Na Amina Athumani
TIMU ya Taifa ya mchezo wa pool, imeshika nafasi ya 10 kati ya nchi 12, zilizoshiriki mashindano ya Dunia ya mchezo huo, yaliyomalizika Novemba 13, mwaka huu nchini Ufaransa.
Mashindano hayo ambayo ni mara ya kwanza kwa Tanzania awali yalipangwa kuwa na nchi 32, lakini kutokana na nchi nyingi kukumbwa na ukata nchi 12 pekee ndiyo zilizokwenda kushiriki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Pool Tanzania (TAPA), Amos Kafwinga alisema licha ya kushika nafasi hiyo, lakini wameweza kujifunza mambo mengi ya mchezo huo kwani hata hivyo wachezai wake watoa changamoto kwa timu shiriki.
"Kwa sasa Tanzania ni ya 12 kwa ubora wa kimataifa katika mchezo huu, kwa kweli ingawa hatukufanya vizuri katika mashindano haya ya Dunia, lakini tumeweza kuitangaza nchi yetu kupitia Mlima wa Kilimanjaro na wachezaji wengi kutoka nchi mbalimbali wapata hamasa kubwa ya kutaka kutembelea mlima huo na mbuga za wanyama," alisema Kafwinga.
Alisema pia kwa kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, Omari Akida alishika nafasi ya 25 kwa ubora wa kimataifa na kwa rekodi ya wachezaji, inaonesha Tanzania bado inafanya vizuri.
Nchi zilizoshiriki michuano hiyo ya Dunia ni wenyeji Ufaransa, Tanzania, Ireland Kusini, Ireland Kaskazini, Hispania, Afrika Kusini, Uingereza, Wales, Gibralta, Scotland, Libya na Morocco.
No comments:
Post a Comment