15 November 2010

'Wazazi msiwe mawakala wa kuuza watoto'

Na Jumbe Ismailly,  Singida 
 
WAZAZI  na  walezi wa wanafunzi  katika Kata ya Unyamikumbi, Manispaa ya Singida wametahadharishwa kuachana na tabia ya kugeuzwa kuwa mawakala wa kupeleka kwenye
Mikoa ya  Dar es Salaam  na  Arusha kwa lengo la kuwatafutia kazi badala ya kuendelea na masomo.
 
Tahadhari hiyo imetolewa na aliyekuwa  Diwani wa Kata ya Unyamikumbi (CCM)  Bw.  Kipandwa Ipini alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya 35  ya Shule ya Msingi Kisaki, iliyopo  katika manispaa hiyo.
 
“Wazazi nawaomba mfanye yafuatayo, msiwe mawakala wa watu wanaotafuta watoto kuwapeleka  Dar-es-Salaam  na  mikoa mingine ya  Arusha”alisema .
 
Bw. Ipini alisema baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wanapofanya mtihani wa kumalizia elimu ya msingi, wamekuwa wakilaghaiwa na maajenti wa kutafuta watoto kwa sh.20,000  ambazo wao hupatiwa sh. 10,000 na kisha kumtoa
mtoto.
 
Hata hivyo  mtoto anapofika katika mkoa hiyo  anakopelekwa hulala uwani na kula makombo ya chakula kinachobaki huku mzazi akitumiwa shilingi elfu kumi zisizoweza kumsaidia kwa lolote lile.
 
“Waheshimiwa haya mambo yapo tunaposafiri mikoa ya mbali tumeleta watoto hapa wakiwa wameshazidiwa,hapewi mshahara, lakini wewe mzazi unaendelea kuridhika unapotumiwa
shilingi hizo elfu kumi”alisema  Bw. Ipini.
 
Kutokana na hali hiyo Bw. Ipini alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutokuwa tayari kuendelea kuwatosa watoto wao kwa kuthamini fedha hizo  zinazotumwa kupitia kwa  mawakala  anayeaminika kwa shughuli hiyo kwenda kumlaghai mzazi huyo.
 
Aliweka bayana kwamba kutokana na umuhimu wa elimu katika karne hii ya sayansi na teknolojia wakati umefika hivi sasa kwa wazazi na walezi hao kutokuwa tayari kushawishiwa na kuwatoa watoto wao kwenda kutafutiwa kazi na badala yake wawajengee
mazingira mazuri katika elimu.
 
Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa Elimu wa Kata ya Unyamikumbi,  Bw. Emanueli Tukiko alitoa wito kwa wanafunzi ambao hawatafanikiwa kuchaguliwa kuendelea na masomo ya
sekondari wajiunge na shule za ufundi.
 
Awali akisoma risala ya shuile hiyo, Mwalimu Mkuu, Bw. Patrick Masong alisema kuwa  baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi nchini (MMEM) mwaka 2002  hadi sasa kuwa ni pamoja na kujenga vyumba vya madarasa saba na matundu 20 ya vyoo vya wanafunzi.
 
Aliyataja mafanikio mengine ni kutengeza madawati 60, kujenga nyumba mbili za walimu,  kukarabati vyumba vinne vya madarasa, kukarabati nyumba sita za walimu na kuandikisha kwa asilimia kati ya 95 hadi 100 ya wanafunzi wa darasa la kwanza kila mwaka.

No comments:

Post a Comment