LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti amekana taarifa zinazodai kuwa bado anatafakari hatima yake, katika klabu hiyo ya Stamford Bridge.Kauli hiyo ya Ancelotti, imekuja baada ya mabingwa hao wa
watetezi wa Ligi Kuu ya England na Kombe la FA, kulazimika kukanusha taarifa za kwamba Muitaliano huyo alijiuzulu Jumapili usiku, hali iliyozua wasiwasi ndani ya Chelsea.
Imekuwa ikiripotiwa kuwa Ancelotti, ambaye alisaini mkataba hadi majira ya joto ya mwaka 2012, alifadhaika baada ya kukiri kuchoka baada ya mechi ya Jumamosi, ambayo timu yake ilifungwa na Birmingham ikiwa ni kipigo cha tatu kati ya mechi nne, jambo lililodaiwa kuwa hana uwezo.
Hivi karibuni mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich aliamua kumtimua kazi ghafla kocha msaidizi wa Ancelotti, Ray Wilkins na kumpandisha daraja Kocha Mkuu wa vijana Michael Emenalo.
Ilielezwa kuwa kuondoka kwa Wilkins kumemwacha, Ancelotti njia panda na ni kwamba ameshawasiliana na Chama cha Makocha wa Ligi Kuu (LMA) kuhusu kazi yake Chelsea, lakini kocha huyo wa zamani wa AC Milan alisema ukweli ni kwamba LMA ndiyo iliyowasiliana naye.
Kocha huyo aliuambia mkutano wa waandishi wa habari juzi, wakati akizungumzia mechi ya jana ya Klabu Bingwa Ulaya, ambayo iliikutanisha Chelsea na MSK Zilina.
"Sidhani kama inatosha kuanza kuchambua kazi yangu kwa sasa na kuanzisha tetesi na uvumi kama huu.
"Tetesi hizi kwa ujumla si sahihi. Sifahamu ni kwanini zimejitokeza. Sijawahi kuzungumza na LMA.
"Walinipigia simu wao wenyewe wakati nikiwa nyumbani usiku, ili kufahamu kilichojitokeza.
"Tetesi hizi si za kweli, kwani nina mkataba hadi mwaka 2012 ndani ya klabu hii na nimeshasema mara nyingi kwamba ningependa kubaki hapa," aliongeza kabla ya kusema kuwa si kwamba anaipenda klabu hiyo pekee, bali na wachezaji.
No comments:
Post a Comment