Na Addolph Bruno
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Grand Malt imeandaa tamasha maalumu kwa vyuo vikuu, litakalofanyika Jumamosi katika viwanja vya
TCC Chang'ombe, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema tamasha hilo litashirikisha vyuo zaidi ya 20 vya elimu ya juu, vilivyopo Jijini Dar es Salaam.
Alisema lengo la tamasha hilo ni kuwakutanisha wasomi katika nyanja ya burudani, ikiwa ni pamoja na kuwakaribisha wanavyuo wapya wanaoanza mwaka wa kwanza wa masomo 2010/2011.
"TBL kupitia Grand Malt tumeamua kudhamini tamasha hilo, kutokana na kutambua na kuthamini umhimu wa wanavyuo katika ujenzi wa taifa, hivyo kukutana kwao pamoja kutasaidia kuendeleza na kudumisha uhusiano waliokuwa nao, tunawakaribisha na wengine ambao hatukuweza kuwaalika, waje waungane na wenzao," alisema Consolata.
Nao wawakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kayumba Totokoko na Lawrence Mwalasalu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa niaba ya vyuo vingine, walisema wamelipokea tamasha hilo na kuahidi kushiriki pamoja na kuwataka wanafunzi wenzao kuhudhuria kwa wingi.
Vyuo ambavyo vitashiriki tamasha hilo ni UDSM, Chuo cha Uandishi wa Habari (DSJ), Chuo cha Biashara (CBE), Chuo cha Ustawi wa Jamii, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo cha Uhasibu (TIA) na vingine vingi.
No comments:
Post a Comment