Na Sammy Kisika, Sumbawanga
WATU wanne wamefariki dunia kwa kuawa katika mazingira matatu tofauti mkoani Rukwa likiwamo la mtu mmoja kumchoma kisu cha tumboni rafiki yake baada ya
kuachishwa kazi ya kupasua mbao na bosi tajiri wao.
Katika tukio la kwanza, Mohamed Kijanga (32) aliuawa na rafiki yake anayefahamika kwa jina moja tu la Leonard katika kijiji cha Mapili kata ya Ilela, wilayani Mpanda
ikiwa ni baada ya siku tatu tangu afukuzwe kazi ya kupasua mbao na tajiri yake kutokana na kutokuelewana na wafanyakazi wenzake wanne.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Bw. Isuto Mantage alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 6:30 usiku muda mfupi baada ya Kijanga akiwa na wenziwe watatu
kurejea nyumbani wakitoka kunywa pombe za kienyeji.
Kamanda alisema kuwa baada ya kurejea ndani ya chumba walichokuwa wamepangishiwa na tajiri wao, walimkuta Leonard aliyekuwa amefukuzwa na tajiri wao na kutoweka kwa siku tatu bila kujulikana alikokuwa amekwenda, akiwa amelala.
Walipomkuta walianza kumuuliza ni kipi alichokifuata ndani ya chumba hicho wakati ameshafukuzwa kazi na kumlazimisha atoke ndani humo, ndipo aliinuka na kutamka kuwa alikuwa amkitafuta Mohamed.
Aliinuka na kuchomoa kisu, kisha kumchoma Mohamed Kijanga tumboni na kufa pale pale, kisha mtuhumiwa huyo akatoroka kwenda kusikofahamika na bado anasakwa na jeshi polisi.
Tukio la pili ni mzee Lazaro Kisanga (82) mkazi wa kijiji cha Mfinga kata ya Muze wilayani Sumbawanga aliuawa na mtu mmoja anayedaia kuwa alikuwa ni kichaa baada
kumkatakata kwa mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi alisema kuwa Kisanga aliuawa juzi akiwa njiani kwenda shamba ambapo alikutana na kichaa huyo aliyemnyang’anya panga alilokuwa nalo na kuanza
kumkata kata na kufa papo hapo.
Mara baada ya kumuua mzee huyo, wananchi wenye hasira kali walimzingira kichaa huyo na kuanza kumshambulia kwa silaha mbalimbali hadi kufa kisha kuuchoma moto mwili wake.
Katika tukio la mwisho, Raymound Mwanakatwe (52) alifariki dunia juzi majira ya saa 6:45 katika hospitali ya mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga alikokuwa amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi baada ya kuokotwa siku moja kabla akiwa ametelekezwa kwenye mtaro, huku akiwa na majeraha katika sehemu za kichwani na mbavuni ihali akiwa hawezi kuzungumza.
Uchunguzi wa awali wa polisi umedai kuwa Mwanakatwe alishambuliwa na Bw. Linus Mwanakatwe, ambaye walikuwa na ugomvi wa muda mrefu wakigombea mashamba.
No comments:
Post a Comment