15 November 2010

Mghana abambwa na kilo 13 za cocain.

Na Said Njuki, Arusha

SIKU moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Saidi Mwema kupangua baadhi ya Makamanda wa Jeshi, Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania, kwa
kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kimemnasa raia mmoja wa Ghana, Kwaku Kanaga (41)
akisafirisha shehena kubwa ya dawa za kulevya aina ya cocaine.

Mghana huyo alibambwa akiwa na kilo 13 za cocaine jana alfajiri Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akitaka kuondoka kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Kenya kuelekea nchini kwake.

Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo, Bw. Godfrey Nzowa zimeeleza kuwa Kanaga amekuwa akisubiri kusafirisha dawa hizo kwa mwezi mmoja sasa tangu aingie nchini.

Bw. Nzowa alisema dawa hizo zilikuwa ndani ya vifurushi viwili vilivyokuwa na uzito wa kilo 6.5 kila moja vikiwa vimefichwa ndani ya mabegi mawili tofauti ya Mghana huyo na kwamba alikuwa aondoke jana alifajiri na ndege hiyo kupitia Nairobi.

Hata hivyo, Bw. Nzowa ameondolewa katika kitengo hicho na kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi kupangiwa kazi nyingine.

Aliongeza kuwa dawa hizo zilihifadhiwa ndani ya mifuko maalumu inayozuia mashine za kutambulia dawa kuzibaini na mbwa kushindwa kunusa dawa hizo.

Mghana huyo alifika nchini Septemba 15 mwaka huu na kufikia hoteli ya Exclusive Mikocheni Dar es Salaam akiwa kama mwanamziki na amekuwa akisubiri dawa hiyo tangu wakati huo.

“Jeshi la Polisi kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya limekuwa likifanya kazi nzuri na katika hili limeshirikiana na wataalamu wa viwanja vya ndege, polisi wa uwanja huo pamoja Mamlaka ya Forodha. Tangu Januari mwaka huu tayari kilo 97.4 za heroine na 58 za cocaine zimekamatwa, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa,” alisema Bw. Nzowa.

Bw. Nzowa alisema kuwa hali imezidi kuwa ngumu kwa wafanyabiashara ya dawa za kulevya licha ya ugumu wa kukabiliana na hali hiyo kwani kadri wanavyobadili mitindo ya usafirishaji wa dawa hizo wamekuwa wakigundua mbinu hizo na kuwatia mbaroni.

1 comment:

  1. Petro Eusebius MselewaNovember 15, 2010 at 10:41 AM

    Kamishna Nzowa anastahili pongezi sana.Kila mara anafanya anachostahili kukifanya.Lakini,harakati hizo ziongezwe.Hivi,nani anapitisha wapi madawa haya yaliyozagaa mitaani?

    ReplyDelete