Na Mwandishi Wetu
KITENGO cha Huduma za Afya cha Agha Khan kimewaomba Watanzania wenye utaalamu wa afya wajenge moyo wa kujitolea ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa
sababu mpaka sasa Tanzania haina madaktari wa kutosha.
Hayo yalisemwa na viongozi mbalimbali wa kitengo hicho hivi karibuni katika ghafla maalamu ya kuwapongeza wafanyakazi waliojitolea katika kambi za kansa ya matiti zilizoitishwa na Hospitali ya Agha Khan na sherehe za kufunga kufanyika hospitalini hapo.
Katika kambi hizo ambazo zilichukua takribani miezi miwili ,zaidi ya akina mama 2,300 walichunguzwa matiti yao. Miongoni mwao 15 waligunduliwa na kansa na sasa wanaendelea na matibabu. Wengine 20 bado wapo katika uchunguzi zaidi.
“Tumejifunza mengi kutokana na kambi hizo kwani kila mtu ameonyesha moyo wa kujitolea bila kuchoka kwa kadri ya uwezo wake. Wagonjwa pia wametuonyesha jinsi walivyokuwa wavumilivu hata pale walipokuwa wamekata tamaa kutokana na ugonjwa huo,” alisema Mama Dilu Kassam.
Mama Kassam ambaye ni mfamasia anayesomea shahada ya uzamili nchini Canada, alisema amegundua kwamba sasa huduma zinahitajika kuhamia vijijini badala ya wote wanaojitolea kufanya shughuli zao mijini peke yake. Safari hii kambi hizo zilikuwa jijini Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa upande wake Mweneyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Bw. Amin Habib alisema uzoefu walioupata umewafanya wajione kwamba wana wajibu mkubwa wa kupanua huduma katika maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa kwa sasa.
“Itabaidi tujitanue twende mbali zaidi tufike Mtwara, Mwanza, Mara hadi wilayani, lengo ni kuonyesha kwamba tunajali huduma kwa umma na kipaumbele chetu ni huduma na wala siyo biashara” alisema
Kwa upande wake Dk. Jaffer Dharsee ambaye ni Daktari Mkuu katika Kitengo cha Afya, Agha Khan, alisema huduma ni tendo la kuleta mabadiliko katika maisha ya watu lengo ambalo kwa kiwango kikubwa taasisi yake imejitahidi kulitimiza.
No comments:
Post a Comment