24 November 2010

KKKT yamtetea Askofu Malasusa.

Na Edmund Mihale.

KANISA la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (KKKT-DMP) limesema kuwa tuhuma zinazotolewa katika vyombo vya habari dhidi ya dayosisi hiyo ni uzushi na chuki dhidi ya
viongozi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Msaidizi wa Askofu KKKT-DMP, Mchungaji George Fupe alisema shabaha ya habari hizo ni kulivuruga kanisa la Mungu katika jitihada zake za kueneza injili ya Kristo.

"Katika kikao chetu kawaida cha Halmashauri Kuu ya KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani kilichoketi Novemba 8 mwaka huu pamoja mambo mengine kilijadili na kuzingatia hoja zenye tuhuma ambazo zimesababisha kujenga dhana na hisia za kukosekana kwa maadili katika utendaji kazi wa viongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani," alisema Mchungaji Fupe.

Alisema kuwa katika kikao hicho walibaini kuwa madhumuni ya tuhuma hizo yalikuwa ni kuvuruga na kuchafua maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 30 wa Dayosisi hiyo utakaofanyika mapema Desemba mwaka huu.

Aliongeza kuwa malengo mengine ya makala hizo ni kudhoofisha uhusiano mzuri ulipo kati ya uongozi wa dayosisi hiyo na uongozi wa kisiasa na kiserikali, kudhalilisha uongozi  wa juu wa sasa wa dayosisi na kuondoa imani ya washirika, wachungaji, watumishi wengine na jamii kwa uongozi ulipo.

Alisema madhumuni mengine ni kuondoa imani kwa wafadhili na wenye mapenzi mema na dayosisi hiyo wanaochangia shughuli mbalimbali za kanisa na za kijamii zinazosimamiwa na KKKT-DMP.

Mchungaji huyo alisema kuwa makala hizo zinalenga kumdhalilisha Askofu Dkt. Alex Malasusa yeye binafsi na familia yake, hivyo kupunguza hadhi yake kama askofu na kuathiri heshima anayopewa na jamii ya wakristo nchini na mje ya nchi kwa ujumla.

"Hivyo Halmashauri Kuu ya KKKT-DMP inapenda kutoa rasmi kauli kuhusu hoja hizi zenye kila uzushi na chuki dhidi ya uongozi wa DMP na shabaha ovu ya kutaka kulichafua na kulivuruga Kanisa la Mungu katika jitihada zake za kueneza Injili ya Yesu Kristo," alisema Mchungaji Fupe.

Alisema halmashuri hiyo ina imani na Askofu Dkt. Malasusa na uongozi wake wenye uadilifu mkubwa kwa kanisa kwa jamii na serikali, inaamuamini, inaridhika kuwa bado ana sifa za uaskofu kama zilivyotajwa katika waraka wa Mtume Paulo kwa Timotheo (1 Tim 3:1-7).

Alisema kuwa Dkt. Malasusa ametumia vema na kwa uaminifu wito wake wa uaskofu katika dayosisi hiyo kwa kipindi chote cha miaka sita.

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika makala mbalimbali kumshutumu kiongozi huyo kwa sababu tofauti zinazohusiana na uongozi wake.

4 comments:

  1. WANAOMSHUTUMU NA KUMCHAFULIA SIFA ASKOFU MALASUSA; NI WALE WANAOSALI KANISANI HUKU WAKIWA VUGUGU, MUNGU WANAMTAKA, NA MAOVU WANAYATAKA; TENA WANAO FANYA HIVYO NI WALE WANAOHUSIANA NA VIONGOZI WANAOHITAJI CHEO HICHO, AMBAO HAWANA SIFA WAKIWATUMIA WAUMINI NA WASHARIKA NJE YA KANISA VIKIWEMO VYOMBO VYA HABARI, AMBAO HAWAJUI TABIA ZAO; NA KWA KUWA VYOMBO VYA HABARI PAMOJA NA KUHABARISHA, LAKINI VINAHITAJI CHOCHOTE HIVYO KUANIKA WANACHOSIKIA, WANACHOONA BILA KUWA NA UHAKIKA.
    MALASUSA AMEFANYA MENGI MAZURI, IKIWA I PAMOJA NA KUPATANISHA MIGOGORO MINGI UKIWEMO WA MOROGORO, DODOMA JUZI, NA MINGINE AMBAPO VIONGOZI WANATAKA WATUMIE KANISA KUJINUFAISHA, IKIWA NI PAMOJA NA KUFANYA BIASHARA AU MIRADI KWA MGONGO WA KANISA, WAPATA UNAFUU WA KODI KUMBE SI ZA KANISA BALI NI ZAO. KWA KUWA MWANYA HUO KWA MALASUSA WAMEUKOSA, NA KUZUIWA, WAMEANZA KUMFANYIA NJAMA NA MTIMA NYONGO.

    ReplyDelete
  2. Mungu amesema tusiwaguse Wapakwa Mafuta wake. ole wao wanaoingia katika vitendo viovu vya kumchafua Mtumishi wake. Wanatakiwa waombe rehema kabla ya fimbo ya Mungu haijawagusa

    ReplyDelete
  3. Kwa kweli tukifika mahali hapa pa kutumia vyombo vya habari katika kuwapaka matope viongozi wetu wa kanisa tutakuwa tunamkosea sana Mungu wetu. Ni matendo yetu maovu ambayo yanatufikisha mahali hapa tukaona kuwa Mungu wetu hayaoni haya tunayo yafanya. Kwa kweli tukiwaheshimu viongozi wetu ndiyo kumheshimu pia Mungu.

    ReplyDelete
  4. Uhuru ukizidi bila ya mipaka matokeo yake ni kutumia vyombo vilivyokusudidwa kutenda kazi kwa nia njema kutenda uhalifu au kueneza matumizi mabaya ya ulimi.Hatuwashangai watumishi wa mshahara iwasemayo Biblia, hata kanisani wamo waliofuata ajira na kugombea ukuu.Kama kipindi cha uchaguzi wa kisiasa kilichopita kwa mizengwe tusiiruhusu hali hiyo kanisani, Busara na hekima ya Mungu itumike kubaini wanaokuja kanisani kwa nia za usanii. Baba Askofu turudi katika magoti tujitakase na kulitakasa kanisa yeye atayapepeta magugu katika mavuno ya ngano. aliyaruhusu kukua na ngano. Mungu atalisimamia Kanisa lake

    ReplyDelete