10 December 2010

Jaydee, Machozi Band kuvamia Morogoro

Na Mwali Ibrahim

BENDI ya muziki wa dansi, Machozi Band inayoongozwa na msanii wa kizazi kipya, Judhith  Wambura ‘Lady Jaydee’ kesho inatarajiwa kuvamia mjini Morogoro kwa ajili ya
kutoa burudani ya nguvu itakayorindima kwenye Ukumbi wa Masuka Royal Village.

Onesho hilo litakuwa la kwanza kwa bendi hiyo inayopiga muziki mchanganyiko katika mji huo wa Morogoro.

Kwa mujibu wa Mratibu wa onesho hilo, Robert Ekerege alisema Dar es Salaam jana kwamba, maandalizi ya burudani hiyo yanakwenda vyema ambapo kupitia onesho hilo, mashabiki watapata fursa ya kupigiwa nyimbo zinazotamba za na bendi hiyo pamoja na zile za Jaydee.

Ekerege aliongeza kuwa sambamba na burudani hiyo, pia kutakuwa na zawadi mbalimbali kutoka kwa wadhamini wa onesho hilo ya Distilleries inayotengeneza kinywaji cha Konyagi na Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, ambapo mashabiki kumi watakaopendeza watapewa katoni moja za Konyagi kila mmoja.

“Pia mashabiki 50 watakaongia wa kwanza wakiwa wamependeza kila mmoja atapewa zawadi ya muda wa maongezi toka Zantel, wenye thamani ya sh. 20,000 pamoja na laini za Zantel”, Alisema.

Bendi ya Machozi inatamba na nyimbo zake mbili za Mtarimbo doro na Nilizama huku, Jaydee naye akitamba na nyimbo mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanya vyema katika medani ya muziki wa kizazi kipya.

No comments:

Post a Comment