23 November 2010

Zain yabadili jina kuwa Airtel.

Na Tumaini Makene.

ILIYOKUWA Kampuni ya simu za mkononi ya Zain Afrika, 'imezikwa' rasmi ambapo kampuni mpya iitwayo Bharti Airtel imechukua nafasi yake na kuzindua nembo mpya, na
kuanzia sasa jina jipya la Airtel ndilo litatumika katika nchi 34 za Afrika na Asia.

Uzinduzi wa nembo hiyo itakayotumika kwa nchi 15 za Afrika zilizokuwa katika mtandao wa Zain na nyingine 19 za Asia, ulifanyika jana Dar es Salaam, ambapo ilielezwa kuwa kampuni hiyo imejipanga kuwaunganisha Watanzania na Afrika kwa ujumla katika dunia ya mawasiliano kwa bei rahisi kadri inavyowezekana.

"Bharti Airtel, moja ya kampuni tano kubwa za mawasiliano ya simu duniani, leo imetangaza kuzindua chapa yake mpya ya kibishara barani Afrika, kwenye nchi 15 ikiwemo Tanzania, kutoka Zain ambayo ilinunuliwa mwezi wa Juni, 2010 sasa kuwa Airtel," ilisema sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari na kuongeza:

"Kuanzia sasa, Airtel ndilo litakuwa jina la utambulisho wa kampuni, Afrika na Asia katika nchi 19 pamoja na bidhaa mbalimbali pia zitabadilishwa, lengo likiwa ni kuweza kuwafikia wateja wote kwa kutumia jina moja imara. Pia huduma za kampuni na bidhaa mpya na kibunifu zitabadilishwa na kushabihiana na chapa ya kibiashara ya Airtel. Huduma ya kutuma na kupokea fedha ya 'ZAP' kuanzia sasa itaitwa 'Airtel Money'.

Akinukuliwa katika taarifa hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Pamoja wa Bharti Airtel Afrika nzima, alisema:

 "Airtel inafikisha kwa pamoja shughuli zetu zote chini ya utambulisho mmoja wa chapa imara na ya kipekee. Tunaweza kuwafikia zaidi wateja wetu zaidi kwa kuendesha kwa utambulisho wa chapa ya aina moja barani Afrika ili kukidhi ahadi yetu ya kutoza viwango na gharama nafuu."

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. Sam Elangalloor alisema kuwa wanadhamiria kuongeza idadi ya wateja wao kwa asilimia 150 barani Afrika ifikapo mwaka 2012 ili kufikia wateja milioni 100 katika bara zima, akisema kuwa ukuaji huo utachochea na kujenga ajira za moja kwa moja, ajira kupitia wadau wa mauzo na usambazaji na hata kuunganisha jamii.

"Sio tu kwamba tutachangia katika maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania, bali pia tutasaidia Watanzania kutimiza malengo yao mbalimbali kupitia mawasiliano ya simu za mkononi ambayo ni bunifu, mahsusi, yenye kupatikana kwa uhakika na yaliyo nafuu," alisema Bw. Elangaloor.

Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel Tanzania, Bw. Sheikh Sarr alisema kuwa mujibu wa ripoti ya Delloite, kwa kuratibiwa na Muungano wa Sekta ya Mwasiliano ya Simu (GSMA), ni asilimia 40 ya Waafrika wote wana uwezo wa kumiliki simu za mkononi na kwa ongezeko la asilimia 10 kwa kila mwaka linaweza kuchangia kuinua pato la ndani la taifa kwa asilimia 1.2 katika nchi zilizoendelea.

"Ni matarajio yetu kuwa simu za mkononi zitakuwa daraja muhimu kuunganisha jamii na teknolojia ili kubadilisha maisha ya watu katika Bara la Afrika kwa ajili ya ubora, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuunganisha watu na ulimwengu," alisema Bw. Sarr.

Ilielezwa kuwa mahitaji ya simu yanaonekana kuongezeka kwa kiwango cha asilimia 25 kwa mwaka na wachambuzi wanabashiri ya kwamba barani Afrika, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara, hadi kufikia mwaka 2013 kutakuwa na ongezeko la watumiaji wa simu za mkononi hadi kufikia asilimia 65, wengi wao wakitokea maeneo ya vijijini.
  

6 comments:

  1. Nimesikitishwa na hatua hii. Kituo cha uwekezaji, Bunge na viongozi watoa maamuzi ni lazima muwajibike kwa hili. Naomba msome na mnielewe watanzania wenzangu. Nafikiri umefika wakati wa bunge na wananchi kwa ujumla kuliangalia suala hili la uwekezaji na katika nchi yetu wakati huohuo kukiwepo na msamaha wa kodi kwa wawekezaji (Tax free holiday) kama motisha kwa umakini mkubwa sana. Sijafanya uchunguzi wa kina kujua kuwa kampuni za mawasiliano zina mkataba gani na serikali juu ya kodi katika kipindi cha mwanzo katika uwekezaji na hivyo wanalipa kodi kwa misingi ipi. Kwa haraka haraka tu katika kipindi kifupi kampuni hii sasa imekua Airtel kutoka Zain na Celtel!??! Kulikoni hapa?? Wachumi na wanasheria mtusaidie katika hili ili kuokoa uchumi wetu tafadhali maana mlisoma kwa fedha za wananchi hivyo ni busara kutumia elimu yenu mtusaidie. Yale yale ya Movenpick, sheraton, Royal Palm n.k. Mwaka 2001 wakati Mh. Abdallah Kigoda akiwa Waziri wa mipango na ubinafsishaji aliulizwa swali na wabunge juu ya "Tax free holiday" kwa wawekezaji; naye alijibu kuwa "Ni bunge hili hili ndilo lililopitisha sheria hiyo" Kwa maneno mengine alikiri upungufu mkubwa uliopo katika sheria hiyo. Sasa tunaendelea na hadithi hizohizo. Tutafika lini jamani?? Serikali yetu inaangalia tu na inaendelea kupiga debe la kuja kwa wawekezaji nchini. Hebu ufike wakati wa viongozi waone haya na aibu na watetee maslahi ya nchi yetu. Inachefua; watu mmesoma na mnaendekeza wizi na hadaa kwa nchi yetu. Hivi Mwl. Nyerere angefanya hivyo, taifa letu lingekuwepo jamani?? Pamoja na Bunge la sasa kuanza kwa mikiki na tofauti za kimtizamo na kisheria, Utaifa unatakiwa utawale hasa kwenye maamuzi yenye maslahi kwa taifa letu. Hatuwezi kuendelea hivi na kuwa kichwa cha mwendawazimu (Tumkumbuke Mzee Ruksa). Wabunge wote mnatakiwa kuliona hili na kulifanyia kazi na kuibadili sheria hiyo maramoja. Tutachekwa hadi lini ndugu zangu. Siasa za halohalo "Za Uswahilini" hazina tija. Historia itatuhukumu kwa vizazi vijavyo. Kwa kifupi, sheria hiyo haifai na ni unyonyaji/ Ukoloni mamboleo. Eeeh Mungu tutasamehe kwani hatujui tulitendalo.

    ReplyDelete
  2. Nakuunga mkono Mtanzania halisia,mchezo huu huu dio uliofanywa kwenye makampuni ya Migodi hapa Tanzania,nasi tunachekelea tu pale viongozi wetu wanapoitwa kuzindua makampuni mapya ymabayo nayo yatapewa tax exemption na huo msamaha wa kodi ukikaribia kuisha wanauzia wengine au wanabadili jina kwani tayari wanakuwa wamechuma vya kutosha na mchezo wa msamaha wa kodi unaendelea kwa kampuni mpya etc etc,kind of vicious circle of poverty.

    ReplyDelete
  3. Nakuunga mkono Mtanzania halisia,mchezo huu huu dio uliofanywa kwenye makampuni ya Migodi hapa Tanzania,nasi tunachekelea tu pale viongozi wetu wanapoitwa kuzindua makampuni mapya ymabayo nayo yatapewa tax exemption na huo msamaha wa kodi ukikaribia kuisha wanauzia wengine au wanabadili jina kwani tayari wanakuwa wamechuma vya kutosha na mchezo wa msamaha wa kodi unaendelea kwa kampuni mpya etc etc,kind of vicious circle of poverty.

    ReplyDelete
  4. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 23, 2010 at 10:31 AM

    Mimi nikiwa Mwanasheria niliyesoma kwa fedha zenu za walipa kodi naomba nikujibu kwa kufupi.Ingawa sijapata muda wa kutosha kufanya mapitio ya kutosha juu ya Sheria mbalimbali zinazogusa ubadilishaji wa majina ya Kampuni kama hizi,lakini ninaamini kuwa Kampuni hii yaweza kukwepa kodi kwa njia hii.Wakati wa makusanyo ya kodi yatakapokuwa yakifanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA,Kampuni ya Zain haitakuwepo kwenye orodha ya walipa kodi(Tax Units)badala yake kutakuwepo na Kampuni ya Airtel.Kwakuwa Kampuni hiyo mpya itakuwa imefanya biashara kwa miezi michache,jumla ya mapato yake(yale ya Zain hayatakuwepo),itakuwa ndogo hivyobasi kodi kuwa ndogo.Ingawa kubadili jina kuna gharama za zinazolipwa kwa Msajili wa Makampuni,bado kodi itakayoepukwa itakuwa kubwa sana.Siamini kuwa jina jipya linasamehewa kodi kwa muda fulani.Nijuavyo mimi,'Tax holliday' ipo kwa makampuni mapya kabisa ya uwekezaji.Hatahivyo nayo si njema kwa mustakabali wa kimapato wa nchi yetu.Ujanja huu wa kubadili majina una mkono wa mkubwa sehemu fulani,naamini hivyo.Kwanini kampuni iwe kinyonga wa jina tena ndani ya muda mfupi halafu wahusika bado wapo? Nani anayeruhusu mchezo huu mchafu uendelee? Ukiuliza utaambiwa eti wamiliki wamebadilika.Kwani Sheraton,Royal Palm,Movenpick,Kilimanjaro,Celtel,Mobitel,Airtel na Zain ni majina ya watu au babaya kiasi gani hadi yabadilishwe mara kwa mara? Huu sasa ndo ufisadi wenyewe alioupigia kampeni Dr.Slaa.Unatutafuna sana.Kwa maelezo ya kina niemail kwenye thepresident2000@hotmail.com

    ReplyDelete
  5. huu ni usanii ,kila mara kubadilisha jina ili wapewe msamaha wa kodi,na pia mwandishi hii kampuni inatoa huduma katika nchi 19 na sio 34 kama ulivyoandika.

    ReplyDelete
  6. Hii ndiyo zawadi ya umbumbumbu tutabaki kupokea kijacho. Utaalamu wetu utabaki kwenye maneno na kuchakachua. Kama ni mafuta, kura au hata ulinzi wa nchi. Makampuni yatatuchezea mpaka kesho...

    ReplyDelete