15 November 2010

Wenye ulemavu wafurahia kupata wabunge.

Na Rabia Bakari

SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA), limevipongeza vyama vya siasa kwa kupata wabunge wenye ulemavu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania la
2005/2010.

Akitoa pongezi hizo kwa vyombo vya habari, Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Bw. Amon Anastaz alisema wanakipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuteua wabunge viti maalumu wawili wenye ulemavu ambao ni Bi. Magreth Mkanga na Bi. Al-Shaimar Kwegiar.

"CHADEMA wamemteua Bi. Regina Mtema na (CUF) kilichopitisha baadhi ya wagombea ambao ni wenye ulemavu hadi kuchaguliwa Bw. Salum Barwan kuwa mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, lakini pia hatuna budi kuwapongeza wananchi wa jimbo hilo waliofanya maamuzi hayo licha ya kauli potofu ya unyanyapaa iliyotolewa na mmoja wa wapambe wa chama kimojawapo cha siasa dhidi ya mgombea huyo wakati wa kampeni," alisema.

Aliongeza kuwa SHIVYAWATA kwa kushirikiana na Asasi zinazohudumia watu wenye ulemavu nchini, wanaamini kuwa Rais Jakaya Kikwete ataongeza wabunge wengine zaidi katika uteuzi wake wa nafasi 10 kama ambavyo alifanya katika bunge lililopita, na hasa ukizingatia kuwa wamepoteza waliokuwa wabunge wenye ulemavu.

Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Bi. Lupi Mwaisaka Maswanya alimpongeza Bi. Anne Makinda kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania 2010-2015.

"Kuchaguliwa kwake kumefungua milango mipya kwa wanawake kushika uongozi mkubwa moja kati ya mihimili mitatu mikuu ya dola nchini ikiwa ni Serikali, Mahakama na Bunge," alisema.

Pia alimpongeza Bw. Freeman Mbowe kuteuliwa kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, "pamoja na pongezi zote hizo lakini pia tunawasihi viongozi hawa pamoja na wabunge wote kutumia busara zao katika kufanikisha maamuzi yaliyo sahihi kwa maslahi ya taifa, pasipo kujali itikadi zao za vyama vya siasa," aliongeza.

1 comment:

  1. POA mko juu, nashukuru CHADEMA haikumpa ubunge mamake Zitto ,kwa kuwa ni mwehu, tapeli na si muadilifu. hili ni jambo la kushukuru.

    ReplyDelete