Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umetakiwa kumtafuta mkaguzi wa mahesabu kwa ajili ya kukagua mahesabu kwa kipindi cha miezi mitatu, tangu uongozi mpya uingie
madarakani.
Katika taarifa ya mdhamini wa klabu hiyo, Yusuf Manji alisema anachojua ni kwamba katika kipindi hicho kuna fedha nyingi zimepatikana, hivyo itakuwa vizuri kama matumizi na mapato yakawekwa wazi.
"Tujenge utaratibu wa kila miezi mitatu kufanya ukaguzi wa mahesabu ili tueleweke kwa wanachama wetu, kwani hilo litatujengea imani kwa kila mtu," alisema Manji.
Alisema tangu kipindi hicho, klabu hiyo imekuwa ikiingiza mapato kwa njia mbalimbali, ikiwemo mapato ya milangoni, kutoka kwa wadhamini wao TBL, kupitia matangazo mbalimbali redioni na kwenye televisheni, vitega uchumi vya klabu hiyo pamoja na udhamini wake yeye mwenyewe.
Manji alisema kila kitu kikiwekwa wazi hakuna mwanachama yeyote atakayehoji matumizi na mapato, kwani kila baada ya miezi mitatu kila kitu kitakuwa wazi.
Alisema anashangaa kuona mbali ya fedha nyingi kupatikana lakini mchezaji Shamte Ally, ameshindwa kupewa dola 3000 za Marekani kwa ajili ya kupata matibabu.
Mdhamini huyo alisema ni muda mrefu sasa mchezaji huyo amekuwa majeruhi, lakini hakuna jitihada zozote zinazofanywa, ili kuhakikisha anatibiwa na kuendelea kuisaidia timu hiyo.
No comments:
Post a Comment