Na Veronica Modest, Musoma
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa na watu wenye hasira katika Kisiwa cha Nyasaungu Wilaya ya Musoma Vijijini, mkoani Mara wakidaiwa kujiandaa kwenda
kufanya uhalifu kisiwani hapo na mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Robert Boaz alisema kuwa watu hao walikuwa wametokea Mkoani Mwanza na
kwenda kisiwani humo.
“Marehemu hao walikuwa wametokea Mwanza na walifikia kisiwani hapo Novemba 16 mwaka huu na kufikia katika nyumba ya wageni iitwayo Ikonjo ambayo mwenyeji wao
anaitwa Magesa Amosi,”alisema Kamanda Boaz.
Kamanda Boaz aliwataja marehemu hao kuwa ni Arute Charles (20), Mkazi wa Igoma, Amos Alphonce (35) mkazi wa Nyakato na Abdul Seleman (37) mkazi wa Buswelu na anayeshikiliwa na jeshi la polisi ni Magesa Amosi Mkazi wa kisiwa hicho.
Alisema kuwa wananchi wa eneo hilo walianza kuwatilia mashaka marehemu hao kuanzia siku walifika kisiwani hapo na siku ya tukio hilo walimkuta Amos akiweka mafuta katika boti tayari kwenda kufanya uhalifu.
“Kwa kuwa wananchi wengi wanamfahamu Amosi aliwahi kuwekwa mahabusu kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 kwa kosa la kunyang’anya kwa kutumia nguvu walianza kumtilia mashaka,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kumuona Amos akiweka mafuta katika boti ndipo wananchi walifika na kumtaka awaoneshe wageni wake na kwenda kuwaamusha wenzake hao na yeye alitoroka ndipo wananchi waliwahoji watuhumiwa hao na baada ya kuona majibu yao hayawaridhishi waliwapiga na kuwaua.
Kamanda Boaz ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutojichukulia sheria mkononi kwa kuwa wanaweza kuua watu ambao sio wahalifu kwa kuwa Jeshi la Polisi lipo
katika kumaliza mtandao wa uhalifu mkoani hapo.
“Natoa wito kwa wananchi wasichukue sheria mkononi waashike wahalifu ili jeshi letu tufanye mahojiano nao na kuwakamata wengine ambapo itatusaidia kuharibu mitandao yao na kuziba njia zote za uhalifu na tutaweza kupata suluhisho la muda mrefu,” alisema.
Jeshi la Polisi lilienda kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa aliyesalimika na kukuta injini mbili za boti, uchunguzi wa kina unaendelea kujua uhalali wa
umiliki wa injini hiyo pia uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment