Na Amina Athumani
MVUA kubwa iliyoambatana na radi iliyonyesha jijini Dar es Salaam jana, imesababisha kusimama kwa mashindano ya muungano kuogelea, yaliyoanza
juzi katika bwawa la shule ya Kimataifa ya Hopac iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya klabu 10 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo hadi juzi klabu zilizojitupa majini zilikuwa zikilingana kwa pointi, hivyo kushindwa kutabir nani angeibuka bingwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Masellino Ngalimo alisema michuano hiyo wameisimamisha kutokana na radi ambayo isingekuwa rahisi kuwaruhusu wachezaji kuingia kuogelea, huku radi ikiwa inaendelea kupiga.
"Mvua pekee si tatizo isipokuwa radi ndiyo tatizo, kwani ingekuwa inanyesha mvua bila radi tungeendelea na mashindano kama kawida, hivyo tutasubiri hadi muda wa saa nane mchana (jana), kama radi itaacha tutaendelea kucheza na kama haitaacha basi tutaahirisha mashindano hayo na tutatangaza siku nyingine ya kuyafanya," alisema Masellino.
Klabu zinazoshiriki michuano hiyo ni Sringrays, UDSM, Dar swim, Talis, Hopac, KMKM, Arusha Swim, Isamilo Swim, JKT, Nyuki, Agakhan, Tanzania Marine na Navy.
Bingwa mtetezi wa michuano hiyo ni klabu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
No comments:
Post a Comment