Na Pendo Mtibuche, Dodoma.
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kesho.Chuo hicho ambacho kilifunguliwa Septemba, 2007 kikitumia
jengo moja la Chimwaga, hivi sasa tayari majengo mbalimbali yameshajengwa kwa ajili ya kupokea wanafunzi, na baadhi yao wameshahitimu shahada mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof Idris Kikula alisema kuwa baada ya kukamilika kwa hatua zote za uzinduzi, waliamua kufikia hatua ya kutafuta muda mwafaka ambao rais angekuwa na nafasi ya kufanya uzinduzi huo.
Alisema kuwa rais atazindua jengo la utawala, ataweka jiwe la msingi la kituo cha uchunguzi wa afya, kuzindua mkongo wa mawasiliano na chuo cha sanaa na sayansi za jamii.
Akizungumzia hali ya miundombinu chuoni hapo, Prof. Kikula alisema kuwa wakati chuo hicho kinaanzishwa kilikiwa katika wakati mgumu hasa kwa majengo mbalimbali yakiwamo nyumba za walimu na wanafunzi, pia tatizo la usafiri.
Alisema wakati huo chuo kililazimika kutumia nyumba 155 zilizoko katika eneo la Kisasa kwa ajiri ya kuwapangisha wanafunzi, ambapo kwa nyumba moja walikuwa wanaishi wanafunzi 16 wakati lengo la nyumba hizo lilikuwa ni kuishi walimu wa chuo hicho.
Mara baada ya chuo hicho kupata fedha kutoka katika mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii, walijenga hosteli za wanafunzi na kupunguza tatizo la wanafunzi kurundikana katika nyumba hizo.
Wakati huo huo, keshokutwa chuo hicho kitafanya mahafali ya kwanza mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa.
Jumla ya wahitimu katika kozi mbalimbali wapatao 1,279 watatunukiwa shahada mbalimbali.
Alisema kuwa hadi sasa chuo hicho kimeshaajiri vijana 300, kati yao 150 wamepelekwa nje kujiendeleza zaidi ili chuo kupata na walimu wazuri.
Chuo hicho kimeajiri walimu kutoka nchi za India, Urusi, Nigeria na Sweden lengo likiwa ni kukiimarisha, kwa kuwa kwani chuo si mwonekano wa majengo bali ni ubora wa elimu.
Tayari chuo hicho kina wanafunzi 20,000, wafanyakazi 925 wakiwamo wanataaluma 525 na wafanyakazi waendeshaji 400. Malengo ya chuo hicho ni kuendelea kutafuta walimu wengi
zaidi ili kufikia malengo miaka 40 ijayo. Ifikapo mwaka 2015 chuo hicho kinakusudia kiwe na wanafunzi 40,000.
No comments:
Post a Comment