16 November 2010

Sikutumia pesa kutafuta uspika- Makinda.

Na John Daniel, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Bi. Anne Makinda amesema hakutumia hata senti moja kutafuta nafasi hiyo wala kumpa mtu maji ya kunywa ili kumsaidia na hivyo kuahidi kuwa
hatashindwa kutumiza wajibu wake kwa kuwa hakuna mtu aliyemfikisha hapo alipo isipokuwa ni Mungu pekee.

Pia Spika huyo mpya amesema anawasangaa watu wanaeneza maneno yasiyokuwa na ukweli kwamba amewekwa katika nafsi hiyo na kundi fulani na kuweka wazi kuwa yeye ni mwadilifu na ataendelea kuwa mwaminifu na mwadilifu hadi kufa kwa kuwa hata Baba
yake mzazi alikuwa hivyo.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumponza iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) katika Uwanja wa Nyerere Square juzi, Spika Makinda alisema anayefikiri kuwa aliwekwa katika nafasi hiyo na watu fulani wanapoteza muda.

"Siku ya uchaguzi nilienda kanisani, nilikuwa namuuliza Mungu hivi kweli nitashinda, nikaomba nikapata matumaini, kupata uspika sikutumia hapa senti moja kumpa mtu wala
kutoa maji ya kunywa, Haleluya, nitafanya kazi hii vizuri maana hakuna
aliyeniweka,"alisema Bi. Makinda

Alisema hata akiulizwa mtu aliyemfanyia kampeni hawezi kusema kwa kuwa hakuwahi kumwomba mtu yeyote kumfanyia jambo hilo lakini kilichomshanga ni kwamba alifanyiwa kampeni na kila mtu bila yeye kujua.

Alisema hana wasiwasi na uadilifu wake kwa kuwa hiyo ni tabia yake ya asili na kwamba hata Baba yake mzazi alitumikia umma hadi alipofariki akiwa mwadilifu hivyo hakuna wa kumwamisha katika msingi huo.

Kuhusu Spika aliyemaliza muda wake Bw. Samuel Sitta, alisema hana matatizo yoyote na kiongozi huyo na kusisitiza kuwa iwapo Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi kingepitisha jina lake yeye angejiondoa katika kinyang'anyiro hicho.

"Hivi jamani mlitaka Spika na Naibu wake wote wasigombee nafasi hiyo kwani kulikuwa na tatizo gani!, nilishasema kuwa kama jina la bosi wangu (Sitta) likingerudi mimi ningejitoa lakini mimi ndiye niliteuliwa,"alisema Bi. Makinda.

Alisema anamfahamu Bw. Sitta tangu mwaka 1975 walipoanza kazi pamoja Ofisi ya Bunge hivyo hakuna anayeweza kumdanganya juu ya utendaji wake na kusisitiza kuwa kama kuna mazuri aliyofanya katika kipindi cha miaka mitano ya uspika na yeye ni sehemu ya mafanikio hayo.

Kwa upande wake mke wa Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake Bi. Tundu Pinda, alisema amekuwa akimwomba Mungu kwa kipendi kirefu ili apatikane spika mwanameke kuongoza Bunge na kuongeza kuwa hata cheo cha Uwaziri Mkuu katika awamu hii inatakiwa ishikwe na mwanamke.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Bw. Peter  Pinda aliwapongeza wajumbe wa CC na wabunge wa CCM kumpa ushindi Bi.Makinda na kumhakikishia ushirikiano katika utendaji wake.

7 comments:

  1. Watu wa Njombe mjini wanajua kwamba mzee Makinda hakuwa mwadilifu hata kidogo. Tafadhari sana Anne, usimsingizie mzee wawatu, mzimu wake utakukataa bure.

    ReplyDelete
  2. hahaha! nicheke mie! eeh? mzee makinda vipi huko njombe?

    ReplyDelete
  3. Makinda unajichanganya sana, eti unasema km jina la sitta lingerudishwa na cc ungejitoa? Huu ni usanii wa alinacha, sasa kwa nini hukuondoa jina lako baada ya kuona sitta amechukua fomu. Sitta alikuwa mtu wa kwanza kuchukua fomu.Si ungemwachia tu basi. Mama makinda unajua fika nini ulichokuwa unakifanya huu ni unafiki tu. Utasubirije mpaka jina la Sitta lirudi ndo ujitoe, manake unajua ndiye aliyekuwa kipenzi cha wabunge na wananchi na usingeweza kumshinda kama majina yenu nyote yangerudi.Wosia wangu endesha bunge kwa haki acha ubabe, ukoloni wako tunaoujua wape wapinzani nafasi ya kuikosoa serikali km alivyofanya sitta. Usiwe kibaraka wa ccm tu na mafisadi waliokusaidia kupata nafasi hiyo.

    ReplyDelete
  4. siyo siri nafasi hii mama makinda amepewa na mafisadi na sababu ni kuwa akikaa pale kazi yake itakuwa ni kuwalinda kama hamuamini kaeni mkao wa kula mtaona.

    ReplyDelete
  5. Nyie acheni unafiki yule mama uwezo anao na bunge ataliongoza kwa hekima kubwa aliyojaliwa na Mungu

    ReplyDelete
  6. labda hekima hio aliipta baada ya ibada yake kama anavyodai...alikesha akiomba ili ashinde, ila ukweli nauona kuwa Mama Makinda amekuja kwa sababu maalumu, muda utatuambia ukweli na wakati umefika

    ReplyDelete
  7. Kueni na ustaarabu jamani. Uchaguzi umeisha. Inabidi tuwape nafasi wote waliokula kiapo kufanya kazi zao. Makinda akifanikiwa itakuwa ni ushindi wa watanzania wote. Tunataka hawa watu wote, wabunge, spika, madiwani, mawaziri, etc, watimize wajibu wao katika kuwatoa watanzania katika umaskini uliokithiri. Hivi nyie mnaomtupia madongo Makinda sasa hivi mna maana gani? Akishindwa bungeni itakuwa ni kwa faida ya nani? Halafu wengi wa mnaotoa maoni katika kurasa online ni watu mlio nje ya nchi. Inabidi mje Tanzania muone reality siyo hayo mnayosoma magazetini ambayo nayo yako biased in one way or another. Of course huyu ni mama jasiri hatashindwa, mtakuja kushangaa atakavyofanya kazi. Kila aliyona utendaji wake akiwa naibu spika anajua ataweza. Nyie mlio nje hilo hamlijui, au mnaongea kishabiki tu. Kwani hata huyo Sitta baada ya kuchukuwa toka kwa Msekwa nani alijua atafanya kama alivyofanya? Halafu jamani CCM imaeamua kumbadirisha Sitta ndiyo demokrasia. Kwani yeye ni nani mpaka awe ni yeye tu?

    ReplyDelete