12 November 2010

Makinda, Marando nani zaidi.

Na Tumaini Makene

NCHI bado iko kwenye msimu wa uchaguzi na uteuzi. Baada ya takribani juma moja na nusu kupita tangu uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, umeingia mpambano wa
kuwania uspika, unaohitimishwa leo bungeni kwa wagombea wawili, Mabere Marando (CHADEMA) na Anne Makinda (CCM).

Uchaguzi huo unaofanyika leo, unawakutanisha wanasiasa wazoefu katika siasa za nchi hii, ndani na nje ya bunge, ambao wote kwa namna moja ama nyingine, kwa nyakati tofauti wamewahi kuwa watumishi wa serikali.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka Dodoma, Bw. Marando ambaye ni mmoja wa waasisi wa siasa za mageuzi na mwanasheria maarufu nchini, alisema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa spika wa bunge la 10, Watanzania watarajie chombo hicho kufanya kazi kwa ufanisi, huku akiahidi kutoependelea upande wowote.

"Watanzania watarajie bunge lenye ufanisi, uongozi makini usiopendelea upande wowote, utakaosimamia umakini kwa mujibu wa katiba ya nchi, sheria na kanuni za bunge, eneo ambalo nina uzoefu nalo sana. Sina wasiwasi wa kupita eti kwa sababu mimi ni mgombea wa upinzani.

"Ninachoamini ni kuwa wabunge wanahitaji kiongozi wa bunge, bila kujali anatoka chama gani, kwa sababu hata kama unatoka upinzani huwezi kupendelea upande huo kwa sababu kanuni zinakufunga. Hata mbunge unapomruhusu kuzungumza, kisha ukamkatisha ni ukiukwaji wa kanuni labda mpaka uone anachokizungumza hakihusiani na hoja," alisema Bw. Marando.

Aliongeza kuwa atahakikisha bunge analoliongoza linakuwa
bora kuliko mabunge mengine yote yaliyokwisha kupita, akitumia uzoefu wake katika nyanja ya sheria, akisema unampatia nafasi ya uelewa wa katiba na sheria za nchi na kanuni za bunge.

Alisema iwapo atachaguliwa hatakwenda bungeni na agenda zake bungeni, kwa kutumia mamlaka ya spika, kwani ni kinyume na kanuni wala hawezi kupata nafasi hiyo kwani kawaida hoja au ajenda zinazojadiliwa bungeni hutoka ama upande wa serikali au kwa wabunge wenyewe, baada ya kuwa zimepitishwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge.

"Mimi kama spika siendi bungeni na agenda zangu, zitatoka kwa wabunge wenyewe, hata hivyo ukumbuke kuwa mbunge anayo haki ya kupinga agenda inayojadiliwa akiona kuwa haifai kuendelea kujadiliwa. Pia bungeni hoja hutoka upande wa serikali, mawaziri...kabla ya hapo kamati ya uongozi ambayo waziri mkuu ni mjumbe wake inakuwa imeshazipitia, huwezi kuingiza hoja zako.

"Wala chama changu hakiwezi kushinikiza kwa sababu hakina wabunge wengi wa kuweza kupitisha hoja bila bunge zima kuazimia, mwenzangu ndiye anaweza kulazimishwa ndiyo maana mimi nafaa zaidi. Sioni kwanini nitashindwa wakati nina sifa, na mtu mwenye sifa si ndiye anachaguliwa bwana au," alisema Bw. Marando. 

Kwa upande wake, Bi. Makinda akizungumza baada ya kutangazwa mshindi kupitia chama chama chake, aliahidi kulifanya bunge kuwa imara na la kisasa zaidi.

Pia aliongeza kuwa atahakikisha anaendesha bunge kwa kuzingatia kanuni na sheria na wabunge wote wanapaswa kuzijua kanuni hizo. Pia atandaa vipindi vya kuelimisha jamii, ili nayo ifahamu kanuni za bunge.

Wasifu

Anne Semamba Makinda


Mpaka hivi karibuni wakati bunge la 10 likiitishwa na Rais Jakaya Kikwete ndiye alikuwa naibu spika wa bunge lililopita.

Ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya bunge la Tanzania, bila shaka iwapo mambo yatamwendea vizuri leo na kupata kura nyingi ataweka historia nyingine ya kuwa mkuu wa kwanza mwanamke katika moja ya mihimili ya serikali nchini.

Ni mwanasiasa mzoefu akiwa amewahi kushika nafasi mbalimbali kama vile ukuu wa mkoa katika mikoa mbalimbali nchini. Amekuwepo katika serikali kwa muda mrefu.

Kwa sasa ni mbunge wa Njombe Kusini. Ukiachilia mbali madai ya baadhi ya wabunge kuwa ni huwa ni mkali, akiwakatisha mara kwa mara wabunge wanapokuwa wakichangia hoja, wengine wamekuwa wakimwona kama ni mwanamke jasiri anayeweza kusimamia shughuli za mhimili huo unaopaswa kuisimamia, kuihoji, kuishauri na kuiwajibisha serikali.

Mbali ya wengine kumwita 'dikteta' akionekana wakati mwingine kuiokoa serikali ya chama chake, CCM, isiaibike dhidi ya hoja za wabunge, hususan kutoka kambi ya upinzani, pia mchakato uliotumika kumpata umeibua gumzo, wengine wakisema amepitishwa kwa gharama ya kuondolewa Bw. Samuel Sitta, ili atumie nafasi hiyo kuisaidia serikali iliyoko madarakani kila inapobidi.


Mabere Nyaucho Marando

Ni wakakili maarufu nchini, akiwa amefanya kazi ya sheria kwa takribani miaka 30. Ni mmoja wa waasisi wa siasa za mageuzi nchini, yeye pamoja na wenzake wengi wakiwa wamehusika katika kuendesha harakati za vuguvugu za kudai mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini, wakipigania demokrasia ya vyama vingi.

Yeye na wenzake kadhaa walianzisha moja ya vyama vilivyokuwa na nguvu mwanzo wa siasa za mageuzi, NCCR- Mageuzi, ambacho hata hivyo baada ya kuitikisa CCM katika uchaguzi mkuu wa 1995, hakikuweza kudumu na nguvu yake mpaka kufikia katika uchaguzi wa mwaka 2000.

Ni shushushu mstaafu, akiwa ameitumikia nchi katika kazi hiyo miaka ya sabini, akiwa katika dawati la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, huku akishiriki kikamilifu pia katika Vita vya Kagera, kumng'oa Nduli Idd Amin.

Ambapo inasemekana kuwa wakati mapambano ya vita hiyo yakiwa makali, huku hali ya hatari ikinukia pande zote husika za vita, aliweza kuingia nchini Uganda na kulala katika Jiji la Kampala katika harakati za kukusanya taarifa muhimu zilizosaidia ushindi wa majeshi ya Tanzania.

Kutokana na kazi yake hiyo ya zamani mara nyingi amekuwa haaminiki sana anaposema kuwa amestaafu kama wafanyavyo kwenye kazi zingine, na wala habanwi kuwa mwanachama wa chama kingine cha siasa tofauti na CCM. Yeye amekuwa akidai kuwa moja ya sababu zilizomfanya astaafu mapema kazi hiyo ni kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama tawala, kinyume na matakwa yake.

Shahada ya kwanza ya sheria aliipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Rorya, mkoani Mara, tangu mwaka 1995-2000. Kisha akawa mmoja wa wabunge wa mwanzo wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki, kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Hivi karibuni alinukuliwa akisema aliamua kustaafu siasa, lakini aliamua kurudi baada ya kufurahishwa na uamuzi wa Dkt. Willibrod Slaa kugombea urais. Sasa ni mjumbe wa kuteuliwa wa Kamati Kuu ya CHADEMA.

Kuashiria kuwa bado ni msimu wa uchaguzi, uteuzi, kuthibitishwa na kuapishwa, baada ya uchaguzi wa spika leo, wabunge wataanza kuapishwa mpaka Jumanne asubuhi wiki ijayo, ambapo mchana watathibitisha jina la waziri mkuu atakayeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, pia watafanya uchaguzi wa naibu spika. 

2 comments:

  1. UPINZANI NI KAZI SANA TANZANIA KWA VILE CCM INAHONGA UPINZANI NA KUWARUBUNI KWA UONGOZI HIVYO WANASALITI UPINZANI, SASA ONA HIVI KWELI MTU ALIYEKUFA MWAKA 2005 KWENYE UJO ZA UCHAGUZI AKIFUFUKA LEO AKUTE MAALIM SELFU NI MAKAMU WA RAIS ZANZIBAR CHINI YA CCM SI ATAOMBA AFE TENA!!
    HIVYO CUF KAMWE HAWATA UNGANA NA CHADEMA KWA VILE WANAMUUNGANO NA CCM! SASA CHAMA KIMOJA HAKIWEZI KWA CHAMA CHA UPINZANI BUNGENI NA NI MSHIRIKA WA CHAMA TAWALA-HUU WOTE NI UFISADI NA NJAA YA MADARAKA.
    MTU MWINGINE AMBAYE NI CCM KIVULI MBUNGE WA VUNJO BWANA MREMA, YEYE WALA SIYO NDUMILA KUWILI BALI NI CCM DAMU.

    ReplyDelete
  2. IMEFIKA KWA CHADEMA NA CUF KUUNGANA KAMA MWALIMU NYERERE ALIVYOUNGANISHA TANU NA ASP ZANZIBAR ILI TUWEZE KUISHINDA CCM

    ReplyDelete