12 November 2010

Sitta kutupwa kwakera wengi.

Tumaini Makene na Gladness Mboma

WAKATI kamati maalumu ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tayari imempitisha kada wake Bi. Anne Makinda kuwa mgombea uspika katika uchaguzi utakaofanyika
leo bungeni Dodoma, uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kulikata jina la spika aliyemaliza muda wake, Bw. Samuel Sitta umezua mjadala mkali, huku baadhi wakisema tatizo si jinsia ya spika, bali fitna za kisiasa.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Majira juu ya uamuzi huo, ambapo CC ilipitisha majina ya wagombea watatu, Bi. Makinda, Bi. Anne Abdallah na Bi. Kate Kamba, waliofikishwa jana mbele ya kamati ya wabunge ambako Bi. Makinda aliibuka kidedea, wamesema kuwa uamuzi huo unaweza kuigharimu CCM mbele ya Watanzania.

Wakizungumza na Majira baadhi ya wananchi wametilia mashaka msimamo wa CCM wakisema uamuzi wa kupatikana majina hayo ulikuwa na msukumo wa kundi fulani ndani ya chama hicho ambalo halikutaka tangu awali spika huyo wa zamani apenye katika vikao kwenda katika kamati ya wabunge wa CCM, kwa kuwa asingeweza kulinda maslahi yao.

Wananchi hao walisema kuwa uamuzi huo wa CC, umetumia hila kulikata jina la Bw. Sitta kwa kisingizo cha usawa wa kijinsia, ili kuondoa malalamiko ambayo yangeweza kutokea, baada ya kuwepo tetesi za muda mrefu kuwa kulikuwa na mikakati ya kumwondoa Bw. Sitta. 

"Yusuf Makamba anasema wakati umefika kwa wanawake kuongoza bunge. Je, huko nyuma hawakujua wanawake wapo? Au wanataka kuwatumia wanawake kama Delila alivyotumiwa na Wafilisti kumnyoa nywele Samson? Tatizo sio spika mwanamke, tatizo ni je, anafaa? Je, nyuma yake hakuna mkono wa mafisadi?

"Kama uteuzi huu ni wa haki, sawa. Lakini kama kuna nguvu ya mafisadi hawatapona, bahari lazima ichafuke! Na ikichafuka lazima watu wazame. Wajiulize je, Mungu ameiona haki?" alisema mmoja wa wasomaji wa Majira aitwaye Catherine Malira mkazi wa Dar es Salaam.

Msomaji mwingine aliyetaka atambulishwe kwa jina moja la Priscus aliyedai ni mkazi wa Tanga alisema, "hayo ndiyo mambo ya CCM, mafisadi wana nguvu, ndiyo maana Sitta kaangushwa kwa kigezo cha usawa wa kijinsia, kwa hili maslahi ya taifa ni muhimu."

Mwanachi mwingine ambaye mbali ya kuwa mwanachama pia ni kiongozi ndani ya CCM, hivyo hakutaka jina lake litajwe kwa sasa, bali atafanya hivyo 'mambo yakiharibika zaidi', alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete anapaswa kukiri mbele ya Watanzania kuwa ameshindwa kuwadhibiti mafisadi kwa sababu kuondolewa kwa Bw. Sitta kunadhihirisha kuwa watu hao ndiyo wameshika hatamu ndani ya chama na serikali.

Mwanachama mwingine wa CCM ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema kitengo cha CC kumbwaga Sitta kitakigharimu chama hicho kwa sababu ndiye aliyekuwa akifukia mashimo ya dhambi ya chama.

Alidai CCM imepoteza mwelekeo na itikadi za chama, huku mafisadi wakiachwa wakigawana raslimali za nchi, huku Rais Kikwete akiangalia bila kuwakemea.

Aliongeza kuwa yeye na wenzake wako tayari kurudisha kadi za CCM kwa sababu hawaoni jitihada za kuondoa ufisadi nchini ambao alisema anaamini unarudisha nyuma maendeleo ya nchi na wananchi kwa jumla.

Kwa upande wake aliyekuwa kada wa CCM kabla ya kuhamia CHADEMA katikati ya mwaka huu, mbunge mteule wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda alisema kuwa wagombea watatu waliopitishwa na CC juzi na kupigiwa kura jana kumpata mmoja, walipitishwa kwa kisingizo kuwa Bw. Sitta na Bw. Andrew Chenge wangesababisha makundi.

"Hawa wanawake ni zao la mapandikizi ya CCM, wanaweza kuongoza na kufanya vizuri, lakini siyo matakwa ya Watanzania," alisema.

Mwananchi mmoja ambaye alijitambusha kwa jina la Samson Simbo alisema kuwa uongozi usitolewe kama 'sadakalawe' bali kwa vigezo vya utendaji wa mtu vinapaswa kuzingatiwa.

"Hatujasema kwamba wanawake hawawezi, lakini hawawezi kuwa na maamuzi kama ilivyokuwa kwa Sitta, watakuwa ni watu wa kupelekwa pelekwa na baadaye watashindwa kujibu hoja na hivyo uspika wao utaishia njiani," alisema.

Alisema CCM imeamua kuweka wanawake ili iweze kushika hatamu na kwamba hoja iliyotolewa na Bw. Makamba, kwamba wametoa fursa kwa mhimili wa chombo hicho kuongozwa na mwanamke kwa mara ya kwanza toka uhuru, si kweli bali wamefanya hivyo kwa maslahi yao.

Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Evangelical Church-PEC la Mjini Mbeya, Bw. William Mwamalanga alisema kuachwa kwa Bw. Sitta kuna ajenda ya siri ya kuhujumu uchumi wa nchi.

"Ukweli ni kwamba kumuengua Bw. Sitta kuomeongeza mashimo ndani ya CCM na kwamba waliopendekezwa kuwania kiti hicho cha uspika hawafai na ni wachochezi na wenye makundi ndani serikali," alisema.

Aliongeza kuwa CCM hakijamtendea haki Bw. Sitta kwa kumtosa, kwani ndiye aliyeipatia heshima Tanzania kwa kukuza demokrasia ndani ya bunge kitaifa na kimataifa.

"Kwa namna hii wananchi wameshaanza kulichukia bunge kabla hata halijaanza."

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Dkt. Paul Kyara alisema kuwa mchakato wa spika umetawaliwa na mvutano wa makundi ndani ya CCM yaliyotokana na mitandao ya kisiasa tangu uchaguzi wa mwaka 2005.

Alisema kuwa mchakato huo umeingia katika sura ya kujiimarisha kisiasa na maandalizi ya uchaguzi 2015, hivyo mtu yeyote anayefuatilia mpasuko wa kisiasa ndani ya CCM anaweza kung'amua haraka kuwa katika majina hayo yaliyowekwa ni nani analengwa.

"Huyu Bw. Sitta alikuwa awe ameondolewa siku nyingi, lakini ilishindikana, mwaka huu kundi hilo ambalo lilikuwa halimtaki limeamua sasa kummaliza," alisema.

Alisema kuwa kama wanawake hao hawatakuwa imara katika kutoa maamuzi itafikia mahali vibao vitatembea bungeni kwa sababu hakuna mtu atakayependa kuona hoja yake inaondolewa pasipo sababu za msingi.

Bw. Kyara alisema kuwa bunge la safari hii lilipaswa kusimamiwa na mtu shupavu kama Bw. Sitta, bila kuangalia maslahi ya chama, bali ya taifa.

8 comments:

  1. CCM wanajidai kwa kuwa huwa hawaadhibiwi kwa madhambi yao. Makinda ni kibaraka wa mafisadi tu wala si jinsia. Mheshimiwa Samuel Sitta atakumbukwa na historia imeandikwa. Kikwete afahamu kuwa wakati wa kuwachezea watanzania umekwisha.

    CCM ina mwisho.

    Kibaraka wao nae ana mwisho.

    Mheshimiwa Sitta adumu na mafisadi wafilie mbali. Vita uliypoigna mheshimiwa Sitta umeshinda, wewe ni shujaa, bali mafisadi ndi waoga. Aluta kontinua .....

    ReplyDelete
  2. Sita sio shujaa kama wachangiaji wengine wanavyoona, bali ni muoga na mnafiki. Yaliyo mkuta nimalipo halali ya tabia yake. Alijua mafisadi hawampendi bado akawalinda na kashifa zao.

    ReplyDelete
  3. Wakati wa kampeni Sita alisema CCM ina wenyewe yeye alidhani yumo kumbe hakujua kwamba yeye hayumo wenyewe ni wenye fedha wamemg'oa.

    ReplyDelete
  4. Tuyaonayo sasa ni dalili tosha ya kuwa Taifa letu ni corrupt, serikali inatiishwa na watu wenye pesa (MAFISADI)kama alivyosema Baba wa Taifa. Mafisadi ndio wenye maamuzi, Rais anakuwa kama rubber stamp. Wananchi, hii ndiyo CCM tuliyoichagua. Miaka mitano iliyopita uchumi wa nchi umekuwa hovyo, vitu vimepanda bei mara dufu, sasa tutarajie maisha magumu zaidi maana wenye nchi yao (MAFISADI)watachukua kila walichokuwa wamebakisha wananchi endeleeni kupata maisha shida bila kuwa na mtetezi. Bunge halitakuwa na msaada wowote maana wabunge asilimia kubwa ni kutoka chama cha mafisadi (CCM) hivyo watakaloamua wao ndilo litakalo tekelezwa. HONGERENI MAFISADI LAKINI KUMBUKENI UFISADI WENU NI HAPA DUNIANI TU KWA MUNGU HAKUNA UFISADI WAHURUMIENI MASIKINI. RASILIMALI ZA NCHI HII NI ZETU WOTE JAMANI MBONA MWALA PEKEYENU?

    ReplyDelete
  5. poleni watanzania?ni yale wanaosema walimwengu,mnyonge mnyongeni laki haki yake mpeni.ccm wameona ni bora kuwafuraisha mafisadi kuliko wananchi kweli?uwezi kuamini jinsia ndiyo imekuwa kigezo cha kumwazibu mtu mchapa kazi kama mh sita?tusije kusema maneno yale bora ya firauni.ccm watajutia maamuzi haya,unamaanisha makinda anajua kazi kuliko sita?wakati sia ndiyo boss wake?makinda umewekwa na hao mafisadi,lakini utajuta kuwekwa hapo kama utafuata maagizo yao.na kumbuka uakuwa chambo chao,ukishamaliza watakuchinjia barabarani kweupe kama wengine uliowaona mwanzo.
    swali langu huyu bwana piusi msekwa ,makamba wameadiwa nini na mafisadi hawa,mbona awaogopi hata kidogo? lakini angalizo langu kwa mwenyekiti wa ccm taifa,miaka mitani ni sawa na kufunga macho na kufungua,jiangalie sana hawa wakina makamba watakuvika shani ya the hue usipofungua vizuri macho yako kama mtanzania kaka.

    ReplyDelete
  6. JK ANAJULIKANA NI FISADI, RAIS NYANG'AU; NI HATARI KULIKO MCHUNGAJI WA MSHAHARA AMBAYE AKIMWONA SIMBA HUKIMBIA NA KUWAACHA KONDOO WAKIRARULIWA. KIPINDI HIKI WATZ TUJIANDAE JK ATATURARUA KWA MAKUCHA 10 KWA HASIRA YA KUTOMPA USHINDI WA KISHINDO. HATA HIVYO, HATUTISHIKI ANGUKO LAKE NA SWAHIBA ZAKE NA CCM LI KARIBU SAAANA. KABURI WALISHAJICHIMBIA WENYEWE.

    ReplyDelete
  7. kwa kumuacha sitta CCM imeonyesha dhahiri kuwa inamilikiwa na mafisadi wachache ambao ni kina Chenge na wenzake, ila wengi wanafata mkumbo na awajajitambua. Sitta ni kiongozi wa bunge aliyeongoza bila upendeleo na kuruhusu maovu ya mafisadi kufichuliwa kwenye bunge lake, tumewaona kina Lowassa, Karamagi na wengine wengi na walikuwa awafurahii uongozi maana waliunbuliwa kwneye bunge la Sitta ambaye hakutetea maslahi ya mafisadi bali ya umma wa watanzania wote. Ila kwa kuwa mafisadi awampendi Sitta, na CCM ni ya mafisadi ndio maana wameweka mtu ambaye atafanya kazi kwa maslahi yao. Mwisho wa CCM umekalibia watanzania wameamka!!!!!!

    ReplyDelete
  8. Watanzania mnalalamika nini?katika kampeini za Kikwete hakuna aliposema atapambana na ufisadi na slaa alieleza mipango mizuri ya chadema lakini mlishindwa kujitokeza kupiga kula kwa wingi hata kama wangechakachua ingekuwa ngumu sana, na hapa tungerudisha nchi mikononi mwa wananchi siyo kwa wachache.Tunajua fika kwamba kikwete hawezi kufanya kitu kwani watu wenye hela ndiyo waliomuweka walitegemea kukusanya hela zao kupitia Richmond na Sita akawaalibia sasa wanaona ni vizuri kumwondoa ili wafanye wanavyotaka.Ndugu watanzania Rostam ni mtu atari sana, Lowasa na gege lao hawa jamaa lazima watanzania tuwakatae,Wamefanya taasisi za serikali kulinda watu wachache Takururu ni ya Lowasa, kikwete, mkapa, chenge na wengine hawa wakikosea hakuna kuchunguzwa kabisa lakini mramba akikosea anakwenda mahakamani, je kuna sheria ya wachaga na wasukuma? DPP , Manumba na Oseah tunajua mnamlinda mzee wenu Chenge lakini sasa umefika wakati Chenge akamatwe huyu anatuhumiwa na rada, kama hahusiki basi chunguza hela zote alizoficha nje alizitoa wapi? na ziliingiaje nje ya nchi?
    Wiki tatu baada ya uchaguzi mmesahau na mmeanza tena.

    ReplyDelete