23 November 2010

Karume mgeni rasmi kumuenzi Nyerere Mzumbe.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro.

CHUO Kikuu cha Mzumbe kimeandaa siku maalumu ya kesho  kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kama sehemu ya kutambua mchango wake katika
ukombozi na maendeleo ya Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na chuo hicho kupitia kitengo chake cha Habari na Mahusiano kwa Umma jana, ilisema kaulimbiu ya siku hiyo ni Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu Uchaguzi wa Kidemokrasia.

Chuo hicho kimekuwa ni miongoni mwa taasisi zenye utamaduni wa kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere tangu mwa 2004. 

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kutokana na chuo kutambua mchango wake katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na hususani katika kuimarisha demokrasia hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa, wakati ya siku hiyo wanataaluma na wageni mbalimbali hukutana na kujadili masuala mbalimbali yanayoligusa taifa na kutafakari kuhusu mawazo ya Mwalimu Nyerere kuhusiana na masuala hayo.

“Maandalizi ya siku hiyo yamekamilika na ukizingatia kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati huu kutokana na ukweli kuwa Chuo Kikuu cha Mzumbe pamoja na vyuo vikuu vyote nchini mwaka wa masomo umechelewa kuanza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya Uchauzi Mkuu wa 2010,” taarifa hiyo imeongeza.

No comments:

Post a Comment