23 November 2010

Wanaosaka uwaziri wamchelewesha JK.

*Sasa kutangaza baraza lake leo au kesho.
*Membe, Tibaijuka wagongana mambo ya nje.


Na Tumaini Makene.

WAKATI Watanzania wakiwa katika kimuhemuhe cha kusubiri baraza jipya la mawaziri, habari zimevuja kuwa mpaka jana ilikuwa imeshindikana kutangazwa kutokana na
mambo kadhaa likiwamo shinikizo la baadhi ya maswahiba wanaoshinikiza wateuliwe katika baraza hilo kwa majaliwa yao kisiasa, hasa urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Habari hizo pia zimezidi kutaja majina ya watu yenye uwezekano wa kuteuliwa katika baraza hilo, likiwa na sura kadhaa mpya, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa Chama Cha Wananchi (CUF) kupata nafasi katika baraza hilo.

Habari kutoka vyanzo vya kuaminika katika duru za kisiasa, hasa serikalini zimelithibitishia Majira kuwa marafiki wa Rais Kikwete bado wanatia shinikizo wakitaka wawemo katika baraza jipya la mawaziri kwani kinyume chake itakuwa ni sawa na kutangaziwa maafa katika harakati zao za kusaka madaraka ya juu kisiasa.

Imezidi kuelezwa kuwa mantiki ya shinikizo hilo la maswahiba wa rais kuwemo katika baraza hilo, inasababishwa na ukweli kuwa itawapatia nafasi ya kushikilia madaraka ambayo yatawafanya kuwa karibu na wananchi, huku wakiendeleza mikakati yao ya kujiimarisha kisiasa, kwa majaliwa ya baadaye, hasa wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uchaguzi mkuu wa 2015.

Habari hizo zilisema kuwa maswahiba hao wanashinikiza uteuzi wao au wa watu wao wengine wa karibu katika mikakati yao ya kisiasa, ikidaiwa kuwa wamesema wakikosekana katika baraza hilo na serikalini kwa ujumla itakuwa ni sawa na kutangaziwa mwisho wa zama zao za kisiasa Tanzania na hasa ndoto zao za kushika madaraka makubwa nchini.

Imeelezwa kuwa hofu ya kugombania kuwemo katika baraza la mawaziri inatokana na kuwa mwaka 2015 kutakuwa na mabadiliko ya uongozi ndani ya CCM, ambapo mgombea urais mpya atakuwa anachaguliwa, hivyo washinikizaji wamedaiwa kusema ni bora wakaingia na mtu ambaye wanamfahamu kuliko aingie mtu ambaye si 'mwenzao' kwani itakuwa hatari kwa mstakabali wa maisha yao kisiasa.

"Mpaka sasa baraza halijatangazwa kwa sababu akina...(anataja majina yao washinikizaji) wanataka wateuliwe katika baraza la mawaziri, wanasema kuwa wasipoteuliwa ni sawa na kumaliza mbio zao za kisiasa, wanalalamika kabisa kuwa watakuwa wametangaziwa mwisho wao wa kisiasa hasa majaliwa yao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

"Wanasema kuwa mwaka 2015 ni mwaka wa change of guard (mabadiliko makubwa ya uongozi) hasa katika nafasi ya urais, kwa sababu atakuwa anaingia rais mpya, hivyo hawajui nani atakayeingia, hivyo wakitoswa sasa hivi wanaona kuwa itakuwa ni hatari kwao...wanataka wawemo serikalini ili kujipanga," alisema mmoja wa wapashaji habari wetu.

Habari hizo zilisema kuwa ingawa kuna uwezekano mkubwa wa Bw. Bernard Membe kurudi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuna shinikizo kubwa la watu wanaosemwa kuwa karibu na taasisi ya urais, wakitaka asirudishwe katika nafasi hiyo kwani atakuwa tishio kwani atakuwa na mazingira mazuri ya 'kuelekea' ikulu, ambapo amekuwa akitajwa kuwa ni kati ya watu wenye matamanio ya kuwania kiti hicho ndani ya CCM mwaka 2015.

Lakini pia mbali na shinikizo la kutaka Bw. Membe asirudishwe katika nafasi hiyo ili kuyumbisha kile kinachoitwa mikakati yake ya urais, imeelezwa kuwa uwaziri wa wizara hiyo una changamoto kubwa kwani Rais Kikwete anataka kuendeleza imani yake kwa wanawake katika wizara hiyo kama alivyomteua Bi. Asha-Rose Migiro, kabla hajateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

"Wengine wanaona kuwa nafasi hiyo inamstahili zaidi Profesa Tibaijuka (Anna) kwani inadaiwa kuwa aliitwa kurudi nyumbani agombee ili atumike katika nafasi hiyo, lakini tatizo linakuja kuwa ukimwondoa Membe hapo unaonekana kabisa kuwa umekatilia mbali mipango yake, lakini pia unampeleka wapi...labda wizara ya mambo ya ndani alikokuwa kabla...lakini pia wengine wanataka Prof. Tibaijuka apewe wizara inayohusika na makazi, kwani ndiyo hasa fani yake aliyokuwa akiifanyia kazi huko UN, ashughulikie tatizo la makazi holela na migogoro ya ardhi.

"Wizara ya Afya haina tatizo Prof. Mwakyusa (David) atarudi, akina Makamba (January), watakuwa junior ministers tu (naibu waziri) lakini pia kuna uwezekano CUF watapata nafasi...hii ni kutokana na makubaliano ya mwafaka huko Zanzibar, majina yanayotajwa hapa ni Hamad Rashid Mohamed na Habib Mnyaa...lakini hapa pia kuna issues (masuala) mbili zinatatiza...inahojiwa.

"Wizara nyingine yenye mgogoro ni wizara ya masuala ya fedha na uchumi, hapa alisemwa Dkt. Cyril Chami, lakini anaonekana kuwa ni man of principles (mtu mwenye msimamo) hawezi kupelekeshwa...pale wanataka mtu ambaye wakubwa wakisema wanataka hiki anafuata tu bila kuhoji, hivyo yeye anafikiriwa kupewa uwaziri kamili wa Viwanda, Biashara na Masoko, ili hapo fedha atafutwe mwingine...labda Meghji (Zakia Hamdan).

Wengine waliotajwa ni pamoja na Prof. Makame Mnyaa Mbarawa aliyeteuliwa ubunge hivi karibuni na Rais Kikwete ubunge, ambaye ameelezwa kuwa anaweza kupewa wizaya ya masuala ya elimu, huku Bi. Zakhia Meghji akiendelea kutajwa pia.   

15 comments:

  1. Muafaka wa CCM na CUF ni kwa nchi ya Zanzibar na si bara CUF Haikuwa na mgogoro na CCM bara msituchanganye na vyama venye mlengo wa uislam huku bara tazama kampeni zote za CUF bara ni sehemu zenye uislam tu.Tafadhari JK usilete bara Matitizo ya Zanzibar.Kasanga

    ReplyDelete
  2. another gossip, this is another unfounded speculations!

    ReplyDelete
  3. mnaacha habari za maana mnatumika kuwakampenia watu wanotishiwa nafasi zao za awali, halafu baadaye mnaanza kuwalaumu watu kumbe vyanzo ni ninyi wenyewe. kwani cheo akipewa mwingine kuna ubaya gani kama ni msafi na anaweza kazi?, acheni hizo rushwa za maandishi na mashinikizo ya kumtisha na kumfanya Rais JK achague viongozi kwa mapenzi yenu kwa vijisenti. andikeni vitu vya maana vingi vinavyoonekana na kusikika mnaandika vyenye maslahikwenu na kalamu zenu badala ya maslahi ya Taifa.Saidi Sadick Lindi

    ReplyDelete
  4. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 23, 2010 at 9:57 AM

    Kwani habari hii ni ya kampeni au? Mwacheni Kikwete aharibu au kutengeneza mwenyewe.Halafu kufanya hivi ni kuwavimbisha vichwa watu kuwa eti watamrithi Kikwete.Hakuna cha Membe,Lowassa,Tibaijuka,Migiro wala nani sijui..wananchi ndio watakaoamua kuhusu nani awe Rais 2015.Na mwaka huo,kitaeleweka kweli...subiri muone.

    ReplyDelete
  5. Sipendi kuingilia taaluma ya habari, lakini si hekima mwandishi kutumbukiza dhana zake akazisukumia kwa vyanzo visivyokuwepo. Ni sawa na uchochezi, hasa kwa Watanzania wa leo wasiopisha chambo hata kwa kauli pepe kiasi gani.Huhitaji kuwa mwandishi wa habari Tanzania hii kujua kwamba CCM haiwezi kuwa na mpango wa kuijumuisha CUF kwenye uwaziri. Kwa kigezo kipi? Kama kuna wanaosema hivyo, ni wachache wasioelewa mambo, na magazeti hayapaswi kuripoti kila kauli ya kila mzushi. Mbona haijaripotiwa jinsi watu kule Kariakoo wanaposema kwamba mpenzi wa Timu fulani alifariki kama kafara baada ya Timu yake kuishinda timu pinzani? Si yanasemwa? Hayaripotiwi kwa sababu hayana mantiki.Lakini kwenye siasa, kila jambo lisipokuwa na mantiki zaidi ndivyso linavyoripotiwa zaidi. Waandishi na magazeti yenu mnataka kutupeleka wapi?

    ReplyDelete
  6. wewe kasanga ni mdini na mnafiki mkubwa ktk nchi hii. mbona chadema hajaenda mtwara Luindi wala Tanga? nayo ni dini gani? acha chembechembe za ushetani.

    ReplyDelete
  7. He kumbe Zanzibar ni nchi? hebu muulizeni tena Pinda na uso wake uliopindapinda!

    ReplyDelete
  8. Wachaguliwe watu waadilifu, siyo kufuata majina ya watu mashughuli "we want to see changes". Ukiwa wazri lazima utumikie jamii na kuanglia ni mambo gani ya msingi wananchi waliahidiwa kuyatekeleza.

    ReplyDelete
  9. Membe mbakaji asipewe tena mambo ya nje atatutia aibu, CUF hawahusiki bara, wao nchi yao Zanzibar, Makamba junior asipewe, ni kumpa bichwa makamba senior, au la basi Masauni naye apewe kuleta usawa

    ReplyDelete
  10. Lakini Tanzania ni ya wakubwa tu. We angalia wapi Makamba jr. ameanzia. Ni wakuletwa tu ndo maana utakuta kapata nafasi kubwa Ikulu huku kuna watu walioota vipara huko na elimu zao. we acha tu. Utaona anachaguliwa kuwa pengine waziri kwa maaana mipango ya wakubwa hawa ni ya muda. Wanajua

    ReplyDelete
  11. Hatufanyi biashara ya uridhi hii sio nchi ya kifalme . Eti leo Prince makamba hatutaki vinginevyo tutakwenda CHADEMA WOTE

    ReplyDelete
  12. january makamba apewe uwaziri wa mambo ya nje na ridhiwani naibu waziri

    ReplyDelete
  13. ridhiwani apewe wizara ya fedha

    ReplyDelete
  14. hizi ni idiology zilizokufa kabla hazijaanza, utopian ideas ya kuchagua nafasi na mtu wake. kuna mambo mawili hapa technique know who and technique know how naamini ni time ya technique know how kwa sasa maana tunakiu ya maendeleo sasa, wasomi wa mambo ya afya, hela, elimu, maendeleo na uhusiano wanajulikana tayari, kwa hiyo rais atazame kwa makini sana

    ReplyDelete
  15. Waandishi wa habari nao ni watupu kama wanasiasa wenyewe.Kilichosemwa hapo sikioni. Aibu!!Nendeni mkasome kwanza.

    ReplyDelete