19 November 2010

Tatizo la maji Mwananyamala lapata dawa.

Na Athman Hamza

TATIZO la upungufu wa maji katika Hospitali ya Mwananyamala litabaki kuwa historia baada ya Manispaa ya Kinondoni inayoimiliki kuchukua hatua kuepukana nalo.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Rafael Ndunguru alimweleza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Rugimbana kuwa manispaa imeongeza uwezo wa hospitali hiyo kutunza maji ambapo wameongeza matanki matatu yenye ujazo wa lita 10,000 kila moja.

Pia manispaa hiyo imeipatia hospitali hiyo gari maalumu la kubeba na kuhifadhi maji (Boza) lenye ujazo wa lita 8,000 na imechimba kisima na kutakasa maji hayo kwa dawa maalumu ili yawe safi kwa ajili ya matumizi salama.

"Usimikaji wa matanki haya matatu utakamilika kesho (leo) na hivyo kuipa hospitali uwezo wa kutunza maji mpaka kufikia lita zaidi ya 60,000, nia yetu ni kuwa na maji ya uhakika na uwezo wa kuhifadhi maji pindi maji ya DAWASCO yanapokosekana," alieleza Bw. Ndunguru.

Alisema manispaa hiyo imezungumza na DAWASCO ili kuunganisha bomba moja kwa moja kwenda hospitali bila kuwa tegemezi kwa kuchangia na wananchi wanaozunguka maeneo ya hospitali kama ilivyo sasa ambapo wananchi wengi wanachangia njia moja na hospitali, hali ambayo husababisha hospitali kupata maji kidogo kutokana na mgao.

Hospitali hiyo awali ilikuwa na tanki moja la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 30,000 ilhali uwezo wa DAWASCO kuhudumia hospitali hiyo ni lita 10,000 kwa siku kutokana na uhaba wa maji na mgao unaoendelea jijini Dar es salaam, hali ambayo imekuwa ikisababisha upungufu wa maji hospitalini hapo.

Bw. Rugimbana alisema serikali imeridhika na hatua iliyochukuliwa na manispaa na kuomba waendelee kushirikiana na DWASCO Kinondoni ili kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha.

1 comment:

  1. WIZI MTUPU....SUBIRI MIEZI MIWILI IPITE.... MIMI NI MFANYAKAZI WA MANISPAA HII NAWAELEWA SANA HAWA JAMAA WA IDARA YA MAJI....NA AFYA....WATAMWINGIZA MJINI HUYU NDUGURU ASIYEPENDA KUSIKILIZA WAFANYAKAZI WAKE..USIPOAMINI HILI KOPI MAWAZO YANGU HARAFU SUBIRI MIEZI MIWILI IPITE...

    ReplyDelete