24 November 2010

Serikali kuwajengea albino kituo Arusha .

Na Peter Mwenda.

WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda ameahidi kujenga kituo kwa ajili ya kutoa elimu na matibabu wa ngozi watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) mkoani Arusha.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha pamoja na albino hao kilichoandaliwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Under the Sun ya Canada yenye tawi lake nchini, Bw. Pinda alisema ameomba ekari 50 mkoani Arusha na amekubaliwa ili kujenga kituo hicho.

"Nimewachukua vijana albino naishi nao nyumbani kwangu, kumbe hawa ni wazungu, wakiishi vizuri na kula wanapendeza sana, tutawajengea mahali Arusha ambako watapata huduma za matibabu na kusoma vizuri," alisema Bw. Pinda.

Alisema watu wanaopata saratani ya ngozi ni albino ambao wanalazimika kwenda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hivyo kukipatikana kituo cha albino kitasaidia kuwatibu.

Hata hivyo, albino hao walijikuja katika katika majozi na kuangusha kilio baada ya kuoneshwa filamu ikionesha wenzao waliouawa na kukatwa viungo kwa imani za kishirikina.

Katika tukio hilo filamu hiyo ilionesha mtoto mmoja albino aliyeshuhudia dada yake akichinjwa kwa panga na wauaji kutega damu yake na kuinywa akishudia.

Filamu hiyo pia ilionesha maeneo mbalimbali ambako albino waliuawa na wengine kunusurika kifo na kuongeza simanzi kwa wote waliokuwepo ukumbini na kujaa kelele za vilio.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi aliwaliwaza albino hao na kuwataka wajipe moyo kwa sababu ukatili huo una mwisho kwa vile Mungu hajashindwa kukomesha mauaji hayo.

Awali Waziri Mkuu alisema wanaoua albino wanapata dhambi kubwa, kwani kufanya hivyo ni jambo la kishetani si la kibinadamu.

Aliitaka taasisi ya Under the Sun kusambaza filamu hiyo mikoani ili wananchi waone ukatili unaofanywa kwa imani potofu ambako Mwenyekiti wa IPP ameahidi kusaidia kutekeleza agizo hilo.

Mwenyekiti wa taasisi ya Under the Sun, Bw. Peter Ash ambaye pia ni albino alitoa wito mauaji ya albino Tanzania yakomeshwe na kesi hizo kuharakishwa kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment