Na Elizabeth Mayemba
KAMATI ya Nidhamu ya Yanga, imemsamehe mchezaji wake Bakari Mbegu, aliyesimamishwa kwa muda na uongozi huo kwa utovu wa nidhamu.
Mchezaji huyo alisimamishwa kwa muda katika timu hiyo, baada ya kudaiwa kufanya utovu wa nidhamu wakati timu yake ilipokuwa Tanga, kucheza na Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema baada ya Kamati ya Nidhamu chini ya Mwenyekiti wake, Mark Anthony kupitia maelezo ya mchezaji huyo aliyoyatoa kwa njia ya maandishi, iliamua kumsamehe.
"Alikiri kosa lake na kuomba msamaha kwa uongozi, hivyo kamati imeona imsamehe kwa sababu ndiyo kosa lake ya kwanza," alisema Sendeu.
Akizungumzia kipa wake, Ivan Knezevic ambaye amepewa adhabu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sendeu alisema kamati hiyo inasubiri taarifa kamali kutoka shirikisho hilo, ili itoe maamuzi yake kuhusu mchezaji huyo.
Kipa huyo anadaiwa kumtolea mwamuzi lugha chafu, wakati timu yake ilipocheza na African Lyon, pia watajadili na faini ya Sh.500,0000 waliyopigwa na TFF.
Wakati huo huo, Sendeu alisema suala la mchezaji wake wa kimataifa Mghana, Kenneth Asamoah lipo mikononi mwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Alisema wataendelea kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi, ili mchezaji huyo aweze kuichezea timu hiyo.
Pia alisema mchezaji, Abdi Kassim 'Babi' amekwenda nchini Dubai kufanya majaribio katika Klabu ya Dongpam Longan.
Sendeu alisema mchezaji huyo alifuata taratibu zote kwa kuandika barua kwa Katibu Mkuu kuomba ruhusa na uongozi ukampa baraka zake.
No comments:
Post a Comment