19 November 2010

Wanafunzi wataka vita ya ufisadi CCM.

Na Peter Saramba, Dodoma

UMOJA wa wanafunzi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa vyuo vikuu Mkoa wa Dodoma umewataka wabunge vijana wa chama hicho kuongeza kasi na nguvu ya
kupambana na ufisadi ndani na nje ya bunge ili kurejesha imani ya wananchi kwa chama hicho tawala.

Katika risala yao waliyoisoma wakati wa sherehe za kuwapongeza wabunge vijana wa CCM zilizofanyika mjini hapa juzi, umoja huo uliwaeleza wabunge hao kuwa ufisadi ndio kero kubwa kwa wananchi, hivyo lazima waufanyie kazi kwa manufaa ya chama na nchi kwa
ujumla.

Akisoma risala hiyo mbele ya wageni rasmi, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Bw. Bernard Membe, mbunge wa Mtama, Mwenyekiti wa wanafunzi wa Chuo cha Mipango, Bw. Kwagilwa Nhamanilo alisema kudhani ufisadi ni tatizo dogo ndani ya chama na taifa ni kujidanganya, hivyo kinachohitajika ni kushughulikia tatizo hilo
kwa nguvu na kasi zaidi.

"Ni wazi kuwa suala la ufisadi limekuwa kero kubwa kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao, hakuna anayeweza kujidanganya kuwa hilo ni tatizo dogo kwani kila kona ukitembea utasikia kilio cha wananchi dhidi ya ufisadi. Mnapaswa kuongeza kasi na nguvu dhidi ya vitendo hivi ndani na nje ya bunge kwa ajili ya ustawi wa chama na
taifa letu," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya kurasa mbili.

Katika kutekeleza majukumu yao, wabunge vijana wametakiwa kuonyesha kwa vitendo kuwa vijana ni taifa la leo, kesho na keshokutwa kwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi utakaodhihirisha kuwa vijana wakipewa nafasi wanaweza, na hivyo kupalilia njia kwa vijana waliopo vyuoni wanaotarajia kuingia kwenye siasa na uongozi wa umma kuaminika.

Jukumu lingine walilokabidhiwa wabunge hao vijana ni kuhakikisha marekebisho yanafanyika katika suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo mikopo inayotolewa haikidhi mahitaji halisi, huku baadhi ya taratibu za bodi ya mikopo zikiwakandamiza au kuondoa kabisa uwezekano wa upatikanaji
wake.

"Tunawaomba mjenge hoja ya ongezeko la mikopo na uboreshaji wa sheria za mikopo, ili kutoa fursa zaidi kwa vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu bila kukwama kutokana na vikwazo vya upatikanaji mikopo," ilisema taarifa hiyo.

Wasomi hao pia wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwakumbuka vijana katika muundo wa serikali na baraza lake la mawaziri atakalounda hivi karibuni kwani uzoefu umeonyesha kuwa wabunge vijana katika bunge lililopita walimudu nafasi zao.

Akitoa salamu mmoja wa wageni waalikwa katika serehe hizo, aliyekuwa waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa katika serikali iliyopita, Bw. Bernard Membe alisem  anaamini vijana watapatiwa nafasi za uwaziri katika serikali ijayo huku akiwaomba wabunge vijana kuondoa hofu.

Bw. Membe aliyeonekana kuzolewa na hamasa kubwa iliyokuwepo kwenye sherehe hizo alienda mbali kwa kuahidi kuwa serikali itarekebisha na kutatua kero zilizopo kwenye bodi ya mikopo ya elimu ya juu kwa kutenga fedha zaidi na kuongeza nafasi za vijana wanaojiunga na elimu ya juu ni hiyo imeahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

"Lengo ni kuhakikisha vijana wengi wanajiunga na kupata elimu ya juu ili kuandaa viongozi wa siku zijazo kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 50 ijayo. Wale jamaa zetu wa magwanda walitubipu katika vyuo vikuu sasa sisi tunawapigia kwa kuhakikisha hamasa hii ya vijana wa CCM inaenea katika vyuo vyote
nchini," alisema Bw. Membe.

Ingawa hakutaja chama au jamaa wa magwanda aliokuwa akiwazungumzia, ni wazi alikuwa akikilenga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ndio hutumia magwanda kama mavazi rasmi ya chama hicho na kimekuwa kikiungwa mkono na wasomi na wanazuoni
wa vyuo vikuu nchini.

Katika uchaguzi mkuu uliopita serikali iliamua kufunga vyuo vya elimu ya juu hadi baada ya zoezi la uchaguzi huku ikidaiwa kuwa jambo hilo lililenga kuwanyima wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakionekana kuunga mkono upinzani wasiptate fursa ya kupiga kura kwa sababu wengi wao walijiandikisha maeneo ya vyuoni.

Sherehe hizo ziliandaliwa na kuratibiwa na mbunge wa Singida Kaskazini, Bw. Lazaro Nyalandu ambaye ni mwenyekiti na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mara, Bi. Ester Bulaya aliyekuwa katibu wa sherehe na wabunge vijana wa CCM.

3 comments:

  1. Safi sana vijana maneno mazuri mradi uende mbele lakini Rohoni unajua mwenyewe hiyo ndio mnajua mnge soma vizuri lakini mafisadi wamezuia jasho lenu mpaka uwe na kijani. Sasa mshinikize babu yenu makamba aondoke vijana wana mambo ya kitecknologia sio ushabiki tena. Tanzania mambo ya kuimba au kumwabudu mtu yalishapitwa na wakati. Kwanza sidhani kama CCM wanasoma maoni kwenye web site za magazeti. Vijana pambaneni msichoke sasa wanataka kuwalaghai na CCM yao. Fikiria maisha wanayoishi wazazi wako, jirani yako, mjomba, shangazi, nk halafu utathimini ni kwa nini? Ni kweli haliwezekani au linawezekana sasa kama linawezekana kwa nini tusiseme basi.

    ReplyDelete
  2. NANI ALIKUAMBIA KUWA CCM WANAWEZA KUPIGA VITA UFISADI? HIVI KWELI MNASOMA CHUO KIKUU STILL YOU DON'T KNOW THE TYPE OF YOUR LEADERS IN THAT CORRUPTED PARTY? CCM HAS NOTHING NEW TO OUR COUNTRY...THIS TIME CCM IS GOING MORE TRIBULATION IN THE COUNTRY AND THOSE WHO VOTED FOR CCM WILL REAP THE BITTER HARVEST.

    ReplyDelete
  3. ccm hamna jipya mnadhulumu watanzania,mwalimu alisema ccm imepoteza muelekeo,

    ReplyDelete