22 November 2010

M'kiti CHADEMA Mbeya ajiuzulu.

*Akimbia tuhuma za kukihujumu chama kwenye uchaguzi.

Na Rashid Mkwinda, Mbeya.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, Bw. Sambwee Shitambala ametangaza kujiuzuru wadhifa huo ili kupisha uchunguzi dhidi
yake kuwa amepokea mlungula wa sh milioni 600 na kukihujumu chama chake.

Bw. Shitambala ambaye amejitosa kwa mara ya pili kuwania ubunge wa Jimbo la Mbeya vijijini na kukosa, mara ya kwanza akituhumiwa kuhujumu chama kwa kukosea kiapo, amesema ameachia ngazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake ufanyike kwa uhuru.

"Nimeamua kuachia ngazi kwa hiari yangu, nimetuhumiwa kuhujumu chama. Nimeambiwa nimehongwa mamilioni ya fedha na CCM ili nikikoseshe ushindi chama changu, naachia ngazi ili uchunguzi dhidi ya tuhuma hizi ufanyike," alisema Bw. Shitambala.

Alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo walimuamini kwa kiasi kikubwa na kuwa wengi wao walijitokeza kumuunga mkono wakiamini kuwa atashinda uchaguzi huo na kwamba kitendo hicho pekee kilitosha kuwathamini wapiga kura wake na kutokubali kuhujumu chama.

Alifafanua kuwa tuhuma dhidi yake zimejenga chuki kwa wapiga kura wake, kwa wanachama wa ngazi ya mkoa na hata taifa na kwamba imefika mahala hata akimpigia simu Mwenyekiti wa Taifa, Bw. Freeman Mbowe hapokei simu yake, jambo ambalo linaonesha tuhuma hizi zimepandikizwa na kukubalika kuwa ni kweli amehujumu chama.

"Inaonesha mbegu hii imepandwa na kukubalika kwa wanachama….nimempigia simu mwenyekiti wangu wa Taifa mara kadhaa lakini hapokei simu yangu, hili si jambo la kawaida, bora niachie ngazi," alisisitiza Bw. Shitambala.

Akizungumzia suala hilo, Bw. Mbowe alisema suala hilo ndio alikuwa analisikia kupitia kwa mwandishi wa habari hizi, na hivyo asingependa kujibishana na kiongozi wake kwenye vyombo vya habari.

Kuhusu kutopokea simu yake, alisema katika kipindi hiki ametingwa na mambo mengi, ikiwamo ya kuweka sawa kambi ya upinzani bungeni, kuweka sawa halmashauri kuhakikisha wanapata mameya, kushughulikia suala la kura za mgombea urais na mengine, ndio maana hata watu wengine wakiwamo waandishi wa habari wamekuwa wakimkosa.

Hata hivyo, alisema kama Bw. Shitambala aliona mwenyekiti hapatikani angeweza kuwasiliana na viongozi wengine waandamizi wa chama, kwa kuwa chama sio Mbowe.

"Vile vile angeweza kunitumia ujumbe mfupi wa maandishi. Mara ngapi hata nyie mnanitafuta lakini siwezi kupokea simu?" alihoji Bw. Mbowe.

Alifafanua kuwa kwa muda mfupi ambao chama hicho kilikuwa mikononi mwake amefanikiwa kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufanikisha kupata majimbo mawili, la Mbeya Mjini na Mbozi Magharibi lakini hata hivyo matunda hayo yote hayaonekani bali kuelekeza tuhuma za kupokea fedha kutoka CCM ilhali yeye binafsi ametumia fedha nyingi katika kampeni za chama mkoani bila kupata nguvu yoyote ya chama makao makuu.

"Nimetumia resources zangu kuimarisha chama Mkoa wa Mbeya, sijapewa fungu lolote kutoka makao makuu kuendeleza chama, leo hii natuhumiwa kuwa nimeuza chama. Mbona yapo majimbo ambayo yalikuwa chini ya CHADEMA na yamepokonywa na CCM lakini hatujasikia kuwa wagombea wake wamepewa fedha," alisema.

Bw. Shitambala alisema kuwa yeye atabaki kuwa mwanachama wa CHADEMA na ataendelea kuwatumikia wananchi kama ambavyo alikuwa anawatumikia kipindi kilichopita, bali anaachia nafasi hiyo ili chama kifanye uchunguzi wa kina kujua kama ni kweli amepokea rushwa na kukihujumu chama hicho.

Akizungumzia sababu za kushindwa katika uchaguzi huo, alisema kuwa ni pamoja na jiografia ya jimbo hilo ambapo kuna baadhi ya kata mawakala ambao waliwaamini waliamua kuchukua rushwa na kukimbia na kwamba chama kinaendelea kufanyia uchunguzi jambo hilo ili kubaini ukweli.

Katibu wa CHADEMA mkoani hapa, Bw. Eddo Makatta alisema kuwa amepokea taarifa hizo kwa mshutuko na kwamba hakutarajia uamuzi kama huu, na kwamba hata hivyo atafikisha taarifa hizo katika vikao vinavyohusika.

6 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 22, 2010 at 9:25 AM

    Huo ni uwajibikaji uliotukuka.Hongera Msomi mwenzangu(Mwanasheria Mwenzangu),Mh.Sambwee Shitambala kwa kuonyesha ukomavu wako wa namna ya kuwajibika kisheria.Hii ni kuonyesha kuwa CHADEMA ni chama makini chenye watu makini na taratibu makini....kama Ulaya vile! CCM na Serikali yao nao waige utaratibu kama wa Shitambala.CHADEMA ni darasa tosha.

    ReplyDelete
  2. Nakuunga Mkono Shitambala hiyo ndiyo sifa kubwa ya kiongozi aliyekomaa kisiasa na kidemokrasia. Kukubali kukaa pembeni ni njia mojawapo ya kumaliza malumbano. Hongera sana. Viva Shitambala, Viva CHADEMA

    ReplyDelete
  3. hiyo ndo demokrasia, ccm wanatakiwa kiuga kutoka kwenu. hongera sana Chadema

    ReplyDelete
  4. Shitambala hiyo ndiyo faida ya unafiki. Umepokea pesa toka ccm kisha ukawasaliti wananchi wako. Dhambii hiyo itakutesa miaka mitano ambayo wananchi watakuwa wanateseka. Unatakiwa kutubu kweli na kurudisha hizo pesa ulizochukua ili usamehewe

    ReplyDelete
  5. NANI ANGEKATAA MIL 600? ANAUMWA?

    ReplyDelete
  6. Nashauri Mwenyekiti Bwana Mbowe umuite na mkae na kuyaongea na kuyafanyia ufumbuzi matatizo yaliyojitokeza huko kwenye jimbo la Mbeya Vijijini na kujua kama ni kweli au si kweli na wala usifunge milango kwa jambo hili, sifa ya kiongozi mzuri ni kwamba kama limetokea jambo hukurupuki na kushtumu bali unalifanyia utafiti na kujua ukweli wake kama Shitambala ana makosa au hana na apewe haki yake. CHADEMA IDUMU MILELE

    ReplyDelete