Na Anneth Kagenda,Dar es Salaam.
UMOJA wa Wafanyabiashara wenye Ulemavu Dar es Salaam (UWAWADA), umesema kuwa kamwe hautakubaliana na uongozi uliokuwepo madarakani kwa miaka mitano kuendelea
kuwaongoza kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza wakati ukiwa madarakani.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa UWAWADA na wafanyabiashara wenzao uliohusu kupinga uongozi huo kurudi madarakani.
Mwenyekiti wa muda wa Kamati Teule UWAWADA, Bw.Tobias Lyankulia alisema wafanyabiashara hao wamechoshwa na ubabaishaji wa uongozi huo ambao nao unajiita UWAWADA ambapo tangu kuingia kwao madarakani umeshindwa kufanya mikutano ili kujua matatizo yanayowakabiri watu wanaowaongoza.
"Tunachotaka ni mageuzi, pamoja na kwamba sisi ni walemavu lakini tumekuwa hatutendewi haki, tunanyanyapaliwa huku wengine hadi leo hawajapata vizimba vya kufanyia shughuli zao hivyo mwaka huu lazima tufanye mabadiliko," alisema Bw. Lyankulia.
Aidha alisema kuwa uongozi huo pia umekuwa ukichangisha fedha holela bila kuwa na utaratibu unaoeleweka hivyo kuwafanya wahusika kutojua fedha hizo zinakwenda wapi na zinafanya nini jambo lililosababisha uongozi wa muda kukaa na kuzungumzia matatizo hayo na kuona kwamba ni bora ukachaguliwa uongozi mwingine utakaoshughulikia matatizo ya wafanyabiashara hao.
"Tunachojua ni kwamba uongozi uliokuwepo madarakani ambao nao unajiita UWAWADA unategemea kufanya uchaguzi kwa ajili ya kuteua uongozi mpya lakini tumeisha fika katika vyombo vya usalama pamoja na kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kupinga uchaguzi huo kutokana na kwamba hatuutambui na hauna lengo zuri kwa wafanyabiashara," alisema.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja huo Bw. Mohamed Chinyapi alisema kuwa awali walitaka kukaa na kufanya mazungumzo na upande wa pili lakini jambo hilo lilipingwa vikali na kupelekea kutokuwapo maelewano.
Alisema kuwa kutokana na kwamba maelewano hamna basi UWAWADA haitakubaliana na uchaguzi wa uongozi mpya na kusema kuwa lengo lao lilikuwa ni walemavu kumaliza tofauti walizonazo ili kuwapo Amani, upendo na taratibu kufuata mkondo wake.
"Tusingependa tuwe na migogoro isiyokwisha ila kuwa na ushirikiano katika kufanya shughuli zetu na kuwepo kwa ushirika ni moja ya sababu zinazoweza kutuletea amani na upendo kuliko kurumbana jambo ambalo halina faida kwetu na jamii nzima inayotuzunguka," alisema Katibu huyo.
No comments:
Post a Comment