21 November 2010

Chanzo cha kupungua wapiga kura Nkenge chabainika.

Na Theonestina Juma, Missenyi.

BAADHI ya wakazi wa Jimbo la Nkenge Wilayani Missenyi Mkoani Kagera wakazi wengi wa eneo hilo hawakujitokeza kupiga kura Novemba 14, mwaka huu kutokana na ukosefu wa
uhamasishaji, ugumu wa maisha na kutoona manufaa yoyote yanayopatikana kutoka kwa viongozi wanaowachagua mbali na kuwajekeli tu.

Hayo yamebainishwa wiki hii kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimboni humo waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa gazeti kuhusu kwa nini asilimia wakazi wengi wa jimbo hilo hawakujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo uliokuwa umeahirishwa katika majimbo saba nchini.

Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT) wa Kata ya Bunazi  ambaye pia ni Balozi wa Nyumba kumi katika kijiji cha Omudongo, Pastory Martin alisema kuahirishwa kwa uchaguzi kuliwafanya baadhi ya wapiga kura kughairi na kuona kama ni usumbufu, kutokana na hata hali ngumu ya maisha inayowakabili.

Alisema licha ya kuwa matangazo mengi yalikuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti kwenye vyombo vya habari,  haikuweza kuwafikia watu kikamilifu kutokana na baadhi ya
watu wa vijiji wa jimboni kukosa fedha kununua betri za redio zao kwa ajili ya kusikiliza redio.

"Huwezi kuamini kungalia na hali halisi inayowakabili wananchi, hasa kwa wakati huu wa jua kali huku mazao yao yakiwa yamenyauka mashambani, hawana hela za kununulia betri
kwa ajili ya kuweka kwenye radio ili kuweza kusikiliza taarifa mbali mbali, hivi unategemea mtu anaweza kutoa hela kununulia betri huku nyumbani hakuna hata chumvi
kwa ajili ya kuweka kwenye mboga?alihoji.

Naye Bi. Stephania Kokutabulula (38) mkazi wa Omudongo ambaye naye hakujitokeza kupiga kura ya awamu ya pili alisema  kuwa alijua wazi kuwa Mbunge aliyechaguliwa, Bi. Assumpta Mshama wa CCM angeshinda kwa kuwa wengi walikuwa wakimjua tofauti na wangombea wa vyama vingine.

Alisema wagombea wa vyama vya upinzani hawakuwahi kufika katika maeneo yao kuomba kura, na kwamba hata katika eneo lao hakuna wapinzani na hivyo, hakuona umuhimu wa kupoteza muda wake kwenda kupiga kura licha ya siku ya kura ya Oktoba 31, mwaka huu alishiriki kupigakura kutokana na upande wa urais kulikuwa na mchuano mkali na haikuwa raihisi kutabiri ni mgombea gani wa rais angeibuka mshindi.

"Siku hiyo nilikuwa tu nyumbani nikifanya shughuli zangu, nilioona kwenda huko ni kupoteza muda tu, kwani hakukuwa na upinzani mkali kati ya wagombea wa nafasi ya
ubunge, "alisema Bi. Kokutabulula.

Katika Jimbo la Nkenge Tume ya Uchaguzi iliahirisha uchaguzi wake kwa upande wa ubunge kutokana na makaratasi ya kupigia kura kutofika kwa wakati.

 Wananchi walioshiriki katika uchuguzi wa awali walikuwa ni  42,074 kati ya watu 90,631 waliojiandikisha, ambapo kwa uchaguzi wa ubunge wapiga kura waliojitokeza walikuwa ni  24,335 hii ikiwa ni pungufu  ya watu 17,000.

1 comment:

  1. mbowe kaza uzi, usimsikilize mrema au maalim self, hao tako zamani ni ccm damu na nia yao kubwa si kuwakomboa watanzania bali ni kulilia madaraka, rejea mrema akimkampenia kikwete badala ya mgombea wa chama chake ingawa yeye ni mwenyekiti wa chama hicho NA AKIOMBA APEWE UWAZIRI WA MAMBO YA NDANI, au maalim self yeye ameshapewa umakam na sare ya suti ya ccm, sasa anaona eti kumgomea rais kikwete ni UHAINI!!JAMANI SIASA WEWE MAALIM SELF HATA UNAKUJA DAR UNAFIKIA IKILU HATA BILA KUFIKA BUGURUNI KUONANA NA NDUGU YAKO LIPUMBA!!!UMESAHAU JINSI WANA CUF WALIVOPIGWA RISASI!!
    KATIBA MPYA, TUME HURU YA UCHAGUZI NI LAZIMA,

    ReplyDelete