Na Tumaini Makene.
NCHI za Afrika, Tanzania ikiwemo, hazijaweza kutumia raslimali nyingi zilizobarikiwa kuwa nazo pamoja na fursa nyingine zilizopo, kufanya mageuzi makubwa ya viwanda ili kubadilisha
uchumi wao, kama zilivyofanikiwa nchi za Bara Asia.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam katika Siku ya Viwanda Afrika na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce Mapunjo, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Bi. Mapunjo alisema kuwa nchi nyingi za Afrika, bado zinauza bidhaa zake zikiwa ghafi, hivyo kiasi cha mapato kinachopatikana kutokana na mauzo ya bidhaa hizo hayawezi kuchangia kwa kiasi cha kutosha katika pato la taifa, kwa mataifa ya bara hilo.
"Tumeshuhudia nchi nyingi zikitekeleza mageuzi ya kiuchumi na kisiasa kwa lengo la kuchochea maendeleo na kukua kwa sekta kuu za uchumi kama vile mageuzi ya kilimo, mageuzi ya viwanda. Uzoefu wa mataifa ya Asia unaonesha kuwa wamefanya mageuzi...;
"Makubwa ya viwanda na kuweza kutumia vizuri fursa za utandawazi katika kubadilisha uchumi wa nchi hizo. Pamoja na rasilimali nyingi tulizonazo bado hatujaweza kutumia fursa zilizopo. Mageuzi kidogo yaliyokwishafanyika hadi sasa yamekuwa na mafanikio kidogo sana," alisema Bi. Mapunjo.
Aliongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu 'Viwanda vyenye ushindani kwa maendeleo ya Afrika' inahimiza nchi za Afrika kutilia mkazo katika viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa zenye ushindani katika masoko, ili kuongeza mapato kisha kuwa na uwezo wa kujiletea maendeleo.
Alisema kuwa ili viwanda viweze kuwa na ushindani ni lazima vizalishe bidhaa bora, kwa gharama ndogo ili kukidhi mahitaji ya walaji, "ubora wa bidhaa unaambaatana na ubora wa teknolojia pamoja na malighafi. Suala la teknolojia bora kwa Tanzania ni suala ambalo limekuwa ni ajenda kubwa katika sekta binafsi."
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Viwanda Vidogovidogo la Umoja wa Mataifa (UNIDO) nchini, Bw. Emmauel Kalenzi, mpaka sasa sekta ya viwanda nchini inachangia asilimia 8 katika pato la taifa, huku pia ikito ajira kwa asilimia 0.7 kwa nguvu kazi yote iliyoko nchini.
"Tanzania ni moja kati ya nchi maskini sana duniani, ambayo sekta yake ya viwanda ingali chini ikichangia karibu asilimia 8 ya pato la taifa na kutoa ajira kwa karibu asilimia 0.7 kwa nguvu kazi yote iliyopo, asilimia kubwa ya watu.
"Zaidi ya asilimia 80 bado wanasumbuka katika kilimo cha kizamani, ikiwa ndiyo nguzo ya maisha yao ingawa pia bado karibu asilimia 30 yao wanaishi chini ya dola moja kwa siku, ambayo ni chini ya mstari wa umaskini," alisema Bw. Kalenzi.
Naye Bi. Jonitha Onabanjo kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alberic Kakou, alisema kuwa kuuza bidhaa za kilimo na madini, zilizosindikwa ni muhimu kwani zinaongeza ubora na thamani wakati wa kuuzwa, hivyo itasaidia nchi za Afrika katika uchumi wa dunia.
No comments:
Post a Comment