24 November 2010

Leo ndiyo leo.

*Rais Kikwete kuanika Baraza lake la Mawaziri.
*Ikulu yathibitisha, yakwepa kutaja muda, mahali.


Na Tumaini Makene.

LEO ndiyo leo. Muda wowote, kwa njia yoyote na mahali popote, kadri itavyoonekana kufaa, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuweka wazi baraza lake jipya la mawaziri litakalomsaidia
kuendesha serikali katika awamu yake ya mwisho ya uongozi.

Taarifa fupi kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema "Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atatangaza Baraza jipya la Mawaziri kesho (leo), Jumatano Novemba 24, 2010. Rais Kikwete atatangaza Baraza la Mawaziri hilo jipya kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Oktoba 31, mwaka huu 2010."

Majira lililopataka kujua muda ambao Rais Kikwete atatangaza baraza hilo, mahali na njia atakayotumia, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Salvatory Rweyemamu alijibu "hayo mambo yote unayouliza yamekuwa withheld deliberately (hayakusemwa kwa makusudi) tutawataarifu ikishakuwa tayari, si bahati mbaya, hayajasemwa kwa makusudi kabisa, tutawataarifu tu."

Pamoja na hayo, Majira limezidi kupata taarifa kutoka vyanzo vya ndani, vilivyo karibu na mamlaka za uteuzi zikisema kuwa mbali ya kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wanaotaka wateuliwe kuongoza wizara nyeti kwa ajili ya kukidhi matamanio yao ya kisiasa baadaye, zipo sababu zingine tatu zilizochelewesha utangazaji wa baraza hilo jipya, kwa siku kadhaa sasa.

Sababu hizo zimeelezwa kuwa ni hoja ya dini ambayo  kwa siku za karibuni imeingizwa vichwani mwa Watanzania, ukanda na suala la watu wasomi wenye taaluma katika fani fulani, wateuliwe katika nafasi ambazo zinaendana na taaluma zao ili watumikie kwa ufanisi badala ya hali ilivyo sasa ambapo watu wanateuliwa kisiasa zaidi.

"Unajua suala la udini hapo kabla halikuwepo, limeibuliwa siku za hivi karibuni tu, halikuwepo kabisa hili suala huko nyuma, sasa hilo nalo limesababisha utangazaji wa mawaziri uchelewe maana inabidi kulingalia kwa makini...lakini pia kuna suala la ukanda, unajua kati ya mambo yaliyochangia kuwa na watu wasiokuwa na uwezo katika baraza lililopita ni kuangalia uwakilishi wa kanda.

"Yaani karibu kila kanda au mkoa ulikuwa na waziri, hii si sahihi, safari hii ilikuwa muhimu kuangalia uwezo wa mtu zaidi si kule anakotoka, ukitaka kuridhisha kanda au mkoa inasababisha mambo ya hovyo, uwezo wa mtu ndiyo kitu cha msingi hapa," kilisema chanzo chetu cha habari, ambacho jina lake linahifadhiwa.

Kiliongeza kwa kusema "kitu kingine ni suala la taaluma za wasomi wanaoteuliwa kushika nafasi za kisiasa, imeshauriwa kuwa wapewe nafasi zinazoendana na fani zao, kama mtu ana udaktari wa falsafa (PhD) basi iangaliwe paper (chapisho/utafiti) yake aliandikia kitu gani, hicho ndicho akakifanyie kazi, si kuteuliwa kisiasa tu, hii ya kuteuana tu imesababisha baadhi ya mawaziri ku-mess up things (kuharibu mambo) vibaya sana, kwa sababu wanajikuta katika mambo wasiyokuwa na uelewa nayo hata kidogo."

Hata hivyo katika suala hilo la mtu kutumika katika fani ya taaluma yake, chanzo chetu kilieleza kuwa linahitaji kuangaliwa kwa uzuri, kwa sababu iko mifano hai ambapo mawaziri wenye sifa za uwezo, umakini na ufuatiliaji wa mambo, wamewahi kuongoza wizara mbalimbali na kote walionekana kufaa pamoja na kuwa elimu zao zinaonesha kuwa hawana taaaluma wala utaalamu na wizara husika.

Ilielezwa kuwa suala hilo linahitaji kutazamwa vizuri kwa sababu katika wizara watendaji wakuu wanapaswa kuwa ni makatibu wakuu, ingawa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na 'tatizo' la watendaji hao kuhamishwa ovyo, hivyo nao kujikuta wakitumika katika wizara ambazo hawana utaalamu nazo, hivyo wanapokutana katibu na waziri wote hawana taaluma au utaalamu wa wizara husika tatizo linakuwa kubwa zaidi, na kuongeza uwezekano wa wizara kutofanya vizuri.   

Taarifa hiyo ya ikulu inaifanya siku ya leo kuwa ni siku ya kutambua mbivu na mbichi, juu ya sura zipi hasa, mpya na zile za zamani, zitakuwemo katika baraza jipya pale ambapo Rais Kikwete atakuwa akitumikia ngwe yake ya pili ya uongozi, baada ya uchaguzi mkuu uliopita ambapo alishinda kwa asilimia 61 ikiwa ni takribani pungufu ya asilimia 20 ya ushindi alioupata mwaka 2005.

Baraza hilo limekuwa likisubiriwa kwa hamu na Watanzania walio wengi, huku baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini wakisema kuwa ndiyo turufu ya muhimu kati ya chache alizobaki nazo Rais Kikwete kuweza kurudisha matumaini ya Watanzania kwa serikali yake, kwani imekuwa ikielezwa kuwa serikali katika awamu yake ya kwanza haikuweza kukidhi matarajio makubwa ya wananchi, kama walivyoahidiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambapo walimpatia ushindi wa asilimia 81..

Pia imekuwa ikielezwa kuwa, uteuzi pamoja na muundo wa baraza hilo utaonesha picha ya agenda ya serikali na rais mwenyewe kwa miaka mitano ijayo, hasa katika kuwa na viongozi wanaowatumikia wananchi na maslahi ya taifa kwa ujumla, ikichukuliwa kuwa Baraza la Mawaziri ndilo mshauri mkubwa na wa karibu wa rais katika utendaji kazi wa serikali kwa kila siku.

Wakati ikulu ikitoa taarifa hizo, fununu za uwezekano wa wapinzani kupata nafasi katika baraza hilo jipya la Rais Kikwete, zaimezidi kuenea, huku ikielezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa Chama Cha Wananchi (CUF) kikafanikiwa kuwa nafasi katika baraza jipya la mawaziri kutokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofanyika Zanzibar, na chama chenye wabunge wengi wa upinzani, CHADEMA kukataa matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Kikwete.

"Wizara ya Afya haina tatizo Prof. Mwakyusa (David) atarudi, akina Makamba (January), hao watakuwa junior ministers tu (naibu waziri) lakini pia kuna uwezekano CUF watapata nafasi...hii ni kutokana na makubaliano ya mwafaka huko Zanzibar...majina yanayotajwa hapa ni Hamad Rashid Mohamed na Habib Mnyaa.

Baraza hilo litatangazwa leo baada ya takribani wiki moja tangu Rais Kikwete amteue Waziri Mkuu Mizengo Pinda ili wasaidiane kuunda serikali, huku pia kukiwepo na habari zinazovuja kuwa kumekuwepo na watu wanaotajwa kuwa ni maswahiba wa rais, kushinikiza wao wenyewe au watu waliokaribu nao kuteuliwa katika wizara nyeti, ikidaiwa kuwa ni mkakati wa makundi yanayojipanga kuwania urais mwaka 2015.

Imeelezwa kuwa wizara zinazomezewa mate na baadhi ya wanasiasa hao ni zile nyeti kama vile inayohusika na mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, wizara ya mambo ya ndani, inayohusika na tawala za mikoa na serikali za mitaa na ile ya mambo ya ndani ya nchi.

Wizara zingine zinazomezewa mate, ambapo imeelezwa kuwa wanasiasa wanapigana vikumbo, kuhakikisha wanazipata kulingana na makundi ya wanaowania urais kupitia CCM yalivyojipanga ni pamoja na ile inayohusika na ulinzi, elimu na miundombinu, ambayo imeleezwa kuwa ni kivutio kwa kuwa inahusisha tenda nyingi na nono za ujenzi.  

9 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 24, 2010 at 9:09 AM

    Hata kama kuna ucheleweshaji wa namna gani,hakutakuwa na jipya..watu watakuwa walewale,mambo yaleyale,urasimu uleule..mvinyo uleule ukibadilishwa chupa tu.Kiukweli CCM ni wajuzi wa kucheza na akili za watu.Eti Rais anajifanya kuchelewesha Baraza ili watu wamuone kuwa yuko makini kupangan safu makini ya kufanya kazi vyema.Hakuna lolote..usanii mtupu! Kwani nani hamjui Rais Kikwete anavyojua kumpa tension mwananchi wakati anapotaka kufanya mambo yaliyo katika mamlaka yake.Nani hakumbuki jinsi Rais Kikwete alivyotangaza kwa mbwembwe Baraza lake alilomaliza nalo baada ya lile la akina Lowassa kuvunjwa? Eti mwishoni akamalizia kwa kusema'nimemaliza...wamekwisha'.Nani hakumbuki siku ile,pale Ikulu,kwenye kile kiti chake kitukufu kinachohamahama, aliposaini kwa mbwembwe Sheria iliyochakachuliwa na Waziri bila ya Idhini ya Bunge(kwa ugunduzi wa Dr.Slaa)ya Gharama za Uchaguzi? Rais Kikwete hana jipya wala hatakuwa na jipya ....usanii mtupu.Anaweza kuwatamka Mawaziri au Manaibu ambao hata yeye hakuwaandika!! Subirini muone.

    ReplyDelete
  2. Hakuna jipya hapa, tutazamie mafisadi wapyaaa!

    ReplyDelete
  3. Hivi udini wewe kama mwandishi uliushuhudia katika chama gani? TBC & Star Tv walirusha matangazo ya mikutano ya kampeni.Vyama Vikubwa vyote vina viongozi na wabunge wakristo na waislamu...kama CHADEMA au CUF ilinadi wagombea wa dini fulani kwa nini wagombea wao dini nyingine hawakulalamika na kuhama chama.Kama Askofu Kakobe kumnadi Slaa ni udini,je alipomnadi Mrema 2000 ilikuwa nini? Sheikh Yahya amekuwa akimpigia debe Kikwete na hata kudiriki kuwatisha wagombea wengine kifo. Je JK naye mdini? Mbona hakumkana Sheikh Yahya? Mkurugenzi, Meneja na wapambe wengi wa Kikwete kwenye kampeni ni dini gani? Mkewe ni dini gani? Wanae? Kwani lazima kwenye familia muwe dini moja? JK umepata urais ulioutaka, acha kutuletea tatizo jipya!

    ReplyDelete
  4. Tatizo la viongozi wa Africa, ni urasimu kwani kila Raisi anaipita kwenye uchaguzi wowote awe amepita kwa haki au kwa ubadirifu wa kuuiba kura ni kwamba anapoingia madarakani kwa wale waliomsaidia kwa kampeni kwa pesa na kwa jinsi yoyote nae kama reward anataka awape uwaziri au unaibu waziri na hapo ndipo tunaongelea urafiki ila sio kumpa mtu kwa sifa zake na utendaji wake, swala la pili ni swala la urafiki kama tulivoona kwa awamu iliyopita kama waziri mkuu alio pita alichaguliwa kirafiki rakini angalia alivo muaibisha niswala ambalo yeye Raisi hawezi kuliongelea hadharani ila ni swala ambalo liko wazi kila mmoja hata ambae hahitaji elimu hata ya secondary analijua na kuliona wazi kuwa alichangua baadhi ya mawaziri kirafiki na ambapo inasemekana x-waziri aliejiudhuru alimsaidia mheshimiwa kwenye chaguzi zilizo pita za mwaka 2005, ila nafikiri this time tutegemee mabadiriko yalio mazuri kama ni makosa ameisha jifunza, Swala jingine ni swala la kuchagua mawaziri kama wenzangu walivo jaribu kuchanganua tatizo sana kwa nchi za africa tulilo nalo la kuchagua mawaziri na ma naibu waziri kwenye nafasi wasizo na frofesional zano ndiomaana watu wanashindwa kufanya kazi kwamaana wale walioko chini yako wanachukulia advantage ya weekness uliyo nayo kukuburuza na kufanya wanachotaka, ila mfano mzuri na waziri wa afya huo ndio mfano mzuri wa kumpa mtu kitengo alicho somea na anauwezo wa kukimudu kwani hakuna mtu wa chini yake kumdanganya kwani ni taaruma aliyoisomea. Mfano mbaya ni kama Dr. Husein Mwinyi kumuweka kua sijui waziri wa ulinzi? Medical Doctor na Mambo ya ulinzi wapi na wapi kama sio kupeana madaraka na kukuza CV ambazo haziendani hata kidogo, ndiomaa Africa maendeleo yatachelewa sana kuja. Asante

    ReplyDelete
  5. Huo udini wanao CCM Tizama Rais/Makamu/Rais wa Zenj/ Makamu wake wa 1 na wa 2 na safu zinazo wafuata.

    ReplyDelete
  6. Tuangalie kwa makini sifa na elimu uteuzi unapofanyika na kuangalia nyongeza ya sifa kwa kuchambua uzoefu an uadilifu wa anayeteuliwa.

    Hili kuwapo na utendaji wenye ufanisi i vema waziri na naibu wake wawe na taaluma ya wizara au mmoja wao kati ya hao wateule awe na taaluma ya wizara husika.

    Pia tunasahau swala la makatibu wakuu wengi hawana taaluma ya wizara wanazofanya kazi kitu ambacho kiutendaji kinakuwa hakina ufanisi kwani wakurugenzi katika wizara husika wana-take advantage ya kumburuza katibu na waziri/naibu wake.Hapa nashauri Mh.Rais pia wakati wa uteuzi wa makatibu azingatie taaluma.Mfano katibu mkuu wa wizara ya ujenzi ni mtaalamu wa madini kwanini asiende wizara hiyo na ujenzi akapewa mwenye taaluma ya uinjinia?Huu ni mfano tu kuna wizara pia zenye hali kama hii.
    Kwa kweli nasisitiza ushauri wangu TAALUMA,UZOEFU,UADILIFU VIWE VIGEZO.

    ReplyDelete
  7. Inawauma sana kuona safu yote ya uongozi zanzibar kuwa ni waislamu sasa wewe ukitaka iwe vipi? Mambo ya udini yako huko kwenu Tanganyika na si Zanzibar.
    Mambo ya zanzibar musiyajadili hayawahusu.

    ReplyDelete
  8. TUANGALIE WATEULE MBALI NA UZOEFU WAO ,ELIMU NA UADILIFU WAWE WABUNIFU WA MAENDELEO.MFANO HAPA UINGEREZA WATENDAJI WANAPOINGIA MADARAKANI WANAONYESHA MABADILIKO BILA KUJALI LAWAMA.MFANO SWALA LA UKUSANYAJI KODI LAZIMA WAZIRI WA FEDHA AWE MBUNIFU WA VIANZIO VIPYA VYA KODI ILI KUPATA FEDHA YA KUTEKELEZA SERA.
    KUNA VANZIO VINGI HAVIJAFIKILIWA NA WIZAR YA FEDHA-TRA KAMA KODI YA KUMILIKI TV(TV LICENCE)NA PIA MIFANO KATIKA WIZARA NYINGINE NISHATI(TANESCO)KUWEKA UTARATIBU MPYA HUSIOVUJISHA MAPATO NA WIZI WA UMEME.HAPA KUTUMIA KADI KULIPIA UMEME KUPITIA KWA MAJENTI WATAKAO TEULIWA SWALA LA UKILITIMBA LA KULIPIA OFISI ZA TANESCO NI WIZI MTUPU LIACHWE.TANESCO WAJE KUSOMA SYSTEM YA MALIPO YA UMEME/GAS KWA TECHNOLOJIA YA ELECTRONIC PAYMENT SYSTEM OR DIRECT DEBIT KUPITIA BANK KWA MAKAMPUNI MAKUBWA.HAPA SWALA LA KUSOMA MITA LIFE NI WIZI MTUPU.

    WIZARA TAWALA ZA MIKOA-TAMISEMI AWE MTU MWENYE KUWA MBUNIFU WA KUTOA MAELEKEZO NA VITENDO KUHUSU VYANZO VIPYA VYA UKUSANYAJI KODI.MFANO HAPA UINGEREZA COUNCIL ZIMEBUNI VIANZIO VINGI.MFANO KODI YA VIBAO VYA MATANGAZO YA BIASHARA HAISIMAMIWI KIKAMILIFU VIBAO VIMEZAGAA BILA KULIPIWA USHURU,PARKING YA MAGARI KUNA MAPATO YANAPOTEA UBUNIFU UFANYIKE N.K

    TUNATEGEMEA WATU WA NAMNA HII SI TU MTU AWE MKALI OFISINI LA MSINGI AWE MBUNIFU KWA VITENDO.

    ReplyDelete
  9. Orodha ya Baraza la Mawaziri na Manaibu wa Wizara za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2010 - 2015


    Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora - Mathias Chikawe
    Waziri wa Nchi, Mahusiano na Uratibu - Steven Wassira
    Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma - Hawa Ghasia
    Ofisi ya Makamu wa Rais Waziri anayeshughulikia Muungano - Samia Suluhu Hassan
    Waziri wa Nchi Mazingira - Dk. Therezia Luoga-Kovisa
    Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi wa Sera Uratibu na Bunge - William Lukuvi
    Waziri wa Nchi, Uwekezaji na Uwezeshaji - Maria Nagu
    Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - George Mkuchika
    Naibu Waziri Tawala za Mikoa - Aggrey Mwanri
    Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Masuala ya Elimu - Kassim Majaliwa
    Waziri Wizara ya Fedha - Mustapha Mkullo
    Naibu Waziri Wizara ya Fedha (i) - Gregory Theu
    Naibu Waziri Wizara ya Fedha (ii) - Pereira Silima
    Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi - Shamsi Vuai Nahodha
    Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nch- Balozi Khamis Sued Kagasheki
    Waziri wa Katiba na Sheria - Selina Kombani
    Waziri Wizara ya Mambo ya Nje - Bernard Membe
    Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje - Mahadhi Juma Mahadhi
    Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa - Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi
    Waziri Wizara yaMaendeleo ya Mifungo - Dk. Mathayo David Mathayo
    Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Mifungo - Benedict Ole Nangoro
    Waziri Wizara ya Mawasiliano Sayansi ya Teknolojia - Profesa Makame Mnyaa M'barawa
    Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano Sayansi ya Teknolojia - Charles Kitwanga (almaaruf Mawe Matatu)
    Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi - Profesa Anna Kajumulo-Tibaijuka
    Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi - Goodluck Ole Medeye
    Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii - Ezekiel Maige
    Waziri Wizara ya Nishati na Madini - William Mghanga Ngeleja
    Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini - Adam Kighoma Ali Malima
    Waziri Wizara ya wa Ujenzi (Barabara na Viwanja vya Ndege) - John Pombe Magufuli
    Naibu Waziri Waziri Wizara ya wa Ujenzi - Dk. Harrison Mwakyembe
    Waziri Wizara ya Uchukuzi - (Reli, Bandari, Usafiri wa Majini) - Omary Nundu
    Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi - Athuman Mfutakamba
    Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara -Dk. Cyril Chami

    Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara - Lazaro Nyalandu
    Waziri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi - Dk. Shukuru Kawambwa
    Naibu Waziri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi - Philipo Mulugo
    Waziri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii - Dk. Haji Hussein Mpanda
    Naibu Waziri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii - Dk. Lucy Nkya

    Waziri Wizara ya Kazi na Ajira - Gaudensia Kabaka
    Naibu Waziri Wizara ya Kazi na Ajira - Dk. Makongoro Mahanga
    Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto - Sophia Simba
    Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto - Ummy Ali Mwalimu
    Waziri Wizara ya Elimu, Habari, Vijana na Michezo - Emmanuel John Nchimbi
    Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Habari, Vijana na Michezo - Dk. Phenela Mukangala
    Waziri Wizara ya Ushirikiano Afrika Mashariki - Samuel John Sitta
    Naibu Waziri Wizara ya Ushirikiano Afrika Mashariki - Abdallah Juma Abdallah
    Waziri Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika - Profesa Jumanne Maghembe
    Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika - Christopher Chizza
    Waziri Wizara ya Maji - Profesa Mark James Mwandosya
    Naibu Waziri Wizara ya Maji - Gerson Lwenge

    ReplyDelete