*Mbivu na mbichi ya Asamoah leo.
Na Zahoro Mlanzi
KLABU ya Yanga, inatarajia kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu bara na mashindano ya Kimataifa Novemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam.Mbali na
hilo, uongozi wa klabu hiyo leo unatarajia kutoa taarifa rasmi ya mchezaji wao raia wa Ghana, Kennett Asamoah baada ya vyombo mbalimbali vya habari kutoa taarifa tofauti tofauti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema baada ya kuwapa mapumziko marefu wachezaji wao, mwishoni mwa mwezi huu wataingia kambini.
"Kama unavyojua baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika wachezaji wote walipewa ruhusa ya kwenda kuona familia zao, ila Novemba 26 wanatakiwa kuripoti kambini," alisema Sendeu.
Mbali na hilo, pia alizungumzia suala la usajili ambapo alisema watasajili wachezaji kati ya watatu au wanne kwa ajili ya kuziba pengo lililoonekana katika mzunguko wa kwanza.
Alisema tayari wachezaji kutoka nchi mbalimbali kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Zambia, tayari wameshaanza kufanya majaribio na timu hiyo.
Pia alizungumzia suala na Asamoah ambapo alisema vyombo mbalimbali vya habari vinalizungumzia suala hilo katika mtazamo wao na si hali halisi ya suala lenyewe lilivyo.
"Kutokana na hali hiyo, kesho (leo) tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kulitolea ufafanuzi, ili jamii na wanachama wetu wajue hili suala limefikia wapi, hivyo kila kitu tutakizungumza kesho," alisema Sendeu.
Wakati huo huo, Sendeu alisema Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo, ilitarajia kukutana jana jioni kujadili mwenendo mzima wa nidhamu ya timu hiyo katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
No comments:
Post a Comment