Na John Daniel, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemchagua Mbunge wa Kongwa, Bw. Job Ndugai, kugombea nafasi ya unaibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kumpa kura 197 kati ya 199 zilizopigwa na wabunge wa chama hicho mjini hapa jana.
Bw. Ndugai ambaye awali aliomba kugombea uspika akichuna na wana-CCM 13 akiwemo Spika Makinda, alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo mwishoni mwa wiki huku kukiwa na taarifa kuwa alishauriwa kufanya hivyo na vigogo wa chama hicho ili kuweka usawa wa kijinsia baada ya mfumo kumkubali Bi. Makinda kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya uwasa wa kijinsia na kutekeleza maazimio ya Beijing.
Katika uchaguzi huo wa CCM, jumla ya wabunge waliopiga kura walikuwa 199 huku kura moja tu ikimkataa na nyingine ikiharibika, hivyo kumpa ushindi wa asilimia 99 baada ya wagombea wawili waliokuwa wakichuana naye, mbunge wa Peramiho, Bi. Jenista Mhagama na Mbunge wa Magu, Dkt. Festus Limbu kujitoa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Bw. John Chiligati alisema kabla ya Bw. Ndugai kuibuka na ushindi huo wa kishindo, Bi. Mhagama alijitoa kwa maelezo kuwa anazingatia usawa wa kijinsia baada ya Spika Makinda kuchaguliwa, hivyo kuwaomba wabunge wasimpigie kura.
Alisema kabla ya Bi. Mhagama kutangaza na kuwaomba wabunge kutompigia kura, Dkt. Limbu alitangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho kwa maelezo kuwa hana sifa kama walizonazo wagombea wenzake, hivyo haoni sababu ya kuendelea kugombea badala
yake anaondoa jina lake.
Katika hatua nyingine, dalili ya mgawanyiko ndani ya Kambi ya Upinzani bungeni imezidi kudhihirika baada ya Chama Cha Wananchi (CUF) kushirikiana na TLP, NCCR-Magezui na UDP kumteaua Mbunge wa Mkanyageni, Mwandisi Mohamed Habib Mnyaa huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kikimteua Mbunge wa Mbulu, Bw. Mustapha Akoonay pia kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na Majira jana, Mkuu wa Kambi hiyo ya vyama vinne ambaye alikuwa Kiongozi wa upinzani katika Bunge lililopita, Bw. Hamad Rashid Mohamed alisema walifikia uamuzi huo baada ya juhudi zao za kutaka kukaa pamoja kushindikina.
"Kama nilivyokwisha kusema sisi CUF sera yetu ni kuungana na wapinzani wote bila kubagua mtu hadi pale atakapobainika kukiuka makubaliano yetu kama kambi, lakini wenzetu bado hawajahafiki hilo, basi tumefanya hivyo maana hatuna njia nyingine, hata
sisi hatupendi kufanya hivyo lakini sasa hatuna namna," alisema Bw. Mohamed.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge uchaguzi wa Naibu Spika utafanyika kesho (Jumanne). Leo saa 10 jioni ni siku ya mwisho kwa vyama vyote kuwasilisha majina ya wagombea wa nafasi ya Naibu Spika katika Ofisi ya Bunge.
I like this, CHADEMA simameni imara. CUF waliwakaribisha kwenye KUB kwa vile hawakuwa na sifa kamili ya kuunda kambi ya upinzani. Wao wanaka tu kushika uongozi tuu, sio kuleta mabadiliko. Ona visiwani walivyofanya. sasa ni nani wa kupinga mwenzake.
ReplyDeleteHaya marafiki zangu, hao ndiyo wapinzani mliotaka kuwapa nchi. Watu wanasema watanzania ni mbumbumbu wanaochagua ccm kila mara, au ccm inaiba kura. Hakuna watu wenye upeo wa kuelewa mambo kama watanzania. Haya yote wanayaona na wanajua chama kilicho makini baada ya kufanya utafiti. Angalia wabunge wa viti maalumu wa chadema, wangapi wanatoka wapi, na wanahusiana na nani utajua Chadema ni chama cha namna gani. Hiki chama hakikuwa tayari kuchukuwa dola kama wengine walivyokuwa wanafikiri. CCM haikuchakachua kura kama wengine walivyokuwa wanadhani. Hakukuwa na haja hiyo. Matukio haya ya bungeni ni mwanzo mbaya kuelekea safari ya 2015. Wananchi watakumbuka. Wamekaa kupiga kelele ya Sitta Sitta, CCM kwa kutumia demokrasia walimchagua Makinda, hatujui Marando ulitumika utaratibu gani kumpata. Hakuna aliyehodhi kiti chochote kama tunavyoona kwenye vyama vya upinzani. Wamejaa ubinafsi ndiyo maana kila mwaka unasikia viongozi wale wale. Kwa style hii CCM itaongoza milele.
ReplyDelete