12 November 2010

Picha za CCTV zazua ubishi kesi ya Muro.

Na Rabia Bakari

PANDE mbili katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. mil.10 inayomkabili Mtangazaji wa kituo cha televisheni cha TBC1, Bw. Jerry Muro na wenzake wawili zimevutana kuhusu
ushahidi wa picha, uliotolewa mahakamani, ambao upande wa mashtaka ulitaka upokelewe kama kielelezo.

Hali hiyo ilitokea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wakati shahidi wa pili katika kesi hiyo, Bw. Aluru Kumar alipokuwa akitoa ushahidi wake.

Bw. Kumar alijitambulisha kama meneja wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano katika Hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, ambapo alidai kuwa anakumbuka Februari Mosi mwaka huu, akiwa kazini aliitwa na Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Bw. Calvin Stanley ambaye alimtambulisha kwa askari watatu waliokuwa wakitaka kuona matukio ya kuanzia Januari 29 mpaka siku hiyo kupitia kamera ya CCTV.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, alidai kuwa aliongozana na askari hao mpaka ofisini kwake, na kuwaonesha matukio hayo, ambapo ilifikia picha ya watu watatu ambao askari hao waliwatambua, na kuomba kuchapiwa picha hizo, na baada ya taratibu kukamilika, waliwapatia askari hao nakala ya picha hizo.

Bw. Kumar alizitambua picha hizo mahakamani na alipotakiwa kuzitoa kama kielelezo alikubali, lakini upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wa kujitegemea, Bw. Richard Rweyongeza ulikataa picha hizo kutolewa kama kielelezo bila kuwa na nakala halisi, ambapo waliiomba mahakama iamuru nakala halisi kutolewa.

Mvutano ulianzia hapo, ambapo upande wa mashtaka uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Boniface Stanlaus ulipojibu hoja hizo, kwa kuainisha vipengele vya sheria vinavyokubali ushahidi wa nakala kivuli, huku akiishawishi mahakama kukubali kupokea picha hizo, kama kielelezo.

Hakimu Mkuu Mkazi anayesikiliza kesi hiyo, Bw. Gabriel Mirumbe baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alitoa ahirisho fupi hadi leo, ambapo atatoa uamuzi wa mahakama kuhusu mvutano huo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Bw. Deogratius Mgasa na Bw. Edmund Kapama wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Bw. Richard Rweyongeza, Bw. Majura Magafu na Bw. Pascal Kamala.

Wakati shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, Staff Sajenti, Peter Jumamosi alipokuwa akitoa ushahidi wake, alionekana kujikanganya kuhusu maelezo ya mshtakiwa wa tatu Bw. Mgasa, ambaye maelezo yake ya onyo yanatofautiana na yaliyopo katika hati ya mashtaka.

Maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, yanadai kuwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyify, wakati maelezo ya hati ya mashtaka yanadai aliomba rushwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kuomba rushwa ya sh. milioni 10 na kujivika vyeo vya uongo.

2 comments:

  1. Nchi hii bwana ukisema kweli ni shida saana.kijana muro badala ya kupewa pongezi kwa kazi nzuri ya kupamabana na rushwa iliyokidhiri kwenye vyombo vya serikali wanataka wamchafue kwenye jamii.ni nani akuona kuhusu askari wale wala rushwa wakipokea rushwa?matokeo yake badala ya wale wala rushwa washughulikiwe kadiri ya sheria,wanakuja kubuni jinsi ya kumtesa kijana wetu aliyetoa taarifa sahihi na iliyoonekana duniani.
    swali langu ni ili je kweli serikali ya awamu ya nne ina nia dhabii ya kupambana na mdudu rushwa katika serikali?au ni janjwa ya nyani kula majani?

    ReplyDelete
  2. Ama kweli aliyenacho huongezewa na asiyenacho, hata kile kile kidogo hunyang'anywa! Kati ya Muro na Chenge, nani wa kuchunguzwa???

    ReplyDelete