Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameanza maandalizi ya mchezo wao wa keshokutwa dhidi ya Azam FC, ambapo leo asubuhi wamefanya mazoezi
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Timu hizo kwa mara ya mwisho zilikutana Septemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mchezo wa ligi ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Lakini sasa zitakutana katika tamasha la Amka Kijana, litakalokuwa na burudani mbalimbali wakiwemo wasanii wa bongo fleva na bendi za muziki wa dansi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Cliford Ndimbo alisema tayari wameshatoa taarifa kwa wachezaji wao na leo wataanza mazoezi rasmi wakitokea nyumbani kwao.
"Si unajua sisi ndiyo mabingwa wa Bara, sasa tunapoalikwa katika tamasha kama hili ni dhahiri lazima tuoneshe ubingwa tulimeupata vipi, hivyo kikosi chetu kitaanza mazoezi kesho (leo), asubuhi pale Uwanja wa Uhuru," alisema Ndimbo.
Wasanii watakaotoa burudani siku hiyo ni Berry Black, AT, Omari Omari, bendi ya Bwagamoyo Sound na makundi ya TMK Wanaume Family na Tiptop Connection.
Tamasha hilo limeandaliwa kwa udhamini wa kituo cha radio cha Times FM na Clouds FM, likiwa na lengo la kuhamasisha vijana kubadilika kwa kufanya kazi kwa bidii.
Litaanza saa 4 asubuhi ambapo kiingilio kitakuwa ni sh. 15,000 kwa viti maalumu, sh. 10,000 kwa jukwaa kuu, sh. 5,000 kwa viti vya kijani na sh. 3,000 kwa viti vya mzunguko.
No comments:
Post a Comment