Na Grace Michael
UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya wizi wa mamilioni ya fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA), umeshindwa kufunga ushahidi wake kutokana na jopo la mahakimu
wanaosikiliza kesi hiyo kutotimia.
Kesi hiyo inayowakabili washitakiwa watano akiwemo Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Rajab Maranda ililazimika kuahirishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mmoja wa jopo hilo, Bw. John Utamwa.
Upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Bw. Fredrick Manyanda uliieleza mahakama hiyo kuwa, ulikuwa na nia ya kufunga ushahidi wake lakini kutokana na kutotimia kwa jopo, hawawezi kufanya hivyo.
Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi watano wa upande wa mashtaka walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wao kuhusiana na makosa yanayowakabili washtakiwa hao.
Washtakiwa wengine ni Bw. Farijala Hussein, Ester Komu, Bosco Kimera na Imani Mwakosya ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo, kughushi na kuiba jumla ya sh. milioni 207 kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
Nyaraka za kughushi ni pamoja na hati za makubaliano ya kuhamishiwa deni kutoka Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashas (T) ya nchini Tanzania ambazo walizutumia na kuiba fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa mpaka Novemba 30 mwaka huu ambapo itatajwa na kupangiwa siku ya kuendelea kusikilizwa. Mahakimu wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Jopo hilo Bw. Ignas Kitusi na Bi. Eva Nkya.
No comments:
Post a Comment