10 December 2010

Ajali yaua sita Magu

Na Daud Magesa, Mwanza

WATU sita wamekufa na wengine 48 kujeruhiwa juzi baada ya basi kuacha njia na kupinduka wilayani Magu mkoani Mwanza.Ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Musoma-Mwanza juzi, saa 9:45 katika
eneo la  Kijiji cha Lugeye wilayani Magu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Bw. Simon Sirro alisema basi hilo lenye namba za usajili T 773 ATQ, Nissan Dizel lilikuwa likitoka Musoma kwenda Mwanza lilipindika baada dereva kushindwa kulimudu kutokana na mwendo kasi wake.

Alisema baada ya ajali hiyo kutokea dereva wake, Bw. Ismail John (40) Mkazi wa Nyakato Mwanza, alikimbia na kutokomea kusikojulikana. 

Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mmiliki wa basi hilo, Bw. Apolinary Aloyce (42) linamtafuta dereva huyo.

Bw. Sirro aliwataja waliupoteza maisha kuwa ni kondakta wa basi hilo, Jaronga Orabo (32) na mwanamke mmoja.

Wengine waliokufa ni pamoja na watoto wawili, Namise Ngigwana mwenye umri wa miezi minne mkazi wa mjini Musoma na Malimi Samson mwenye umri wa mwezi mmoja, mkazi wa Pasiansi jijini hapa.

Wengine waliokufa katika ajali hiyo majina yao hayajafahamika ambao ni mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka kati ya 36 na 40 na wanawake wawili. 

Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majeruhi 12 walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu, na wengine 36 walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini
Mwanza.

Hadi jana majeruhi wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hizo walikuwa wameruhusiwa kutokana na hali zao kuimarika kwa vile hawakuwa na majeraha makubwa bali michuko midogo midogo miilini mwao.

Bw. Sirro alisema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na mwendo kasi wa gari hilo kwani baada ya basi hilo kufika katika eneo hilo mahali ambako kuna kona alishindwa kulimudu na hatimaye kuacha njia na kupinduka.

Aliwataka madereva kuendesha magari kwa uangalifu na kufuata sheria ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

1 comment:

  1. Musa Kilulu wa Lugeye Magu Mwanza, Na shukuru kwa hatua za haraka zilizo chukuliwa kwa majeruhi.Pia asante kwa gazeti la taifa la Majira.+255754339733

    ReplyDelete