15 November 2010

Mbatia kumpinga Mdee mahakamani.

Na Rabia Bakari

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kinakusudia kumburuta Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya
na Mbunge wa Kawe Bi. Halima Mdee kwa madai ya kutoa kauli za ubaguzi wakati wa kampeni katika Jimbo la Kawe, ambazo kinadai ni kinyume na misingi ya haki za kibinadamu.

Sambamba na hilo, pia chama hicho kimekusudia kufungua kesi za uchaguzi katika majimbo ya Babati Vijijini na Buyungu kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika majimbo hayo ikiwa ni pamoja na madai ya wizi wa kura.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi, Bw. Faustin Sungura alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya chama kutoa maazimio hayo katika mkutano uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.

"Wakati wa kampeni, TAMWA kupitia kwa Bi. Ananilea Nkya, pasipo halali yoyote na wala sababu za msingi alipotosha umma na kumjengea chuki mgombea wetu, Bw. James Mbatia kwamba anawanyanyasa wanawake.

"Kauli hii ililenga kuwahamasisha wanawake na au wasichana wa Jimbo la Kawe kumchukia Bw. Mbatia na badala yake wawapigie kura wanawake kama njia ya kumkomoa," alidai.

Aliongeza kuwa kauli hiyo ya TAMWA iliathiri wapiga kura wengi na hasa ilihamasisha wanawake kupigiana kura na hata kufanya matokeo ya uchaguzi kuongozwa na wanawake kwa kushika nafasi za kwanza naya pili.

Sambamba na hilo, Bw. Sungura alikanusha madai ya Bi. Mdee kwamba CCM walikuwa wakimpa Bw. Mbatia milioni 80 kila wiki wakati wa kampeni.

Alisema wao kama NCCR-Mageuzi na CCM hakuna mahali popote katika vitabu vya mahesabu ya vyama hivyo, panapoonesha kwamba waliwahi kulipa au kupokea kiasi hicho cha fedha.

"Kama kiasi hiki cha fedha kilitolewa, lakini pasipo utaratibu wa mambo ya mahesabu, na hasa kama fedha hizo hazikuwahi kukifikia chama chetu, na wala kuoneshwa kwenye kumbukumbu za vitabu vya mahesabu, basi mazingira ya rushwa ndiyo yaliyotawala katika makabidhiano ya fedha hizo.

Bw. Sungura aliongeza kuwa kwa misingi hiyo Bi. Mdee alijua kuwa anasema uongo, na alikusudia kupotosha wapiga kura, na kama aliyoyasema yana ukweli atakuwa amevisaidia vyama hivyo juu ya ufujaji mkubwa wa mali za vyama, na kudai kuwa hakuna sehemu ya kujua ukweli wa kauli hizo bila ya kufika mbele ya mahakama.

Akizungumzia Babati Vijijini, Bw. Sungura alisema kuwa wana ushahidi wa kutosha kuwa mgombea wa chama hicho, Bw. Laurent Tara alishinda, tofauti na msimamizi wa uchaguzi alivyotangaza matokeo.

"Majumlisho ya vituo vyote yanayonesha kwamba, Mgombea wa CCM Bw. Jitu Soni alipata kura 32,190 na Bw. Tara alipata kura 32,248, kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi mkuu anayetakiwa kutangazwa mshindi ni yule aliyepata kura nyingi.

"Kwa sababu hii halali na kwa mujibu wa sheria, Bw. Tara ndiye alitakiwa kutangazwa mshindi, kwa kuwa hatuwezi kupigana ili kushinikiza atangazwe, basi mahakama ndio itakayoenda kuamua.

Akizungumzia kuhusu jimbo la Buyungu, Bw. Sungura alisema baada ya upigaji kura kumalizika, walikuta kura za mgombea wa NCCR-Mageuzi zimezagaa mitaani na mawakala wao waliwageuka na kukataa kuwapa fomu za matokeo.

"Tumeshindwa kufahamu sababu za baadhi ya kura za mgombea wetu kukutwa mitaani, hivyo tuna wasiwasi na baadhi ya watu na ambao tuliwaamini na kuwafanya wawe mawakala wetu huko vituoni, lakini kabla hawajaanza kazi tuliyowapa walikula kiapo cha kutunza siri za mtu au mamlaka tofauti na sisi.

"Kwa misingi hii, tunaamini kwamba uchaguzi huo uliendeshwa kwa siri na kukiuka taratibu, na hivyo kutangazwa kwa Bw. Christopher Chiza wa CCM kuwa mshindi ni batili, na mahakama ndiyo itaenda kuamua.

Bw. Sungura alisema kuwa kesi hizo zimefikia hatua ya mwisho kukamilika na wanatarajia kabla au Novemba 19, mwaka huu zote zitakuwa zimefunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda za Tabora, Arusha na Dar es Salaam.

2 comments:

  1. Petro Eusebius MselewaNovember 15, 2010 at 10:33 AM

    Sasa nyie NCCR-MAGEUZI mnakwenda Mahakamani kumshtaki nani? Mdee,Ananilea Nkya au Tume ya Uchaguzi? Kwanini hizo zisiwe kesi za 'Defamation'zinazojitegemea badala na kuzihusisha na matokeo ya uchaguzi? Mwacheni Dada Halima Mdee aanze kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Kawe(karibu vigogo wote wa Serikali)na wenzangu na mie.Muda ndio huu.Nadhani Mheshimiwa Mbatia umenielewa.Mfikishie habari hii na Mheshimiwa Sungura na Mwalimu wangu Dr.Sengondo Mvungi.Mbarikiwe!

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli hizi ni hatua muafaka mnakusudia kufanya. nawatakia kila la kheri, na hii ndio itakuwa fundisho kwa wale wote wanaosema uongo na kutukana wenzao ili washinde kwa hila. watz hawatuwezi kupata viongozi wanaowadhalilisha wenzao kwa makusudi kiasi hiki.

    ReplyDelete