15 November 2010

Kikwete atakiwa kuondoa makundi CCM.

Na Faida Muyomba, Geita

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Rais Jakaya Kikwete ameshauriwa kuondoa makundi ndani ya chama hicho kwa kuwatimua wanaokisaliti vinginevyo kitamfia
mikononi mwake kabla ya mwaka 2015.

Pia Rais Kikwete ametakiwa kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kwa usahihi ili kumwezesha kubaini mahitaji ya wananchi walio wengi ikiwa ni pamoja na kutokubali matajiri kutumika kwa maslahi yao binafsi.

Kauli hiyo ilitolewa  na mwanachama mkongwe wa chama hicho wilayani Geita, Bw. Michael Makongoro (76) katika mazungumzo maalumu na Majira, yaliyofanyika ofisini kwake jana.

Bw. Makongoro ambaye alijiunga na TANU mwaka 1954 hadi sasa akiwa ni mwanachama wa CCM, alisema kuwa cha hicho hivi kinayumbishwa na wanachama wachache waliojiunga kutokana na maslahi yao binafsi badala ya manufaa ya chama.

"Rais Kikwete anatakiwa kubadilika iwapo anataka CCM iendelee kutawala mwaka 2015, atoe kauli, nchi haiweze kuendeshwa bila kauli, amekuwa mkimya mno kiasi kwamba makundi yanazidi kukimaliza chama. Hatuwezi kufiwa na chama tunaona hivi hivi," alisema mwanachama huyo mkongwe wa CCM.

"Wanachama wasiofaa ndani ya chama, Mwenyekiti atoe kauli bila woga wala kujali hata kama mwanachama huyo ni shangazi yake, ni tajiri wala masikini. Amechaguliwa kuwa rais wa nchi, hivyo asimamie maslahi ya nchi na chama chake, atumie vyombo vya dola
alivyo navyo kupata taarifa sahihi iwapo anaona hawafanyi kazi ipasavyo, basi afike kwa wananchi moja kwa moja na kuzungumza nao kujua matatizo yanayowakabili," aliongeza mzee huyo.

Alisema kuwa ubinafsi na viburi vya fedha kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho ndivyo vinakifanya kiyumbe na kuonekana kuwa hakifai hasa kwa vijana, jambo alilosema endapo halitatafutiwa dawa mapema huenda wapinzani wakashika nchi mwaka 2015.

Kuhusu baraza lake la mawaziri analotarajiwa kuunda hivi karibuni, Mzee huyo amemshauri Rais Kikwete kuhakikisha anachagua watu safi wasio na tuhuma zozote ndani ya jamii ili kuliletea sifa Taifa nje na ndani ya nchi.

Alisema kuwa endapo baraza hilo litakuwa na viongozi wasio safi ndani ya jamii, huenda akapata wakati mgumu kuwaeleza wananchi kwa kuwa roho zao hazitokuwa na amani, hivyo kuiona serikali haina msaada kwa maisha yao.

Mwanachama huyo alikuwa akizungumzia hali halisi ya kisiasa iliyopo hapa nchini hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu uliomweka madarakani kwa kipindi cha pili Rais Jakaya Kikwete, huku baadhi ya wagombea maarufu wa CCM wakianguka katika uchaguzi
huo.

1 comment:

  1. SHIBUDA ALISHASEMA KUWA CCM ITAMFIA KIKWETE MIKONONI IWAPO HATAKISAFISHA NA NDIKO TUNAKOELEKEA SASA TUNAELEKEA KUCHAGUA WENYEVITI WA HALMASHAURI NA MAMEYA MAKUNDI YAMEAANZA CCM INAELEKEA KUFA TUNAIOMBEA IFE VIZURI ILI ISISAMBARATIKE.

    SAMWEL ELIAS

    ReplyDelete