28 December 2010

CHADEMA yampongeza Jaji Chande

Na Mwandishi wetu

SIKU moja baada ya uteuzi wa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania, Mohamed Chande, kisha kuapishwa jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa pongezi, kikimuahidi ushirikiano, lakini kikitoa tahadhari pia.Akizungumza
na Majira jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. Erasto Tumbo, alisema kuwa chama hicho kinapongeza uteuzi huo na kumtakia heri Jaji Mkuu Chande katika majukumu yake mapya ya kuongoza moja ya mihimili ya dola, mahakama.

"CHADEMA tunatoa pongezi za dhati kwa Jaji Chande kwa kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu...lakini tunaomba uteuzi wake usije ukawa kikwazo na kuturudisha nyuma hasa katika vuguvugu la sasa la katiba mpya...aige mfano wa aliyemtangulia, ambaye aliweka bayana msimamo wake.

"Jaji Mkuu Chande ni mtu mkubwa, atambue kuwa sauti yake ina nguvu na inasikilizwa na watu wengi, tunatarajia atakuwa jaji mkuu makini...lakini pia asiwe tatizo kama aliyepita ambaye alishindwa na kuacha kiporo suala la mgombea binafsi," alisema Bw. Tumbo.

Alisema kuwa suala la mgombea binafsi liliwashangaza Watanzansia wengi baada ya mahakama kushindwa kutoa ufafanuzi wa kikatiba na kisheria ambayo ni majukumu ya mhimili huo, badala yake likarusha mpira kwa bunge kwa kusema kuwa katiba ni suala la kisiasa.

"Kwa kweli hakikuwa kitu cha kawaida, wananchi wamekuwa wakitegemea kuwa mahakamani ni mahali ambako ufafanuzi wa kisheria na katiba wa masuala kama hayo unapatikana.

"Lakini mahakama chini ya jaji mkuu aliyepita ikashindwa na kuacha kiporo suala la mgombea binafsi...tunatumaini Jaji Chande atatuongoza vizuri hasa katika kuelekea kupata katiba mpya," alisema Bw. Tumbo.

3 comments:

  1. CHADEMA muangalie kwa jicho la pili uteuzi huu, maana sio wa kukimbilia kupongeza. Huyu ni mteule wa rais. Uwezekeno wa kufanya matakwa ya serikali ni mkubwa, ukizingatia yaliyoandikwa magazetini kuwa ana uhusiano wa kindugu na mkuu wa usalama wa taifa, mnaowatuhumu kuwahujumu matokeo ya uchaguzi mkuu.
    Mtihani wake wa kwanza ni suala la Katiba. Yetu macho kama sio masikio!

    ReplyDelete
  2. Halafu sasa udini bado unaendelea kwa kasi kubwa tu

    ReplyDelete
  3. mmh, mie nashangaa na uteuzi huu, kwa nini Muhimili huu unateuliwa na Rais na haupigiwi kura na wanamuhimili wenzao kama vile watawala na watunga sheria?aaah kumbe muhimili wa mahakama ulikuwa option nzuri kwa kikwete kuweza kuteua mwanamke kuliko kuwasaidia mafisadi kuteua spika wao.

    ReplyDelete