LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti anatarajia kuwatumia chipukizi wake wakati timu hiyo itakapokuwa ikiumana na Zilina katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, itakayofanyika
baadaye leo usiku.
Blues tayari ilishajihakikishia nafasi katika hatua ya makundi, baada ya kujikusanyia pointi za kutosha katika mechi nne za kwanza kwenye kundi F.
Hali hiyo ndiyo inampa fursa kocha huyo kutoka Italia kuweza kupima safu yake baada ya Blues, kukumbwa na wakati mgumu katika michuano ya nyumbani.
Vipigo vitatu ilivyokutana navyo katika mechi tatu, vimeiruhusu timu hiyo kukabwa koo na Manchester United katika msimamo wa ligi, zikiwa na pointi sawa huku klabu hiyo ya Stamford Bridge ikiendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya magoli.
Katika mechi hiyo ya leo kiungo kinda, Josh McEachran ana uhakika atakuwemo katika kikosi cha kwanza na kocha Ancelotti, ana uhakika mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17 anajiandaa vyema kwa ajili ya mtanange huo na kinda huyo ambaye aling'ara katika mashindano hayo atahitaji kulazimisha njia kwa kocha wake kuweza kumtumia kwenye mechi ya nne ijayo ya Ligi Kuu, dhidi ya Newcastle.
Akisisitiza hali hiyo, Ancelotti alisema: "Josh lazima ataanza dhidi ya Zilina.
"Yupo tayari kwa sababu ana uwezo na atacheza nafasi muhimu uwanjani, akishikilia sehemu ya kiungo. Nafikiri ataweza kuonesha kiwango kizuri na yupo tayari kufanya hivyo," aliongeza kocha huyo.
"Samba na McEachran kuna wachezaji wengine chipukizi ambao nitawatumia dhidi ya Zilina. Kuna Kakuta, Van Aanholt, Bruma nataka kufanya mabadiliko ya kitu katika mchezo huu," alisema kabla yakuongeza kuwa jambo muhimu analolitaka ni kutoa fursa kwa vijana kuongeza uwezo wao na wanachokihitaji ni kuchukua pointi moja na uwezekano wa ushindi upo.
No comments:
Post a Comment