Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Ufundi ya Klabu ya Simba, inatarajia kukutana leo jioni kujadili ripoti ya benchi la ufundi iliyoachwa na Kocha Mkuu, Patrick Phiri.Akizungumza
Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala alisema tayari wameshapokea ripoti ya benchi la ufundi na leo, kamati husika wanaijadili.
Alisema katika ripoti hiyo, mambo mbalimbali yamewasilishwa ikiwa ni pamoja na suala zima la usajili na mapendekezo wachezaji watakaosajiliwa na watakoachwa na baada ya hapo kila kitu kitawekwa wazi.
"Ni kweli benchi la ufundi limeshawasilisha mapendekezo yake, kujua nani ataachwa nani ataongezwa itajulikana tu na si hayo, bali hata tarehe ya kuanza mazoezi pia itapangwa siku hiyo," alisema Mtawala.
Simba katika mzunguko wa kwanza imemaliza ikiwa kileleni, baada ya kufikisha pointi 27, ikiwa imeshinda michezo tisa na sare na imefungwa mbili.
Mbali na hilo, wanachama na mashabiki mbalimbali wa timu hiyo licha ya kuwepo kwa hali ya mvua jijini Dar es Salaam jana, walikusanyika Makao Makuu ya klabu hiyo, mtaa wa Msimbazi wakizungumzia hatma ya Mwenyekiti wao, Ismail Rage baada ya kula kiapo cha Ubunge.
"Sijui Rage sasa ataachana na Simba, mimi naona bora aendelee kuwa Mwenyekiti na pia Mbunge, kwani yeye hana shughuli kubwa sana, shughuli zake zitafanywa na Makamu wake," alisema mmoja wa wanachama ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
No comments:
Post a Comment