15 November 2010

TP Mazembe Mabingwa Afrika tena.

TUNIS, Tunisia

KLABU ya TP Mazembe, imeteteza taji lake la ubingwa wa Afrika na kuifanya ilitwae kwa mara ya nne.Timu hiyo ya Congo, iliweza kuibana Esperance ikiwa nyumbani
na kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya marudiano, baada ya kushinda mechi ya awali mabao 5-0.

Esperance ilihitajika kupata muujiza ili kugeuza matokeo, licha ya kuonekana kuwa na ri kubwa lakini muujiza haukuweza kutokea.

Harrison Afful, aliwafungia bao la kwanza dakika ya 13 lakini goli hilo lilisawazishwa na Deo Kanda, ikiwa zimesalia dakika 20 kabla ya mechi kuisha.

Mlinzi wa Esperance, Ayman Ben Amor aliigharimu timu yake kwa kuoneshwa kadi nyekundu, muda mfupi baada ya Afful kufunga goli lao, Mazembe imeibuka bingwa kwa uwiano wa magoli 6-1.

"Hii ina maana sana katika maisha yangu," kiungo wa Mazembe, Christopher Semakweri aliiambia BBC baada ya mechi.

"Tulikuja tukiwa na mipango ya kutwaa ubingwa, mpango ilikuwa ni kuwa makini na mchezo. Hatukujali kuhusu mazingira, tulilimudu hilo."

Katika mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Rades, uliopo mjini Tunis, mashabiki walifanya fujo muda mfupi kabla ya mechi kuisha.

Hata hivyo Polisi walilazimika kutumia nguvu kudhibiti matatizo.

Wakati wa mechi kulikuwa na matatizo kutokana na Mazembe kusawazisha goli, polisi walilazimika kuwaondoa uwanjani baadhi ya mashabiki, ingawa mechi ilikuwa ikiendelea.

Mazembe kwa kutwaa ubingwa huo, imepata kitita cha dola milioni 1.5 na itakwenda Abu Dhabi, kucheza mashindao ya kusaka Klabu Bingwa ya Dunia mwezi ujao.

Mazembe itafungua dimba katika nchi hiyo ya Ghuba kwa kucheza na mabingwa watetezi Pachuca ya Mexico.

No comments:

Post a Comment