23 November 2010

Mzambia wa Yanga atua nchini.

Na Elizabeth Mayemba

MSHAMBULIAJI raia wa Zambia, Davies Mwape ambaye Yanga inataka kumwongeza katika kikosi chake katika dirisha dogo la usajili ametua nchini kwa ajili kumalizana na
uongozi wa klabu hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Mwape alisema amekuja kufanya mzungumzo na uongozi wa Yanga na endapo watakubaliana ataichezea timu hiyo, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Mchezaji huyo aliyekuwa akichezea Klabu ya Konkola Blades alisema,  akikubaliana na uongozi wa Yanga atamwaga wino kwa ajili ya kuichezea timu yao.

"Ndiyo nimefika lakini la kwanza ni kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga na endapo tutakubaliana, ninawezaa kuingia mkataba wa kuichezea timu hiyo," alisema Mwape.

Klabu nyingine alizowahi kuzichezea mchezaji huyo ni Orando Pirates na Jomo Cosmo za Afrika Kusini na Zanaco ya Zambia, pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Zambia kwa miaka minne na timu ya taifa ya wakubwa 'Chipolopolo'.

Wakati huo huo, kikao cha Kamati ya Utendaji cha Yanga na Mdhamini wake Mkuu Yusuf Manji, kilichokuwa kifanyike mwishoni mwa wiki iliyopita sasa kitafanyika leo.

Awali Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, ilipanga kukutana leo lakini waliahirisha baada ya Manji, kutakiwa kusafiri ambapo walilazimika kukutana Jumamosi iliyopita hata hivyo ikashindikana, baada ya viongozi kutokamilika.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema ni kweli walitakiwa kukutana mwishoni mwa wiki, lakini idadi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji haikutimia.

Sendeu alisema ajenda kubwa ya kikao hicho ni kujadili masuala ya usajili wa dirisha dogo, pamoja na kuzungumzia maendeleo ya klabu hiyo.

Alisema katika kikao hicho wamemwalika Manji ili na yeye aweze kutoa mchango wake wa mawazo wa nini kifanyike, hasa katika kipindi hiki ambacho timu yao inakabiliwa na michuano ya kimataifa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment