18 November 2010

Wananchi wafurahia pinda kurejeshwa.

Na Grace Michael

BAADHI ya wananchi wamempongeza Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, huku wakibainisha kuwa na imani naye kutokana na namna
anavyoumizwa na maisha ya wananchi wa chini na kuchukizwa na matumizi babaya ya fedha za serikali kama ya ununuzi wa magari ya kifahari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Dar es Salaam jana, walisema kuwa hawakutarajia kusikia jina tofauti na la Bw. Pinda kwa kuwa ameonesha uwezo mkubwa katika kipindi chake kilichopita.

"Bw. Pinda ni mtu wa watu anayejali watu wa chini, anayechukizwa na wafujaji wa fedha za serikali, hivyo Watanzania tuna imani kubwa naye," alisema mkazi wa maeneo ya Banana, Dar es Salaam Bw. Juma Malipesa.

Mbali na pongezi hizo, pia walimtaka katika kipindi chake kutosita kuwafukuza kazi watendaji ambao kazi yao kubwa imekuwa ni kuandaa taarifa za mezani kwa ajili ya kuziwasilisha kwa viongozi wa kitaifa wanapokwenda katika maeneo yao.

"Unajua viongozi kama wakurugenzi, wakuu wa wilaya na hata wakuu wa mikoa wamekuwa wakiandaa taarifa za mezani bila kufika katika maeneo husika na kuona hali ilivyo, taarifa hizo zinapofika kwa viongozi wa kitaifa wanaziamini huku wananchi wakighubikwa na matatizo mengi. Watu wa namna hii wasiendekezwe katika kipindi hiki," alisema mzee alijitambulisha kwa jina la Bw. Musa Shaaban.

Wakizungumzia uteuzi wa baraza la mawaziri, waliitaka Mamlaka ya uteuzi kuhakikisha wanateua watu makini wenye uchungu na mali za nchi hii na sio kuangalia uhusiano walionao kwa kuwa watu wa namna hiyo wataiangusha serikali katika utendaji.

Akizungumzia hilo, Bi. Monica Chacha alisema kuwa kimefika kipindi cha kuangalia watu wanaojali maslahi ya nchi na wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji kwa kuwa Watanzania sasa wanahitaji kuona maendeleo kwa vitendo na si kwa nadharia.

"Wananchi tumechoka kuona maisha yakizidi kuwa magumu huku kikundi cha wachache wakiishi maisha ya neema, tunaomba tupewe viongozi ambao watatuwakilisha vizuri katika nyanya mbalimbali na sio kwenda kwa ajili ya maslahi yao," alisema Bw. Chacha.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa bado wana imani kubwa na mamlaka ya uteuzi kuwa itazingatia matakwa ya wananchi na kuondoa dhana ya kupeana madaraka bila kuzingatia uwezo wa mtu husika.

3 comments:

  1. Honger Pinda kwa kupewa nafasi ambayo ulikuwa ukikilia toka muda, na hongera Jk kwa kumchagua Pinda kuwa waziri mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani Mh. Pinda ni mchapa kazi na mwenye kjali maslahi wa wananchi watanzania, tulimuona kipindi kichopita alifanya kazi kw umakni sana.

    Sasa kazi kwako Jk kuchagua baraza la mawaziri la watu wanaojali watanzania. Mungu ibariki Tz Mungu Ibari Jamh ya Tz Amen

    ReplyDelete
  2. HIVI MAALIM SEIF KATIKA KUFUATA ITIFAKI YA TANZANIA YEYE NA WAZIRI MKUU PINDA NI NANI ZAIDI? NIMEONA MHESHIMIWA SEIF KWENYE PICHA YA PAMOJA NA VIONGIZI WENGINE WA CCM AKIWA AMEULAMBA NA SUTI YA CCM, KWELI INAPENDAZA UKIWA MKUBWA, SASA SELF KAULA.

    ReplyDelete
  3. Hongera sana Pinda kwa kuchaguliwa tena kuwa waziri Mkuu. Ulifanya kazi nzuri sana na ulionesha thamani kwa waliowadogo. Kweli Kikwete uliongozwa na Mungu kumrudisha Pinda kuwa waziri Mkuu. Mungu bariki nchi yetu Tanzania.

    ReplyDelete