Addolph Bruno
FAINALI za mashindano ya kusaka na kukuza vipaji kwa vijana 'Bongo Star Search', zinatarajiwa kufanyika Ijumaa katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Benchmark Production, ambao
ni waandaaji wa kinyanga'anyiro hicho, Rita Paulsen, alisema shindano litaanza saa moja jioni na kumalizika saa sita usiku.
Alisema fainali hizo zitarushwa na kituo cha televisheni cha ITV kuanzia saa tatu na dakika kumi usiku kutoa nafasi kwa mashabiki watakaokosa nafasi ya kuhudhuria ili waweze kushuhudia na kujionea utaratibu utakavyokuwa.
Alisema kwa watakaoingia ukumbini, tiketi zimegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza la viti maalumu (VIP), zitauzwa kwa sh. 45,000 na la pili viti vya kawaida zitauzwa sh. 20,000.
Alisema tiketi zinapatikana katika maduka yote ya Shear Illusion, Big Respect, Ofisi za Benchmark Production na katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ambako fainali hizo zitafanyika.
Rita alisema fainali za mwaka huu zitapambwa na burudani nyingi za muziki mchanganyiko kutoka kwa wanamuziki Diamond, Mh. Temba na Chege kutoka TMK Wanaume, Mwasiti, John Makini, Marlaw, Kibonde na mwanamuziki Cindy kutoka Uganda.
Kwa upande wake Meneja wa bia ya Kilimanjaro ambao ni wadhamini wa shindano hilo, George Kavishe, alisema zawadi iliyopangwa awali kutolewa nao itakuwa kama walivyopanga sh. milioni 30.
Alisema mshindi wa pili atazawadiwa sh. milioni 10 na mshindi wa tatu sh. milioni 5.
Aliwataja washiriki walioingia fainali ni Bella Kombo mwenye namba BSS 02, Joseph Payne namba BSS 07, Mariam Mohammed namba BSS 017, James Martin namba BSS14 na Waziri Salum BSS 11.
No comments:
Post a Comment