Na Grace Michael
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Sophia Simba amesema elimu inayotolewa kuhusu madhara ya ukeketaji katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ndio iliyofanikisha kuzima njama za
kuwakeketa zaidi ya watoto 160 wilayani Tarime mkoani Mara.
Hayo aliyasema Dar es Salaam juzi wakati akizungumza na Majira kuhusu suala la ukeketeji na mikakati ya serikali katika kumaliza tatizo hilo linaloendelea mkoani Mara.
Alisema kuwa baada ya wizara kupata taarifa za watoto waliokuwa wakitarajiwa kukeketwa wilayani Tarime ameuagiza uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufuatilia suala hilo.
Bi. Simba alizipongeza asasi za kiraia kwa kushirikiana na serikali kupitia halmashauri mbalimbali kueneza elimu ya madhara na kufichua vitendo hivyo ambavyo ni vya kikatili kwa watoto wa kike.
Alisema kuwa awali matatizo hayo yalifanywa siri kubwa na jamii husika lakini baada ya elimu kutolewa juu ya ukatili huo wananchi wameamka na wameanza kufichua siri hizo.
"Katika hili unaweza ukakuta familia imegawanyika na mara nyingi wanaolazimisha hili ni akina baba na kwa kuwa akina mama ni waoga basi wanaona njia sahihi ni kumtorosha mtoto, lakini serikali bado inaendelea na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha tatizo hili linakoma," alisema Bi. Simba.
Hata hivyo, alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa sheria ya watoto namba 21 ya mwaka 2009 ambayo adhabu yake ni kubwa inayomtaka mzazi au mlezi anayefanya ukatili kwa mtoto wake atalipa faini ya sh. milioni tano au kifungo cha miezi sita itasaidia kupunguza tatizo hilo la ukatili.
No comments:
Post a Comment