKA YENU INATOKA WAPI? NA NINI KINAWAFANYA MUWE NA PUPA KIASI HICHO? JIFUNZENI..
    WANAMAPINDUZI WA KWELI WA UHALISIA NA UKWELI WANAJULIKANA.NYIE ACHENI HIZO PAPARA..

    ReplyDelete
  4. Sasa kweli nimeanza kuamini kumbe wale wachangiaji wengi humu Majira ama wana akili-mgando au ni washabiki HEWA wa Chadema. Chadema ni chama kilojipatia sifa hivi karibuni tu na kinaweza kuleta changamoto poa katika siasa za Tanzania.

    Kilio chetu sote ni maendeleo na mustakabali (future) ya vizazi vyetu. Sote ni watanzania. Iwapo tutafikia malengo yetu hayo kila alieshiriki atastahiki credit.

    Chadema, Cuf,CCM, NCCR, TLP nk, ni moja wa njia za kufikia matakwa ya wanachi. Si vyema kuonesha ubinafsi iwapo suala linalopiganiwa ni maendeleo.

    Akina Mnyika tunawahitaji, pia pressure kutoka katika jamii inahitajika vilevile. Kitendo cha ku discredit mwenzako anaekupigania wewe ulielala mda wote huo ni cha kusikitisha sana.

    Bila ya kuwa na umoja wa wapinzani, demokrasi haiwezi kupatikana kirahisi. Tunaweza tukawa na fikra tofauti lakini madamu lengo letu ni maendeleo, so let be it.

    Mpe credit na motisha kila anaekupigania wewe uliebahatika leo kutoa maoni mtandaoni, alau alieko nyuma kimaendeleo na kukosa uhuru nae afaidi demokrasi ya kweli.

    ReplyDelete
  5. Tusitafute umaarufu kwenye katiba mpya,wapo waliofungwa kwa kupingana na katiba iliyopo toka enzi za Nyerere. Tatizo la Watz si watu wa kujisomea sana na kuelewa mambo ni wavivu wa kusoma. nina wasiwasi kwa niliowaona kwenye tv katika maandamano ya CUF kama kweli wanajua katiba maana yake na hii iliyopo ina tatizo gani,walichofanya ni ushabiki tu wa kisiasa kutokana na viongozi wao kutaka kupata umaarufu kwenye hili la katiba mpya. la muhimu kwanza ilitakiwa ipatikane elimu ya uraia kuielewa katiba maana yake ni nini? na hii iliyopo ina tatizo gani na ikiboreshwa ina faida gani. ni vyema wasomi na wanataaluma kwanza waisome katiba na kuielewa kisha wafanye hayo maandamano hayo ya amani,lakini siungi mkono maandamano ya layman aliyeambiwa na katibu mkuu wa chama chake kuandamana basi naye anafanya na hata ukimuuliza katiba ina kasoro gani atakuambiwa tunaibiwa kura,baas hana jingine kumbe katiba yetu inahitaji mambo mengi yanayo husiana na haki za kijamii. TOENI ELIMU YA URAIA KWA WAFUASI WENU WAILEWE KATIBA NA KISHA MUWABAINISHIE HII ILIYOKO INA KASORO GANI NA TUNAYOITAKA INA FAIDA GANI

    ReplyDelete
  6. kweli tusitafute umaarufu kwenye katiba mpya,katiba iliyopo imepingwa kwa miaka mingi na watu wametiwa jela kwa ajili ya kudai mabadiliko ya katiba toka enzi za Nyerere,pia wapo kina Mtikila nao wameshaonja joto ya jiwe kutokana na kudai malalamiko ya katiba,Mtikila ameisha wahi hata kuingusha serikali mahakamani katika masuala ya katiba,kina mapalala wa cuf enzi zile,kina Seif Sharrif Hamad na wenzake walisota kwa miaka jela.hivyo nyie wajinga wa chadema mnadanganya watu hilo ni hoja ya chadema? tuambieni aliyeteseka na madai ya katiba mpya hapo chadema,kama ni udandiaji ni nyie wajinga wa chadema, jambo la pili hawa vijana walioandamana mimi nawaona ni watu wanaotumiwa tu na viongozi wa kisiasa kufikia malengo yao,maana wengi wao ukiwauliza katiba iliyoko ina tatizo gani atakuambia tunaibiwa kura baas,hawajui katiba ni nini na watanzania wengi hata vijana wetu walioko vyuoni wengi hawaijui katiba ya nchi yetu,hivyo tuache mambo ya kihuni ya maandamano yanaathiri shughuli nyingi za watu,toeni elimu ya uraia inayohusiana na katiba watu waielewe hii ilopo ina tatizo gani na inayokuja ina faida gani,wanasiasa msiwatumie wananchi kama ngazi ya kufikia malengo yenu

    ReplyDelete
  7. Jamani CHADEMA imejifunza siasa kutoka CUF. Hata hivo sina dhamiri ya kuponda chama kimoja dhidi ya chengine, ila inaonyesha wazi hawa member wa Chadema wamechonga midomo mapema sana. Nampongeza aliye comment kuwa hata akina Mnyika tunawahitaji. Kwa hio tuambiane ukweli. Kila aneongea anavuta upande mmoja tu.. Hawa wanaojisemea hivi (biase) HAWAFAI katika dibeti yeyote. Sisi Hatupo katika kutia KURA hapa. Hawa Wanafaa kuongeza fujo mjini.... Tunaomba wanaotoa Hoja wasichangane vyama na Udini penye suala la Serikali. Watanzania Jifunzeni Kuongea, Musiwe wabishi tu... Ndio maana munaibiwa hela zenu kwa kuwa akili yenu ni kwenye Kula, na Kulana wenyewe kwa wenyewe.

    ReplyDelete
  8. NAOMBA JAMBO MOJA MUHIMU SANA TULIZINGATIE. hebu tufikirie suala hili, MOJA TU!! Suala la kuwa Tanzania bado wanatumia siasa za vitisho kwa wanachi wao. Ni Kwa nini? Ni kwa kuwanyima "Uhuru" watu wake. Kwa kweli ni jambo gani Polici kutumia vin'gora na marisasi pakiwa na maandamano amani? Wanajiona sana hawa polisi wa Tanzania!! Si vile alivyowaweka Julius, kuwa wao wawatishe watu tu! Hapana jengine lolote. Ni kuwatia Hofu wananchi ili viongozi wazidi kula..... Tusikubali.

    Ikiwa ni Chadema, CUF, NCCR au CCM ndio aloanza maandamano iwapo ni suala la maendeleo kwa wote, na sio chama kimoja, basi na wengne wote tujiunge kutoa sauti zetu. Tusisahau PEOPLE'S POWER! Hawa viongozi wetu hawataki salama,ndio maana pakitokea jambo lolote wao tia polisi na mabunduki mjini, kamat kamata, piga - wamefundishwa na Chatu wao mkuu - Nyerere. Hizo karne zimepita za utawala wa mabavu na UBINAFSI, Tunataka Tanzania mpya. Kina Mkapa na waliopita wawekwe barazani waonyeshwe vipi nchi zinajengwa. TUAMKENI!!!

    ReplyDelete