24 November 2010

Udini wapenya uchaguzi wa meya Tanga.

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MBIO za kumsaka Meya wa Jiji la Tanga, zinazidi kupamba moto huku kukiwa na suala la udini likipenyezwa na  baadhi ya wagombea kuchafuliwa kwa tuhuma walizokuwa nazo wakiwa
watumishi wa serikali kabla ya kuingia kwenye udiwani.

Uchunguzi uliofanywa na Majira katika Jiji la Tanga umebaini kuwa kati ya wagombea saba waliochukua fomu za kugombea kiti hicho, sita wanaelezwa kwamba hawafai kushika nafasi hiyo kutokana na tuhuma mbalimbali wanazaokabili wakati wakiwa watumishi wa serikali.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, Bw. Shekue Pashua aliwataja waliochukua fomu kata zao kwenye mabano ni pamoja na Bw. Omar Guled (Ngamiani Kaskazini), Bw. Danny Mgaza (Mzizima), Bw. Muhina Mustafa 'Seleboss' (Nguvumali), Bw. Abdi Abu (Tangasisi), Bw. Fadhil Bwanga (Mzingani), Bw. Telesphor Chambo (Chumbageni) na Bi. Mwana-Uzia Juma (Pongwe).

Wengine ni Bw. Muzamil Shemdoe (Mabawa) na George Mayala (Kiomoni) ambao wameomba Unaibu Meya na Rukia Mapinda na Saida Ghadaf wameomba ukatibu wa madiwani.

Uchunguzi huo umebaini tayari kuwepo kwa taarifa kutoka katika idara mbalimbali walizokuwa wakifanya kazi wagombea hao, zikiwaelezea kuwa hawafai kugombea.

Moja ya chanzo kilisema kuwa kamati inayohusika na uteuzi huo imekuwa ikipokea taarifa hizo na kuzijadili na nyingi zinaonesha wagombea hao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali hasa katika hoja ya udini na usaliti katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu.

"Wamejadiliwa na majina yao yamepewa alama kulingana na sifa zao, lakini sisi wajumbe tumekuta karatasi zenye taarifa mbalimbali za tuhuma za wagombea wote walioomba, kwa kweli wapo wenye tuhuma nzito ambazo kama chama itabidi zizingatiwe unajua wengine hawakuonesha uaminifu huko walikotoka serikalini," kilisema chanzo hicho.

Majira ilishuhudia moja ya karatasi zenye majina ya wagombea wanaotuhumiwa na tuhuma wanazokabiliwa nazo.

Chanzo hicho kilisema kikao hicho kilijadili majina yote lakini hoja ya udini ilionekana kuchukua nafasi zaidi hasa pale wajumbe wa kikao hicho walipotaka meya wa jiji hilo kuwa muislamu kutokana na historia ya wakazi wa Tanga.

Alisema kutokana na historia hiyo jiji hilo halikuwahi kuongozwa na meya kutoka katika dini ya hiyo.

Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na baadhi ya wajumbe ambao walitaka meya wa jiji hilo achaguliwe kwa kuzingatia uwezo, uadilifu na kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ikiwemo miongozo ya Serikali za Mitaa
(TAMISEMI).

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga, Bw. Pashua alikanusha kuwepo kwa taarifa hizo.

Alisema anashangazwa na taarifa hizo kwa kuwa wagombea wakristo ni wawili na wamepewa alama nzuri za mapendekezo ya sifa za kustahili kuwa Meya.

Alisema majina ya wagombea hao tayari yamewasilishwa katika ngazi ya mkoa kwa ajili ya hatua zaidi kwa kuwa kikao hicho hakina mamlaka ya kuteua meya.

Hadi jana tunapoelekea mitamboni kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tanga kilikuwa kikiendelea kwa ajili ya kuchuja majina ya wagombea.

Wakati huo huo mwandishi wetu Humphrey Shao naripoti kuwa jumla ya ya madiwani 13 Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani Temeke wamejitokeza kuchukua fomu ya kuwania kiti cha umeya katika  Manispaa ya Temeke na jiji.

Akizungumza na mwandishi wa Majira Dar es Salaam jana, Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke Bw. Saadi Kusirawe alisema kuwa mpaka sasa madiwani waliojitokeza ni 10, wawili wamechukua fomu ya unaibu meya na mmoja kachukua fomu ya unaibu meya wa jiji.

Aliwataja kuwa madiwani hao na kata zao katika mabano kuwa ni Bw. Keny Makinda (Vituka), Bw. Ally Kinyaka  (Mtoni), Bw. Noel Kipangule (Chang'ombe), Bw. Francis Mtawa  (Keko) na Bw. Andeson Chale (Mtoni Kijichi),

Wengine ni Bi. Zena Mgaya (Tandika) Bw. Shabani Nsombo (Temeke) 14, Bw. Victor Mwakasindile (Makangarawe) Bi. Cesilia Macha  (Mianzini Charambe) na Bw. Mabadi Selemani (Pemba Mnazi Kigamboni).

Aliwataja waliochukua fomu ya kugombea kiti cha Unaibu Meya ni Bw. Sanya Muhidini  (Kimbiji) na Bw.Abdalah Chaulembo (Kurasini) Bw. Wilfred Kimath  amechukua fomu ya kugombea Unaibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam.


"Idadi ya madiwani walio chukua fomu ni ya kutosha hivyo tunasubiri kuyapeleka majina yote katika Halmashauri Kuu ya Wilaya na kuyapitisha kwenda mkoani kisha taifa, ili kuletewa majina matatu yatakayopigiwa kura na madiwani wa CCM kumpata mmoja atakaye wawakilisha katika uchaguzi wa Manispaa," alisema Bw. Kusirawe.

No comments:

Post a Comment