23 November 2010

Nguzo za umeme zachelewesha uwanja wa ndege.

Livinus Feruzi, Bukoba

SHIRIKA la umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Kagera limesema lipo tayari kuhamisha nguzo za umeme karibu na eneo la Uwanja wa Ndege mjini Bukoba baada ya kulipwa fidia ya
zaidi ya sh. milioni 7.5 na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini.

Meneja wa TANESCO mkoa wa Kagera, Bw. Charles Urio alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Majira juu ya sababu za kuchelewa kuhamisha nguzo hizo kama ilivyoshauriwa na mamlaka ya usalama wa anga kabla ya kuruhusu ndege kubwa kutumia uwanja huo.

Bw. Urio alisema kuwa uhamishaji wa nguzo hizo hauwezi kufanyika mpaka mamlaka ya viwanja ilipe fidia na gharama zinazotakiwa na kuwa baada ya kulipwa fidia hiyo TANESCO wataanza kuhamisha nguzo hizo.

Alisema kuwa nyaya za umeme karibu na eneo la kutua ndege karibu na uwanja huo, zinatakiwa kupitishwa ardhini kwa ajili ya usalama wa ndege wakati wa kutua na usalama wa abiria na wananchi kwa ujumla.

Bw. Urio alisema ndege hairuhusiwi kukaribia nyaya za umeme na kuongeza kuwa  kufanya hivyo kunaweza kusababisha ndege kulipuka na hatimaye kuleta madhara.

Kwa mujibu wa Meneja msimamizi wa kampuni ya ujenzi wa uwanja huo United Constraction Limited (UNICO), Bw. Sadik Bawa awali uwanja huo ungefunguliwa kwa ndege kubwa Oktoba Mosi mwaka huu.

Ukarabati na upanuzi wa uwanja huo ulioanza kutengenezwa Juni mwaka jana ulikamilika kwa upande wa wakandarasi kwa asilimia 99 tangu Oktoba Mosi mwaka huu, ambapo maboresho na marekebisho madogo madogo yanaendelea kufanyika katika sehemu za nje ya uwanja katika mitalo.

Bw. Bawa alisema hadi sasa kinachokwamisha uwanja huo kutumika kwa ndege kubwa ni nguzo za umeme ambazo zipo karibu na uwanja huo karibu na Shule ya Msingi Tumaini.

No comments:

Post a Comment