16 November 2010

Wanne watimuliwa CCM Bukoba kwa usaliti.

Na Livinus Feruzi, Bukoba

SIKU chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, wanachama wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Bilele, Manispaa ya Bukoba
mkoani Kagera, wamefukuzwa uongozi na kunyang’anywa kadi za chama hicho kwa kudaiwa kukisaliti chama.

Katibu wa CCM wa Kata ya Bilele, Bw. Rashid Hassan alisema kuwa  uamuzi huo ulichukuliwa na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Kata hiyo, katika kikao chake kilichofanyika Novemba 12, mwaka huu.

Bw. Hassan alisema miongoni mwa tuhuma zilizothibitishwa kuwahusu wanachama hao ni pamoja na kukisaliti chama hicho kwa kushirikiana na wapinzani kufanya kampeni waziwazi, za kuwapinga wagombea wa CCM katika ngazi za udiwani, ubunge na urais kwa kutumia dhamana waliyopewa na chama hicho.

Aliwataja waliovuliwa uanachama pamoja na uongozi kuwa ni Bw. Uddi Miruko, ambaye ni Katibu Mwenezi wa Kata ya Bilele na Mwenyekiti wa Mtaa wa Uhuru.

Bw. Hassan alisema wengine ni Bw. Abdallah Kichwabuta ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa Tawi la Uhuru, Bw. Goodselda Rwitana  ambaye ni Katibu wa Tawi la Uhuru na Bi. Fatma Ahmad ambaye ni Katibu wa UWT Tawi la Uhuru.

Alisema kuwa wanachama hao, mnamo Novemba 1, mwaka huu walikutwa kwa aliyeshinda kiti cha udiwani katika kata hiyo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Ibrahim Mabruk wakishangilia ushindi alioupata katika uchaguzi huo.

Katika kikao hicho, wajumbe wameomba ngazi ya CCM wilaya ya Bukoba kumchukulia hatua Bi. Murungi Badru Kichwabuta, ambaye ni mwenyekiti wa UWT wilayani humo, kwa madai ya kushiriki kukihujumu chama wakati wa uchaguzi mkuu.

Wakati wa kampeni za chama hicho, Bi. Kichwabuta alikuwa miongoni mwa wanachama watano waliosimamishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mjini kushiriki kampeni za chama hicho tangu Oktoba 20 kwa madai ya kukihujumu chama.

Pia wajumbe hao wamewaonya wajumbe wa kamati ya siasa ya kata hiyo, kuacha kutoa siri za vikao nje.

1 comment:

  1. HIYO NDIYO DEMOKRASIA MFU NDANI YA CCM KWAMBA INABIDI UKUBALIANE NA MAAMUZI YALIYOTOLEWA NA CHAMA NA LAZIMA UMPIGIE KURA NA KAMPENI MTU AMBAYE AMECHAGULIWA NA CHAMA HATA KAMA MUHUSIKA HAFAI. NYIE MULIOFUKUZWA NI MASHUJAA WA DEMOKRASIA KWA MAANA MMEWEKA MASLAHI YA NCHI MBELE BADALA YA CCM.

    ReplyDelete